Ujerumani kuipatia Ukraine mfumo wa ziada wa ulinzi wa anga
13 Aprili 2024Matangazo
Hayo yameelezwa hivi leo na wizara ya Ulinzi ya Ujerumani. Taarifa ya wizara hiyo imesema kutokana na kuongezeka kwa hujuma za anga za Urusi, serikali mjini Berlin imefikia uamuzi wa kuipiga jeki Ukraine kuimarisha uwezo wake wa kujilinda.
Uamuzi huo umetangazwa katika wakati mkuu wa majeshi wa Ukraine, Oleksandr Syrsky, amesema hii leo kwamba hali kwenye mstari wa mbele wa mapambano mashariki mwa nchi yake imezidi kuwa mbaya.
Kamanda huyo amesema hilo linatokana na kupamba moto kwa mashambulizi ya Urusi inayotumia silaha za kiwango cha juu. Utawala mjini Kyiv unalalamikia kucheleweshwa kwa msaada wa kijeshi kutoka mataifa ya Magharibi kama sababu ya hali hiyo.