Ujerumani Kupata rais mpya
18 Machi 2012Gauck anachaguliwa baada ya kupata kuungwa mkono kutoka katika vyama vya kisiasa nchini humo, lakini mwanathiolojia huyo huenda akawa mshirika mgumu kwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Merkel amemkubali Gauck kwa shingo upande kushika wadhifa huo ambao ni wa heshima tu , baada ya mshirika katika serikali yake ya mseto kujiunga na vyama vya upinzani mwezi uliopita kumuunga mkono katika hatua ya kuchukua nafasi ya Christian Wulff, aliyejiuzulu kufuatia kuhusika katika kashfa ya kupata takrima ya fedha.
Tofauti na Wulff, ambaye ni mbunge wa zamani kutoka chama tawaka cha kansela Merkel cha CDU, Gauck hana mafungamano na chama chochote, Lakini anafahamika kwa kusema kile anachofikiria , kwa hali ambayo ni kama anahubiri, hata katika masuala yenye utata.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na shirika la Infratest siku ya Jumamosi, asilimia 80 ya Wajerumani wanamuamini Gauck, mchungaji wa zamani wa kanisa la Lutheran na mwanaharakati wa kupigania haki za binadamu. Hata hivyo theluthi mbili wamesema kuwa wanafikiria atakuwa ni rais ambaye vyama vya siasa havitajisikia kuwa katika hali ya utulivu nchini humo.
Nchini Ujerumani, rais anachaguliwa sio na wapiga kura wa kawaida lakini huchaguliwa na baraza maalum lenye wajumbe 620 kutoka bunge la Ujerumani , Bundestag na idadi kama hiyo ya wawakilishi wa majimbo 16 ya Ujerumani .Kuchaguliwa kwa Gauck ni hakika kwasababu anaungwa mkono na vyama vitatu ikiwa ni pamoja na chama tawala cha CDU na kile cha upinzani cha SPD na kijani.
"Tunatarajia wingi mkubwa kwa Gauck" amesema Frank-Walter Steinmeier, kiongozi wa chama cha upinzani cha Social Democratic. Mpinzani wake pekee ni Beate Klarsfeld, mwenye umri wa miaka 73, mwanaharakati anayepambana dhidi ya Wanazi, ambaye ameteuliwa na chama kidogo cha Die Linke.
Kiongozi wa taifa la Ujerumani hana madaraka makubwa ya kiutendaji lakini anatarajiwa kutoa uongozi wa kimaadili , jukumu ambalo Gauck , ambaye ni mtu mashuhuri katika vuguvugu la maandamano ya amani ambayo yamesababisha kuanguka kwa ukuta wa Berlin mwaka 1989, anaonekana kulimudu sana.
Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE
Mhariri : Amina Abubakar.