Ujerumani, na Kenya kuimarisha mafunzo ya Kijerumani
14 Oktoba 2024Hatua hii inalenga kuwaandaa wanafunzi wa vyuo hivyo kwa ajira Ujerumani, hatua itakayowapa fursa nzuri ya kufanya kazi katika taaluma mbalimbali. Hayo yameelezwa na Balozi wa Ujerumani nchini Kenya, Sebastian Groth, wakati wa hafla ya kuadhimisha miaka 60 ya uhusiano kati ya Kenya na Ujerumani iliyofanyika katika makavazi ya Malindi.
Mikakati ya kukuza ujuzi
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi Groth alieleza kuwa vyuo vya kiufundi nchini Kenya vinanufaika pakubwa kutokana na msaada wa mashirika ya Ujerumani. Asilimia 60 ya vyuo hivyo vinapata msaada wa kifedha na kiufundi kutoka kwa mashirika hayo.
Katika jitihada za kuimarisha ujuzi wa vijana wa Kenya, vyuo vikuu vya Nairobi na Kenyatta vimetambuliwa kama vituo maalum vya kufunza wahadhiri lugha ya Kijerumani.
Soma pia: Ujerumani kuruhusu Wakenya zaidi kupata fursa za ajira
Wahadhiri hawa watawafunza wanafunzi kwenye vyuo mbalimbali vya kiufundi nchini ili kuwawezesha kujiandaa kwa ajira nchini Ujerumani.
Groth alisema, “Tutavipa nafasi vyuo vikuu vya Nairobi na Kenyatta vya kuwafunza wahadhiri Kijerumani ili nao wakafunze wanafunzi kwenye vyuo vingi vya kiufundi, ili vijana wanaojifunza taaluma mbali mbali iwe rahisi kwa wanafunzi kupata ajira Ujerumani.”
Ushirikiano kati ya Kenya na Ujerumani una mizizi mirefu na umejumuisha nyanja nyingi kama vile uchumi, elimu, afya, mazingira, na utamaduni. Ushirikiano huu ulianza mara baada ya Kenya kupata uhuru mwaka wa 1960, na tangu hapo, nchi hizi zimeendelea kushirikiana kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi.
Mbunge wa Malindi, Amina Mnyanzi, aliongeza kuwa ushirikiano huo utazidi kuinufaisha Kenya kwa kusaidia vijana kupata ajira za kimataifa. "Kupitia ushirikiano huu, tutawasaidia watu wetu wenye vibali kupata kazi katika sekta kama vile kwenye meli,” alisema Mnyanzi.
Fursa za ajira Ujerumani kwa Wakenya
Ujerumani imeanzisha mpango maalum wa viza za ajira kwa wafanyakazi wenye ujuzi kutoka nchi za nje, zikiwemo Kenya. Viza hii inawawezesha wataalamu wa sekta kama vile teknolojia ya habari, uhandisi, afya, na huduma za kijamii kupata fursa ya kufanya kazi nchini Ujerumani. Mpango huo unalenga kukidhi mahitaji ya soko la ajira la Ujerumani ambalo linahitaji wataalamu wa nyanja mbalimbali.
Soma pia: Ruto atetea rikodi ya uongozi wake wa miaka miwili
Naibu Gavana wa Kaunti ya Kilifi, Flora Chibule, alieleza jinsi Ujerumani ilivyochangia katika kukuza utamaduni wa Kenya, akisema, “Wajerumani wametusaidia upande wa utamaduni, wametutengezea makavazi maeneo ya Rabai ambayo kwa sasa inatumika.”
Kwa jumla, ushirikiano huu unatoa fursa nzuri kwa Wakenya, hasa vijana, kufanya kazi Ujerumani. Hii inatoa matumaini makubwa kwa wahitimu wa vyuo vya kiufundi wanaoazimia kufanya kazi kwenye sekta zenye uhitaji mkubwa kama vile afya, teknolojia, na huduma za kijamii.