Ujerumani kuondoa marufuku ya kusafiri kwa nchi 26
3 Juni 2020Uamuzi huo uliofikiwa Jamatano na baraza la mawaziri wa Ujerumani, utaongeza matumaini ya kufufua tena uchumi wa barani Ulaya unaotokana na utalii ambao umeathirika kutokana na mripuko wa janga la virusi vya corona na vizuizi vilivyowekwa kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amesema marufuku ya safari iliyowekwa nchini Ujerumani Machi 17 dhidi ya nchi mbalimvali duniani, itaondolewa katika nchi 26 wanachama wa Umoja wa Ulaya, isipokuwa Uhispania ambako maafisa wameweka vikwazo kwa wageni hadi Juni 21. Hata hivyo, Maas amewaonya Wajerumani kutokimbilia kusafiri.
"Najua uamuzi huu unaamsha matumaini makubwa na matarajio, lakini pia ninataka kusema tena; tahadhari ya safari sio sawa na marufuku ya kusafiri, na maelezo yaliyotolewa kuhusu safari sio lazima yawe mwaliko wa kusafiri," amesema Maas.
Soma zaidi: Italia, Ujerumani zafunguwa tena mipaka
Uingereza na nchi nyingine tatu zisizo wanachama wa Umoja wa Ulaya washirika wa kundi la eneo la usafiri huru la Schengen za Iceland, Uswisi na Liechtenstein, pia zitaondolewa kwenye marufuku ya safari. Kama ilivyo kwa Uhispania, Norway haiko kwenye orodha hiyo.
Uamuazi huo unamaanisha kuwa marufuku ya kusafiri inaweza ikaanzishwa tena kutegemea na idadi ya maambukizi mapya kwenye nchi hizo.
Mpango wa uwokozi
Wakati hayo yakijiri viongozi wa serikali ya muungano ya Ujerumani wameanza tena mazungumzo kuhusu mpango mkubwa wa uwokozi ili kusaidia kufufua uchumi ulioathirika kutokana na mripuko wa virusi vya corona.
Mazungumzo ya jana usiku mjini Berlin hayakufikia hitimisho. Mpango huo ambao huenda ukawa na thamani ya Euro bilioni 80, utakuwa ni nyongeza ya bajeti kubwa ya kukabiliana na virusi vya corona iliyopitishwa mwezi Machi.
Wakati huo huo, mashirika kadhaa ya habari yameripoti kuwa idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa COVID-19 nchini Uingereza imezidi 50,000. Hata hivyo Chuo Kikuu cha Johns Hopkins kimerekodi takwimu za serikali ambazo ni vifo 39,452.
Soma zaidi: Merkel: Ujerumani imefaulu mtihani wa janga la virusi vya corona
Nalo Shirika la Wauguzi Ulimwenguni, ICN limesema kuwa zaidi ya wauguzi 600 duniani wamekufa kutokana na virusi vya corona na wafanyakazi wengine wa huduma za afya wanaokadiriwa kuwa 450,000 wameambukizwa virusi hivyo.
Rais wa Urusi, Vladmir Putin ametangaza kuwa hana mpango wa kushiriki katika mkutano wa kilele ulioandaliwa na Uingereza kuhusu uwezekano wa kupatikana chanjo ya virusi vya corona utakaofanyika kwa njia ya mtandao.
Vyanzo: DPA, AP, AFP, DW