1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kulegeza masharti kwa wasafiri kutoka Uingereza

Zainab Aziz Mhariri:Yusuf Saumu
6 Julai 2021

Ujerumani italegeza masharti kwa wasafiri kutoka Uingereza na nchi nyingine kadhaa. Watu waliopata chanjo kamili na wale wanaoweza kuthibitisha kwamba waliugua na kupona corona hawatalazimika kukaa karantini.

UK Besuch der deutschen Bundeskanzlerin Angela Merkel
Picha: David Rose/Daily Telegraph/empics/picture alliance

Serikali ya Ujerumani kutokana na ushauri wa taasisi ya Robert Koch ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza inatarajiwa kulegeza masharti kwa wasafiri kutoka nchi kadhaa ikiwa pamoja na Uingereza, India, Ureno, Urusi  na Nepal. Ujerumani iliweka hatua kali za udhibiti kutokana na mlipuko wa maambukizi ya virusi vya aina mpya vya Corona vinavyoitwa Delta.

Soma Zaidi:Uingereza kulegeza sheria kuhusu corona

Uingereza iliwekwa kwenye orodha ya masharti makali tangu mwishoni mwa mwezi Mei na kufuatiwa na Urusi na Ureno. Watu kutoka nchi hizo walipaswa kujiweka karantini kwa muda wa wiki mbili mara baada ya kuwasili nchini Ujerumani. Kunzia sasa wasafiri kutoka nchi hizo au wajerumani wanaorejea nyumbani kutoka kwenye nchi hizo mradi wawe wameshapa chanjo kamili na wale ambao hawajapata chanjo zote mbili watapaswa kujitenga kwa muda wa siku 10 tu. Uamuzi wa kulegeza hatua kali umechukuliwa baada ya kansela wa Ujerumani Angela Merkel kufanya ziara nchini Uingereza wiki iliyopita. 

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Michael Sohn/AP Photo/picture alliance

Wakati huo huo waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameelezea mipango ya serikali yake ya kuondoa vizuizi vilivyowekwa hapo awali nchini mwake kwa ajili ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.  Kwenye hatua mpya zitakazotangazwa ni pamoja na kuacha kuvaa barakoa na kuweka umbali wa mita moja kati ya mtu na mtu. Waziri Mkuu wa Uingereza amesema amri hizo zitalegezwa kuanzia Julai 19, na amewahimiza waingereza juu ya uwajibikaji kwa kila mtu binafsi badala ya amri za serikali.

Ujerumani itaendelea kuweka masharti makali ya udhibiti kwa nchi kadhaa za Afrika na Amerika ya Kusini. Zilizomo katika orodha hiyo ni Afrika Kusini, Botswana, Eswatini, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia na Zimbabwe. Uamuzi huo utaanza kutekelezwa rasmi hapo kesho Jumatano. 

Kushoto: Kansela wa Ujerumani Angela Merkel. Kulia: Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson.Picha: Stefan Rousseau/PA/picture alliance

Kiwango cha maambukizi sasa ni cha chini nchini Ujerumani. Kwa wastani katika kila watu laki moja ni watano tu wanaokumbwa na maambukizi ya corona.

Kwingineko Australia hapo jana Jumanne ilikanusha madai kutoka kwa serikali ya China kwamba inaingilia kati utoaji chanjo zinazotoka China huko Papua New Guinea. Makabiliano hayo kati ya China na Australia kuhusu chanjo yanaashiria mpasuko mwingine katika uhusiano wa nchi hizo mbili, ambao uliporomoka hapo mwaka jana.

Vyanzo:/RTRE/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW