1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Ujerumani kuanza tena ushirikiano na UNRWA

24 Aprili 2024

Ujerumani imesema itarejesha ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina huko Gaza, UNRWA.

Mgogoro wa Mashariki ya Kati
Ujerumani inapanga kurejesha ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA Picha: Mahmoud Issa/ZUMAPRESS/picture alliance

Taarifa hiyo ya Ujerumani imetangazwa Jumatano na Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo. Shirika la UNRWA linalotoa msaada wa kiutu huko Gaza linakabiliwa na mzozo mkubwa baada ya Israel kuwatuhumu baadhi ya wafanyakazi wake kuhusika katika shambulizi la Oktoba 7 lililosababisha watu 1,200 kuuawa.

Madai yalisababisha wafanyakazi kusimamishwa kazi

Wafanyakazi kadhaa walisimamishwa kazi kutokana na tuhuma hizo. Katika siku na wiki zilizofuata, nchi 16 wafadhili wakiwemo wafadhili wawili wakubwa Marekani na Ujerumani, zilisitisha ufadhili na kuacha pengo la ufadhili la takribani dola milioni 450.

Uamuzi huo wa serikali ya Ujerumani umechukuliwa baada ya uchunguzi ulioongozwa na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Catherine Colonna kuhusu madai hayo ya Israel, kubaini kwamba Israel haijatoa ushahidi wowote kuthibitisha madai yake kwamba wafanyakazi wa UNRWA ni wanachama wa makundi ya kigaidi.

Majengo yaliyoharibiwa kwa mashambulizi ya Israel huko Nuseirat, Ukanda wa GazaPicha: Majdi Fathi/NurPhoto/picture alliance

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz Jumatano amelishuruku Baraza la Seneti la Marekani kwa kuidhinisha msaada wa kijeshi wa dola bilioni 13 kwa ajili ya vita vya Israel dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas, akisema unapeleka ujumbe mzito kwa maadui wa nchi hiyo.

Baraza hilo pia limeidhinisha takribani dola bilioni 9 kwa ajili ya msaada wa kiutu huko Gaza, ambao watalaamu wanasema inakabiliwa na baa la njaa. Rais wa Marekani Joe Biden leo anatarajiwa kusaini muswada huo.

Msaada wa dharura kwa Israel

Biden amesema msaada huo umekuwa wa dharura zaidi kwa Israel, ambayo ilikumbwa na mashambulizi ambayo hayajawahi kushuhudiwa kutokea Iran.

Naye Mjumbe maalum wa Marekani katika Mashariki ya Kati, David Satterfield amesema hali ya msaada wa kiutu inaimarika huko Gaza, lakini ameonya kuhusu mashambulizi ya Rafah.

"Hatuwezi kuunga mkono operesheni ya ardhini ya Rafah, bila ya kuwa na mpango unaofaa, unaoaminika kuhusu hali ya kiutu, hasa kutokana na ugumu na matatizo ya utoaji wa misaada," alifafanua David.

Wakaazi wakiwa kwenye kifusi cha nyumba iliyoharibiwa kwa vita RafahPicha: Khaled Omar/Xinhua/IMAGO

Huku hayo yakijiri, jeshi la Israel limesema limepeleka vikosi viwili vya akiba kutoka kwenye mpaka wa kaskazini wa Israel hadi Gaza kwa ajili ya operesheni ya kujihami huko Rafah. Aidha, jeshi limesema kwamba linaendelea kuwaondoa Wapalestina wasio na makaazi kutokana na vita, ambao wanahifadhiwa Rafah.

Iran na Pakistan zataka Israel ichukuliwe hatua

Ama kwa upande mwingine, Iran na Pakistan zimelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua dhidi ya Israel, zikisema kuwa imezilenga kinyume cha sheria nchi jirani na maeneo ya kidiplomasia ya kigeni.

Kauli hiyo ambayo inaishutumu Israel kwa kusababisha kuongezeka kwa mzozo kwenye eneo ambalo tayari lina hali tete, imetolewa leo katika taarifa ya pamoja na Waziri ya mambo ya nje ya Pakistan kufuatia ziara ya siku tatu ya Rais wa Iran, Ebrahim Raisi.

(DPA, AFP, AP, Reuters)