1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UhalifuUjerumani

Ujerumani kuimarisha ulinzi baada ya shambulio la Magdeburg

21 Desemba 2024

Majimbo na majiji kadhaa nchini Ujerumani yametangaza kuimarisha usalama katika masoko ya Krismasi kufuatia shambulio la Magdeburg lililoua watu 5 na kujeruhi wengine 200.

Polisi wa Ujerumani wakiimarisha ulinzi kwenye soko la Krismasi la Magdeburg
Polisi wa Ujerumani wakiimarisha ulinzi kwenye soko la Krismasi la MagdeburgPicha: Ronny Hartmann/AFP

Katika mji mkuu, Berlin, wizara ya mambo ya ndani ya jimbo hilo imesema polisi wataongeza uwepo wao katika soko la Krismasi la mji huo mkuu kama hatua ya tahadhari.

Majimbo mengine, yakiwemo Hesse, Bremen, Lower Saxony, Rhineland-Palatinate na Schleswig-Holstein yameeleza pia kuimarisha hatua za kiusalama.

Jiji la mashariki la Leipzig limetangaza kuwa sherehe za gwaride kwenye mlima itafanyika Jumamosi kando ya soko la Krismasi, na kwamba kutakuwepo maafisa na magari ya ziada ya polisi.

Markus Lewe, Rais wa Jumuiya ya Miji ya Ujerumani, amesema miji hiyo inazingatia kwa umakini mkubwa taarifa ya onyo inayotolewa na mamlaka kuhusu uwezekano wa kutokea vitendo vya ugaidi na hivyo kuchukua mara kwa mara hatua za ziada za usalama zinazohitajika.

Soma pia: Tukio la Magdeburg: Idadi ya vifo yaongezeka, Kansela Scholz autembelea mji huo

Wakati huo huo, Lewe ameongeza kuwa licha ya kiwango cha juu cha juhudi za kiusalama, ni vigumu kuhakikisha ulinzi kwa asilimia mia moja.

Kutokana na miito ya baadhi ya watu waliotaka masoko ya Krismasi yafungwe mapema, Albert Ritter, Mwenyekiti wa Chama cha Maonyesho cha Ujerumani amesema hatua hiyo ingetoa picha mbaya.

"Jinsi tunavyosherehekea Krismasi, ni ishara inayoonyesha tunavyoishi kwenye demokrasia na tunavyoishi pamoja kwa amani, " Ritter aliliambia gazeti la Rheinische Post.

Dakika moja ya ukimya itashuhudiwa katika masoko yote ya Krismasi nchini Ujerumani siku ya Jumamosi saa moja usiku pamoja na kwenye mechi zote za soka la Ujerumani Bundesliga.

Saudia iliionya Ujerumani kuhusu mshukiwa huyo

Soko la Krismasi la Magdeburg nchini Ujerumani kulikotokea shambulio hiloPicha: Ronny Hartmann/AFP

Duru za usalama za Saudi Arabia zimesema kuwa serikali mjini Riyadh iliionya Ujerumani kuhusu mshukiwa wa shambulio la soko la Krismasi la Magdeburg na kwamba serikali ya Ujerumani haikujibu.

Hayo ni kulingana na mashirika ya habari ya Dpa, Reuters na jarida la Der Spiegel, yaliyotaja vyanzo kadhaa vinavyosema kuwa mamlaka za Ujerumani zilitahadharishwa kuhusu mwanaume huyo takriban mwaka mmoja uliopita, lakini aina ya onyo hilo kwa sasa haijulikani. Idara ya ujasusi wa ndani ya Ujerumani hadi sasa imekataa kuzungumzia suala hilo.

Soma pia: Ujerumani: Gari laparamia watu soko la Krismasi mjini Magdeburg

Mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 50 na ambaye sasa anashikiliwa na polisi, ni muislamu wa madhehebu ya Shia kutoka mji wa Al-Hofuf mashariki mwa Saudi Arabia na aliwasili kwa mara ya kwanza nchini Ujerumani mwaka 2006 na baadaye aliomba na kupewa ukimbizi mwaka 2016.

Washia ni wachache nchini Saudia, wakiwa ni karibu asilimia 10% tu katika taifa hilo lenye waumini wengi wa madhehebu ya Sunni. Kumekuwa na ripoti za mara kwa mara za ubaguzi dhidi ya WaShia huko nchini Saudi Arabia.

Rais wa Ujerumani aongoza ibada ya kumbukumbu

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani (kushoto) akiwa na Kansela Olaf ScholzPicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Rais Frank-Walter Steinmeier wa Ujerumani alihudhuria ibada ya kumbukumbu Jumamosi jioni mjini Magdeburg ili kuomboleza watu walipoteza maisha katika shambulio la kutumia gari lililotokea kwenye soko la Krismasi siku ya Ijumaa.

Ibada hiyo itafanyika kwenye kanisa kuu la mji huo. Mapema siku ya Jumamosi, Kansela Olaf Scholz  aliutembelea mji huo kujionea eneo mkasa ulipotokea na kutoa salamu zake za rambirambi kwa wafiwa na pole kwa waliojeruhiwa.

Ijumaa jioni, mwanaume mmoja mwenye asili ya Saudi Arabia alilivurumisha gari kwa makusudi kwenye umati wa watu waliokuwa sokoni hapo na kusababisha vifo vya watu 5 na kujeruhi wengine zaidi ya 200.

Mkasa huo kwenye mji wa Magdeburg uliopo umbali wa kiasi kilometa 150 magharibi mwa mji mkuu Berlin, umezusha simanzi kote Ujerumani na barani Ulaya.

(Vyanzo: DPA, Reuters, AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW