1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuongeza kasi ya kuwarudisha wahamiaji makwao

26 Agosti 2024

Kansela Olaf Scholz ameutembelea mji wa Solingen baada ya raia wa Syria kuwashambulia na kuwauwa watu watatu kwa kutumia kisu. Shambulio hilo limeibua mijadala juu ya sera ya uhamiaji nchini Ujerumani.

Ujerumani Solingen | Olaf Scholz awakumbuka wahanga wa mashambulio ya kisu
Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Henning Kaiser/REUTERS

Kansela Scholz aliweka shada la maua kwenye eneo la shambulizi katika mji huo wa Solingen. Shambulio hilo lilitokea Ijumaa jioni wakati wa tamasha la kusherehekea maadhimisho ya miaka 650 ya jiji hilo.

Wanaume wawili, wenye umri wa miaka 67 na 56, na mwanamke aliyekuwa na umri wa miaka 56 waliuawa. Watu wanane walijeruhiwa, na wanne kati yao wamo katika hali mahututi kulingana na msemaji wa polisi wa Solingen.

Marcel Fiebig, msemaji wa polisi wa mji wa Solingen Picha: DW

Katika hotuba yake, kansela wa Ujerumani alionyesha hasira yake dhidi ya watu wenye misimamo mikali. Scholz ameahidi kuimarisha sheria za silaha na kukabiliana na wahamiaji haramu. Amesema shambulio hilo baya la kisu la wiki iliyopita ni kitendo cha kigaidi dhidi ya wote.

Soma Pia: Mshukiwa wa shambulio la Solingen kufikishwa mahakani Karlsruhe 

Shambulio hilo limezusha mjadala kuhusu uhamiaji wakati ambapo uchaguzi unakaribia katika majimbo mawili ya Ujerumani Mashariki ya Saxony na Thuringia.

Mashambulizi katika mji wa Solingen yameongeza ukosoaji kwa serikali ya kansela Olaf Scholz katika kushughulikia maswala ya uhamiaji. 

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia,cha AfD, kinachojiita chama mbadala kwa Ujerumani na kinachopinga wahamiaji kimezishutumu serikali ya sasa na iliyotangulia kwa kusababisha machafuko kutokana na kuruhusu wahamiaji wengi kuingia nchini humo.

Mratibu wa tamasha la Solingen, Philipp MüllerPicha: Thomas Banneyer/dpa/picture alliance

Kiongozi mwenza wa chama hicho cha AfD, Alice Weidel, ametoa wito wa kuacha kuwadekeza wahamiaji, na pia kufuta muda wa miaka mitano kwa wahamiaji kupata uraia wa Ujerumani.

Wakati huo huo, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha CDU Friedrich Merz, ameitaka serikali kuacha kuwapokea wakimbizi kutoka Syria na Afghanistan.

Msemaji wa kansela wa Ujerumani Steffen Hebestreit amesema katika mkutano wa waandishi wa habari kwamba kusimamishwa kabisa maombi ya hifadhi kutoka kwa raia wa nchi hizo hakuambatani na katiba ya Ujerumani.

Soma Pia: Mauaji ya Solingen na ustawi wa kina mama wadogo Ujerumani  

Kwa upande mwingine, serikali ya kansela Scholz tayari ilikuwa chini ya shinikizo la kuanzisha tena zoezi la kuwarudisha nyumbani raia wanaotoka Afghanistan na Syria, baada ya kusimama kwa miaka kadhaa.

Kiongozi mwenza wa chama cha AfD, Alice WeidelPicha: Revierfoto/dpa/picture alliance

Wajumbe wa muungano unaotawala walitoa wito kama huo wa kuchukuliwa hatua kali za kuwafukuza wakimbizi baada ya raia wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 25 alipomdunga kisu afisa mmoja wa polisi katika mji wa Mannheim mnamo mwezi Mei.

Vyombo vya usalama vya Ujerumani vimekuwa katika hali ya tahadhari tangu vita vya Gaza vilipoanza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kuishambulia Israel.

Vyanzo: DPA/AFP