1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiUjerumani

Ujerumani kuharamisha kitendo cha kukana uhalifu wa kivita

24 Novemba 2022

Nchini Ujerumani, kukanusha mauaji ya Holocaust ni kosa kisheria. Marekebisho mapya yanalenga kuharamisha kitendo cha kukana uhalifu mwingine wa kivita na mauaji ya halaiki popote yanapotokea duniani.

Berlin Bundestag | Generaldebatte in der Haushaltswoche
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Madai ya uhalifu wa kivita huko Bucha nchini Ukraine, mauaji ya kimbari ya jamii ya Yazidi, ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wayghur nchini China. Orodha ni ndefu ya ukatili katika migogoro duniani kote. Hata hivyo mara kwa mara, baadhi ya watu hupuuza au kukana uhalifu huu kuwa uliwahi kutokea. Wabunge nchini Ujerumani hawataki tena kuvumilia hali hii na wanataka kufanya matamshi kama hayo yaadhibiwe kisheria iwapo yatatumiwa kuchochea chuki au kuvuruga amani ya umma.

Bunge la Ujerumani, Bundestag, lilipitisha muswada wa sheria mwishoni mwa mwezi Oktoba, na Ijumaa hii inatazamiwa kupitishwa katika Baraza la wawakilishi wa majimbo Bundesrat. Kuidhinishwa, kukataliwa, na kubezwa kwa uhalifu wa kivita na matukio ya mauaji ya halaiki sasa itakuwa ni kosa la jinai la uchochezi chini ya kifungu kipya nambari 5 katika kipengele cha sheria ya 130.

Soma zaidi: Ukraine: Je! uhalifu wa kivita unaweza kufafanuliwa kivipi?

Michael Kubiciel, msomi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Augsburg hapa Ujerumani ameiambia DW kuwa hilo linalenga kuwapa mwongozo wenye nguvu watekelezaji sheria kuhusu jinsi na nini wanaweza kuchunguza, lakini zaidi ya yote, ilikuwa ni kukidhi matakwa ya Tume ya Ulaya. Na kuwa hilo sasa limefanyika.

Berlin kulazimishwa kuchukua hatua

Kwa hakika, Ujerumani haikuwa na haraka ya kupitisha sheria hiyo. Agizo la Umoja wa Ulaya la kupambana na ubaguzi wa rangi lilitolewa mwaka wa 2008, na serikali ya Ujerumani ililazimika kuchukua hatua sasa kwa sababu ya tishio la kesi za ukiukaji kutoka kwa Umoja wa Ulaya.

Josephine Ballon, Mwanasheria mkuu wa shirika la HateAidPicha: Andrea Heinsohn Photography

Josephine Ballon, mwanasheria mkuu wa shirika la HateAid, ambalo linalosaidia waathiriwa wa chuki mtandaoni, amefurahishwa na hatua hiyo na kusema mabadiliko hayo yanatokea wakati muafaka. Bi Ballon ameendelea kuwa mambo mengi yanaamuliwa kutokana na mazingira ya vita vya Ukraine na marekebisho hayo yanajiri wakati ambao yanaweza kuwa muhimu sana.

Soma zaidi:Zelenksy aishtumu Urusi kwa kufanya mauaji ya halaiki 

Aziz Epik, Profesa msaidizi wa sheria ya jinai katika Chuo Kikuu cha Hamburg anasema ikitungwa sheria iliyorekebishwa pia itatumika nje ya mtandao huku akibaini kuwa, mabadiliko ya sheria hayatoathiri mjadala wa kweli wa uhalifu chini ya sheria za kimataifa.

Ukosoaji mkubwa baada ya mabadiliko

Bunge la Ujerumani, Bundestag mjini Berlin.Picha: Achille Abboud/IMAGO

Kumekuwa pia na ukosoaji mkubwa kuhusu marekebisho hayo kutoka kwa wasomi wa sheria na wanahistoria. Baadhi walilalamikia ukosefu wa uwazi kwa sababu marekebisho hayo yalipitishwa katika Bunge majira ya jioni, bila taarifa na bila mjadala wa awali. Wengine wanafikiri kifungu hicho cha sheria kinaminya kusipo na ulazima uhuru wa kujieleza.

Soma zaidi: Putin 'sio mshukiwa pekee' katika uhalifu nchini Ukraine

Kubiciel hakubaliani na hilo na anasema ni kelele tu za bure kwa maana hakuna kasoro kwa utaratibu au kwa marekebisho yenyewe. Amedokeza kwamba hata kabla ya hatua hii mpya, kuidhinisha hadharani mauaji ya halaiki ilikuwa ni kinyume cha sheria nchini Ujerumani chini ya sheria dhidi ya "Volksverhetzung," au "matamshi ya chuki dhidi ya watu." Kwa hiyo Kubiciel amesema haoni ukiukwaji wowote mkubwa wa uhuru wa kujieleza.

Mvutano wa sera za kigeni unawezekana

Picha: Autentic Distribution GmbH

Uvamizi wa Ukraine na kauli zilizotolewa nje na ndani ya mtandao zimeonyesha kuwa kujumuisha suala hili la kukana na kubeza uhalifu wa kivita huenda ikawa hatua kubwa na yenye matokeo makubwa kimataifa kwa kuwa linaweza kuwa na athari za kisiasa.

Aziz Epik anadokeza kwamba marekebisho hayo yakipitishwa yanaweza kusababisha "hali tete kwa sera za kigeni" kwa serikali ya Ujerumani. Hii inaweza kutokea kwa mfano, kama mahakama za wilaya za Ujerumani zinapaswa kutoa hukumu kwa njia isiyo ya moja kwa moja kufuatia uhalifu unaofanywa nchini China chini ya sheria za kimataifa.

Serikali ya Ujerumani itatakiwa kuchukua msimamo wa wazi zaidi kuliko inavyofanya hadi sasa.

Soma zaidi:UN: Matamshi ya chuki yanachochea vita vya Ethiopia 

Ikiwa Bundesrat itaidhinisha marekebisho hayo, mahakama za Ujerumani zitaweza sasa kutoa uamuzi kuhusu uhalifu wa sasa wa kivita. Josephine Ballon kutoka shirika la HateAid anasema ni muhimu hilo lifanyike kwa hali ya tahadhari. Lakini anadhani kwamba itakuwa hivyo kwa sababu suala la "uchochezi wa chuki" ni tata sana.

Maneno mengi ndani yake yanaacha nafasi kubwa ya kila mmoja kutoa tafsiri yake na ndiyo maana waendesha mashtaka na mahakama tayari wako makini sana na wanaruhusu tu mashtaka na kesi kuletwa katika idadi ndogo na katika kesi zilizothibitishwa vyema. Iwapo kesi hizo zitaongezeka, ikiwa mashirika ya kiraia na watu binafsi watatumia pia kifungu hiki kipya cha sheria, basi hilo litadhihirika tu baada ya miezi au miaka kadhaa.