Ujerumani kupeleka silaha kwa Wakurdi
1 Septemba 2014Silaha zitakazopelekwa kwa Wakurdi ni pamoja na magurunedi yanayorushwa kwa roketi, makambora ya kuteketezea vifaru na bunduki bubu. Wizara ya ulinzi ya Ujerumani imeeleza kuwa ni kuutimiza wajibu wa kibinadamu na kutetea maslahi ya amani, kuwasaidia wale wanaoandamwa ili waweze kuikomesha mipango ya kundi la magaidi wa dola la kiislamu, IS.
Akiyafafanua hayo Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesisitiza umuhimu wa kuikomesha mipango ya magaidi wa dola ya kiislamu. Amesema ikiwa itashindikana kuwazuia wapiganaji wa kundi la magaidi wa dola la Kiislamu IS hali tete katika Mashariki ya Kati itayumba zaidi na eneo lote linaweza kuwaka moto.
Waziri Steinmeier na mwenzake wa ulinzi, Ursula von der Leyen wamesema kuwa uamuzi wa Ujerumani wa kuwapelekea silaha Wakurdi wa Irak umeratibishwa na washirika wa Ujerumani wa nchi za magharibi. Mnamo mwezi huu ndege ya kwanza ya jeshi la Ujerumani itatua Irak ikiwa na shehena ya silaha.
Misaada ya kibinadamu pia itapelekwa
Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen ameeleza kuwa silaha ambazo Ujerumani imeahidi kuzipeleka kwa Wakurdi zitatolewa kwa awamu kadhaa, na hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu askari alfu nne watakuwa wameshamiri kwa silaha hizo. Ujerumani pia imeahidi kuongeza misaada ya kibinadamu ya thamani ya Euro Milioni 50 kwa ajili ya Iraq. Ndege za jeshi la anga la Ujerumani tayari zimeshapeleka nchini Iraq shehena ya tani180 za chakula,mablanketi na dawa.
Ujerumani pia itapeleka vizibao alfu nne vya kumwezesha mtu kujihami. Wakurdi pia watapewa msaada wa kofia za chuma, vifaa vya mawasiliano na miwani ya kuonea usiku. Askari sita wa Ujerumani tayari wapo ugani kuongoza shughuli za kuigawa misaada hiyo ya kibinadamu pamoja na zana za kijeshi.
Tamko la serikali
Baadaye leo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel atatoa tamko la serikali bungeni juu ya uamuzi wa kuwasaidia Wakurdi kijeshi. Bunge pia litaujadili uamuzi huo lakini hakuna kitakachobadilika. Serikali haitakuwa na wajibu wa kuutekeleza uamuzi wa Bunge.
Tofauti na majukumu mengine ya jeshi la Ujerumani katika nchi za nje, Bunge halina sauti katika kuamua juu ya kupeleka silaha kwenye sehemu za migogoro. Idadi kubwa ya wabunge wa vyama vilivyomo katika serikali ya mseto wanauunga mkono uamuzi huo. Ni chama cha mrengo wa shoto tu ambacho kimsingi kinapinga Ujerumani kupeleka silaha katika maeneo ya migogoro.
Pia idadi kubwa ya wananchi wanaupinga uamuzi wa kupeleka silaha nchini Iraq. Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni theluthi mbili ya wananchi wa Ujerumani hawakubaliani na uamuzi huo.
Mwandishi: Pöhle,Sven
Tafsiri:Mtullya Abdu
Mhariri: Josephat Charo