1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Germany: Jinsi ya kuilinda Mahakama ya Juu

6 Machi 2024

Madikteta hujaribu kubana uwezo wa mahakama kuu za nchi zao. Sasa, wakati ambapo makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia yanazidi kuimarika nchini Ujerumani wanasheria wanakusudia kuulinda mhimili huo wa demokrasia.

Mahakama ya kikatiba ya shirikisho la Ujerumani
Mahakama ya kikatiba ya shirikisho la UjerumaniPicha: Uwe Anspach/AFP via Getty Images

Wanasheria na wanasiasa nchini Ujerumani wanaandaa mipango ili kuilinda mahakama ya juu ya nchi dhidi ya  uwezekano wa kuhujumiwa, endapo serikali zinazopinga demokrasia zitaingia madarakani mnamo siku za usoni, baada ya kutukia utata katika nchi mbili ambazo pia ni wanachama wa Umoja wa Ulaya. nchi hizo ni Hungary na Poland.

Mafanikio ya chama cha mrengo mkali wa kulia, kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani, (AfD) kinachozingatiwa kuwa  na pande zinazotishia katiba ya nchi, yamewatanabahisha watu nchini humo.

Soma pia:Ujerumani yakanusha kuitishwa kwa balozi wake Moscow 

Chama hicho kwa sasa kinafikia asilimia 20, nchini kote, katika utafiti wa kura za maoni.

Baraza la shiriklisho ambalo ni tawi la bunge linalowakilisha majimbo yote 16 ya Ujerumani tayari limeshatayarisha mswada wa sheria wenye kurasa 14 kwa lengo la kuweka msingi wa sheria zitakazotumiwa na mahakama ya katiba, kuzizuia serikali zijazo kufanya mabadiliko ya katiba.

Katiba ya Ujerumani inasemaje?

Maandamano ya kupinga chama cha siasa kali cha AfDPicha: Hannes P Albert/dpa/picture alliance

Katiba ya Ujerumani ambayo ni sheria inajumuisha ibara tatu zinazoamua jinsi mahakimu 16 wa mahakama ya katiba wanavyoteuliwa. Kwa sasa nusu ya majaji hao wanateuliwa na bunge la Ujerumani na wengine wanateuliwa na baraza la  shirikisho ambalo ni tawi lingine la bunge linalotokana na majimbo yote 16  ya Ujerumani.

Hata hivyo, kulingana na mswada wa sheria, yapo mapengo ya kutiliwa maanani katika katiba yanayotishia uhuru wa  mahakama. Kwa mfano hakuna ulazima wa kupatikana thuluthi mbili ya kura ili kuwateua majaji wapya. Pia hakuna kikomo cha mihula na kwamba hakuna utaratibu wa kupiga marufuku majaji hao kuteuliwa tena.

Soma pia: Scholz aahidi uchunguzi wa haraka kuhusu udukuzi wa Urusi

Ndiyo kusema endapo serikali ya madikteta itaingia madarakani, mnamo siku za usoni itawezekana kwa madikteta hao kupunguza idadi ya kura zinazohitijika ili kuweza kuwateua mahakimu wanaoegemea upande wa serikali.

Mswada wa sheria wa baraza la shirikisho la Ujerumani unalenga shabaha ya kuondoa uwezekano wa wabunge    wachache au thuluthi moja ya wabunge kuweza kupinga uteuzi wa majaji na hivyo kuivunja nguvu kabisa mahakama ya juu ya nchi.

Sheria za kuteua majaji wapya

Majaji katika mahakama mjini FrankfurtPicha: Kai Pfaffenbach/Pool/AFP

Mgogoro uliosababishwa na mageuzi ya mahakama nchini Poland hivi karibuni, umewapa nguvu wanasheria wengi nchini Ujerumani ya kutafuta njia za kuilinda mahakama ya katiba ambayo ni mahakama ya juu kabisa hapa nchini.

Mgogoro huo wa nchini Poland uliochochea maandamano makubwa, ulianza mnamo mwaka 2015 baada ya chama  tawala cha nchi hiyo, cha "sheria na haki”, (PiS)  kilipolaumiwa kwa kujaza mahakimu wao. Kutokana na kuwa na wabunge wengi, chama hicho kiliweza kubadilisha sheria ili kuwateua majaji wapya.

Soma pia: Jeshi la Ujerumani kwenda bahari ya Shamu

Hata hivyo baadhi ya wataalamu wa masuala ya sheria wanatoa angalizo juu ya mswada wa sheria wenye lengo la kuilinda mahakama ya katiba nchini Ujerumani. Mtafiti mwandamizi kwenye chuo kikuu cha Kiel, Stefan Martini amesema, mageuzi ni jambo zuri lakini inapasa kuzingatia misingi ya sheria.

Mtaalamu huyo amesema kuzifanya sheria ziwe ngumu kubadilishwa sio suluhisho kwa sababu ikiwa serikali ya mrengo mkali inaondoka madarakani na ya kidemokrasia inaingia, serikali hiyo pia itahitaji kuwa na wabunge wengi ili kuweza kubadilisha sera.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi