1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kulegeza kwa hatua vizuizi vya COVID-19

4 Machi 2021

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametangaza hapo jana mpango wa kulegeza vizuizi va kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, ikiwa ni pamoja na masharti ya kufungua upya biashara.

Deutschland Coronavirus l Kabinettssitzung - Merkel und Braun
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Wakati hatua hiyo ikichukuliwa, shirika la ndege la nchini humo la Lufthansa limetangaza kupata hasara ya dola bilioni 8.1 kwa mwaka jana kutokana na vizuizi vilivyoathiri pakubwa safari zake. 

Kansela Merkel ametangaza mpango huko baada ya mkutano uliodumu kwa muda wa masaa zaidi ya tisa na wakuu wa majimbo 16 ya shirikisho jana Jumatano.

"Leo tunaweza kuzungumzia kuhusu matumaini ya kuelekea awamu mpya kwa sababu kwa pamoja tumefanikiwa pakubwa hapa nchini mwetu katika kipindi cha miezi michache iliyopita."

Soma Zaidi: Merkel: Maambukizi mapya ya COVID-19 yanapungua Ujerumani

Kansela Merkel kukutana na wakuu wa majimbo kuhusu COVID-19

Hata hivyo serikali ya shirikisho ilitangaza kwamba kizuizi cha kufunga shughuli kimeongezwa hadi Machi 28.

Mpango huo utahusisha hatua tano kuanzia ngazi ya eneo hadi jimbo. Na kila hatua mpya itakuwa inaanza kutekelezwa baada ya siku 14, ikiwa kiwango cha maambukizi cha jimbo kitadhibitiwa ama kupungua. Chini ya mkakati huo, kutakuwepo na uwezekano wa baadhi ya maeneo kurudishwa kwenye ufungwaji wa shughuli iwapo kutarekodiwa visa 100 kati ya watu 100,000 vya maambukizi kwa siku tatu mfululizo katika kipindi cha wiki moja.

Hatua ya kwanza imehusisha kufunguliwa shule, vituo vya kulelea watoto na saluni, huku hatua ya pili ikiwa ni pamoja na kufunguliwa kwa maduka ya vitabu na maua kwa masharti ya mtu mmoja katika eneo la mita za mraba 10. Hatua ya tatu, itahusu kufunguliwa kwa bustani za kawaida na za wanyama na biashara za rejareja.

Biashara nyingi zimefungwa nchini Ujerumani kutokana na janga la COVID-19Picha: Andreas Rentz/Getty Images

Hatua ya nne, itakayoanza Machi 22 kulingana na mpango huo iwapo kiwango cha maambukizi kitasalia chini ya 50, majumba kama ya kufanyia matamasha, sinema na maigizo pia yatafunguliwa. Na kwenye hatua ya tano kuanzia Mei 5 watu wataruhusiwa kukusanyika na vizuizi vya michezo vitaondolewa.

Huku hayo yakiendelea, shirika la ndege la Ujerumani Lufthansa limesema hii leo kwamba limepata hasara ya kiwango cha juu kabisa cha dola bilioni 8.1 kwa mwaka 2020, kutokana na vizuizi vya COVID-19 vilivyolilazimu kusitisha safari zake. Shirika hilo kubwa kabisa la ndege barani Ulaya limesema linataraji kupata hasara nyingine tena kwa mwaka huu ingawa itakuwa ni ndogo ikilinganishwa na mwaka jana. 

Katika hatua nyingine, utafiti uliochapishwa na taasisi ya Kekst CNC hapo jana umeonyesha nusu ya Wajerumani wanaamini kwamba Umoja wa Ulaya haukufanya vizuri katika mchakato wa utoaji wa chanjo. Uchunguzi huo umenukuu asilimia 51 ya watu waliohojiwa ambao walisema taasisi za Umoja huo zilifanya vibaya sana katika mchakato huo. Matokeo ya uchunguzi huo yanahusisha pia asilimia 35 ya Wafaransa na 24 ya raia wa Sweden waliohojiwa.

Rais wa Ghana, Nana Akuffo Ado, akiwa katika kituo cha kupatia chanjo baada ya taifa hilo kupokea chanjo chini ya COVAXPicha: Information ministry of Ghana

Barani Afrika, mataifa zaidi yanaendelea kupokea dozi za chanjo kupitia mpango wa kimataifa wa kuzisambazia dozi wa COVAX. Pamoja na Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Senegal na Lesotho pia zimepokea dozi za chanjo.

Soma Zaidi:Kenya hatimaye yapokea chanjo ya corona

Pamoja na hatua hiyo ya kutia matumaini, mkurugenzi wa kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani humo John Nkengasong ametoa onyo kwamba bara hilo litatambulika kama bara la COVID , iwapo halitafanikiwa kufikia kwa haraka lengo lake la kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya idadi ya watu wake wapatao bilioni 1.3

Na huko Austria, taifa hilo linataraji kupokea chanjo za ziada ya BioNTech Pfizer kama sehemu ya mkakati wa Umoja wa Ulaya wa kuisaidia kukabiliana na mlipuko wa virusi vinavyojibadilisha vilivyotokea nchini Afrika Kusini ambavyo kwa kiasi kikubwa vimeathiri jimbo la Tyrol, kaskazini mwa Austria.

Kansela Sebastian Kurz aliwaambia waandishi wa habari kwamba lengo lao ni kuhakikisha wanapambana na kitisho hicho si tu Tyrol bali kote nchini Austria.

Mashirika: DW/RTRE

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW