1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIraq

Ujerumani kushirikiana zaidi na Iraq dhidi ya IS

8 Machi 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Uerumani Annalena Baerbock asema wanajeshi wa Ujerumani wako Iraq kwaajili ya kutoa ushauri na mafunzo kwa vikosi vya nchi hiyo kama sehemu ya juhudi za Kimataifa.

Außenministerin Baberbock im Irak
Picha: Hadi Mizban/AP/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock yuko nchini Iraq na  ameahidi Ujerumani itaendelea kuiunga mkono nchi hiyo na kuisadia  katika mapambano yake dhidi ya kundi la kigaidi linalojiita dola la Kiislamu. 

Annalena Baerbock yuko Iraq katika ziara ya siku nne  na jana jumanne alifanya mazungumzo  na waziri mkuu wa nchi hiyo Mohammed Shia al Sudani mjini Baghadad  kabla ya jioni kuelekea Erbil, mji mkuu wa jimbo la Kurdistan lenye utawala wake wa ndani Kaskazini mwa Iraq.

Picha: Hadi Mizban/AP/picture alliance

Leo Jumatano atakutana na viongozi wa jimbo hilo. Akiwa mjini Baghdad  alifanya mkutano na waandishi wa habari pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Iraq Fuad Hussein na katika mkutano huo aliweka wazi kwamba Ujerumani itaendelea kushirikiana na Iraq  kutoa shinikizo dhidi ya kundi la kigaidi linalojiita dola la Kiislamu linalofanya ukatili na linaloendelea kuwa kitisho.

"Kile kilichofanywa na kundi la IS dhidi ya jamii ya Wayazidi,jaribio la kutaka kuiangamiza kabisa jamii hiyo,utekaji nyara,kuendeleza utumwa,yote hayo yanamaanisha neno moja ambalo hatulitazami kwa mzaha, tunaliita, mauaji ya halaiki.''

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema Iraq imepiga hatua kubwa ya mafanikio katika mapambano dhidi ya kundi hilo la IS lakini amesisitiza kwamba kundi hilo bado limebakia kuwa kitisho katika taifa hilo.

Amebaini kwamba wanajeshi wa Ujerumani wako Iraq kwaajili ya kutoa ushauri na mafunzo kwa vikosi vya nchi hiyo kama sehemu ya juhudi za Kimataifa.Anapanga pia kukutana na wanajeshi wa Ujerumani walioko Iraq kupata taswira ya shughuli zao katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.

Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Iran yakosolewa

Kwa upande mwingine  Baerbock pia aliikosoa vikali Iran na kuitaka nchi hiyo kusitisha mashambulizi yake ya makombora dhidi ya Iraq akitilia mkazo kile kilichozungumzwa na waziri mwenzake Fuad Hussein kwamba Iran inapaswa kuheshimu uhuru wa mamlaka ya Iraq.

"Na utawala wa Iran unaonyesha kwa mashambulio yao ya makombora kwamba siyo tu unakandamiza kikatili na bila huruma wananchi wake, ni wazi pia kwamba unahatarisha maisha na uthabiti katika kanda nzima, ili kuendeleza madaraka yake. Hili halikubaliki hata kidogo na ni jambo hatari kwa kanda nzima.''

Picha: KURDPA

Pamoja na suala la mashambulizi ya Iran  na kitisho cha IS Iraq, waziri wa mambo wa Ujerumani katika ziara yake hii pia anasukuma ajenda ya mapambano ya pamoja dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi lakini pia amekumbusha kuhusu umuhimu wa wanawake katika maendeleo ya jamii za ulimwengu akisema, jamii zinauthabiti zaidi na amani  ikiwa wanawake wanaweza kusaidia kutowa mwelekeo,kwasababu hicho ndicho hasa kinachowaunganisha watu wote ulimwenguni.