1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kujadili kupunguza vikwazo vya virusi vya corona

Yusra Buwayhid
6 Mei 2020

Ujerumani kufungua tena shule na kuruhusu mechi za soka mwezi Mei, kulingana na rasimu ya makubaliano iliyoonekana na vyombo vya habari.

Bund-Länder-Runde: Weitere größere Lockerungen wohl noch offen
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

 Kansela Angela Merkel atayajadili hayo Jumatano na mawaziri wakuu wa majimbo yote 16. Merkel amekuwa akifanya mazungumzo ya mara kwa mara na viongozi wa majimbo yote tangu kuzuka kwa janga la ugonjwa wa COVID-19, lakini kupungua kwa maambukizi nchini humo kumeyachochea baadhi ya majimbo kulegeza vikwazo vya tahadhari bila ya ridhaa ya Merkel, kutokana na kwamba sheria inayaruhushu kufanya hivyo.

Katika ripoti iliyoonekana na shirika la habari la dpa pamoja na mashirika mengine kadhaa kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo, serikali ya shirikisho la Ujerumani imesema kwa kiasi kikubwa serikali za majimbo zitapewa jukumu hilo la kupunguza vikwazo vya kuzuia kuenea kwa maambukizi.

Soma zaidi:Siku 100 tangu kisa COVID-19 kuthibitishwa Ujerumani

Rasimu hiyo ya makubaliano inasema, serikali ya shirikisho ya Merkel na serikali za majimbo yote16 zimekubaliana maduka yote yatafunguliwa tena na baadhi ya michezo itaanza kuruhusiwa tena lakini chini ya masharti maalumu. Shule nazo zitafunguliwa tena kwa wanafunzi wote, na shule za chekechea zitaruhusiwa kupokea wanafunzi kuanzia Mei 11. Majimbo hayo pia yamepewa uhuru wa kuamua juu ya kufungua tena mikahawa, hoteli na sehemu nyingine zinazotoa huduma kwa umma.  

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Getty Images/AFP/K. Nietfeld

Ligi Kuu ya Kandanada Bundesliga kuanza Mei 15

Baadhi ya majimbo nchini Ujerumani yanataka Ligi Kuu ya Kandanda ya Ujerumani Bundesliga ianze tena mnamo Mei 15, na watu wawili walio karibu na maandalizi hayo wameliambia shirika la habari la reuters kwamba kuna uwezekano mkubwa wa ruhusa kutolewa na michezo ya soka kuanza tena wiki ijayo.

Ili kuzuia kutokea wimbi jingine tena la maambukizi, serikali ya shirikisho pamoja na za majimbo zimekubaliana katika mazungumzo ya awali kwamba iwapo idadi ya maambukizi mapya itaongezeka tena baada ya kulegezwa vikwazo hivyo, basi lazima virudishwe tena haraka.

Idadi waliyokubaliana ni pale maambukizi mapya katika wilaya yatakapopindukia 50 kati ya wakazi 100,000 katika kipindi cha siku saba.

Ujerumani ni taifa lililofanikiwa zaidi kuliko mataifa mengine makubwa ya Ulaya katika kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya corona. Kulingana na data za leo Jumatano za Taasisi ya udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani Robert Koch, idadi ya maambukizi ya virusi vya corona iliyothibitishwa imeongezeka kwa visa 947 na kufika hadi maambukizi ya watu 164,807. Aidha idadi ya vifo vilivyotokana na maambukizi hayo ya virusi vya corona hadi sasa imefika 6,996.

Vyanzo: (dpa,afp,rtre)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW