1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani itashirikiana na Tanzania kutunza mazingira.

Veronica Natalis16 Machi 2023

Ujerumani imesema itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya utunzaji wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kulinda ikolojia za bayoanuai kwenye hifadhi mbalimbali za taifa.

Kilimandscharo
Picha: picture-alliance/dpa/R. Schnoz

Hayo yamesemwa na mwakilishi wa balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Bi Ursula Thraen, katika hafla ya maadhimisho ya miaka 50 ya hifadhi ya Kilimanjaro, iliyofanyika katika mkoa wa Kilimanjaro uliopo kaskazini mwa Tanzania. 

Maadhimisho haya yanakuwa ni historia nyingine katika shughuli za uhifadhi na utalii inayowekwa nchini Tanzania, tangu kuasisiwa kwake na baba wa taifa hilo la Afrika Mashariki hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Akimwakilisha makamu wa Rais wa Tanzania Dokta Philip Mpango, Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Mohamed Mchengerwa katika hotuba yake mbali na kusema kwamba Ujerumani imekuwa mshirika mkubwa katika shughuli za uhifadhi na utalii, lakini pia amesisitiza kuwa nchi yake itaendeleza hifadhi za maliasili na wanyamapori ili kuenzi juhudi za hayati Mwalimu Nyerere na kwa faida ya vizazi vijavyo.

Hifadhi ya Kilimanjaro ni miongoni mwa hifadhi 22 nchini Tanzania na ya pili kwa ukusanyaji wa mapato baada ya hifadhi ya Serengeti. Umaarufu wa hifadhi ya Kilimanjaro unatokana na uwepo wa vivutio mbalimbali ikiwemo uwepo wa vilele vitatu: kilele cha Kibo ambacho kirefu zaidi, pamoja na kilele cha Mawenzi na Shira.

Shughuli za kibinadamu zatajwa kuharibu mazingira ya mlima Kilimanjaro

Mlima KilimanjaroPicha: Zoonar.com/kavram/picture alliance

Hata hivyo, shughuli za kibinadamu kama vile kilimo zinatajwa kuchangia uharibifu wa mazingira katika mlima huo, pamoja na kutishia uhai wa uoto wa asili katika maeneo yanayouzunguka mlima huo. Ursula Thraen-Lardi, mwakilishi wa balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, anasema Ujerumani itaendelea kushirikiana na Tanzania hasa uwekezaji katika eneo la tafiti.

"Tanzania imekuwa miongoni mwa washirika wetu wakubwa barani Afrika, na kipaumbele chetu ni katika bayoanuai, afya na maji. Katika eneo la bayoanuai pekee Ujerumani kwa sasa imetenga Euro milioni 150 ambazo zitaelekezwa katika mbuga ya Serengeti, hifadhi ya taifa ya Nyerere, Selous pamoja na Katavi,” alisema Bi Lardi.

Pamoja na mambo mengine hafla hii pia imetumika kuutanganza utalii wa Tanzania kupitia Mlima Kilimanjaro, ili kuendeleza lengo la nchi hiyo kufikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025. Sherehe zimebebwa na kaulimbiu inayosema "Mlima Wetu Fahari Yetu.”

Mwandishi: Veronica Natalis, DW, Kilimanjaro.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW