Ujerumani kusitisha kuidhinisha mauzo ya silaha kwa Uturuki
13 Oktoba 2019"Kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Uturuki kaskazini mashariki mwa Syria , serikali ya shirikisho haitatoa tena vibali vipya kwa ajili ya vifaa vya kijeshi ambavyo vinaweza kutumika na Uturuki nchini Syria," Maas amesema.
Maas aliongeza kwamba serikali ya Ujerumani tayari imeweka vizuwizi katika mauzo ya nje ya silaha zake kwa Uturuki katika mwaka 2016 kutokana na mashambulizi ya nchi hiyo katika jimbo la Afrin.
Washirika wa mataifa ya magharibi wamekosoa operesheni ya Uturuki ndani ya Syria, ambayo ilianza siku ya Jumatano , ikisema inatishia mzozo mkubwa wa kibinadamu pamoja na kufufua kundi la itikadi kali la Kiislamu linalojiita Dola la Kiislamu katika eneo hilo.
Siku ya Jumamosi , wizara ya mambo ya nje na ulinzi mjini Paris zilisema kuwa Ufaransa inasitisha mauzo yake ya silaha kwa Uturuki kutokana na mashambulizi ya Uturuki kaskazini mwa Syria.
Serikali mjini Paris imeamua kusitisha mipango yote ya mauzo ya silaha kwa Uturuki ambayo inaweza kutumiwa katika mashambulizi, wizara hizo zilisema katika taarifa ya pamoja.
Siku ya Ijumaa , Uholanzi ilisema imesitisha kwa muda mauzo yake ya silaha kwa Uturuki, na Sweden ikasema itatafuta kuungwa mkono kwa ajili ya kuwekewa vikwazo vya Silaha Uturuki na mataifa yote ya Umoja wa Ulaya katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa Umoja huo wiki ijayo.
Mauzo ya silaha kwa Uturuki
Wanasiasa mashuhuri wa mrengo wa kushoto nchini Ujerumani wamekuwa wakitoa mwisho wa kupigwa marufuku kabisa mauzo ya silaha nchini Uturuki.
Siku ya Jumamosi , maelfu ya watu walishiriki maandamano katika miji nchini Ujerumani kupinga mashambulizi ya kijeshi ya Uturuki. Mjini Kolon , zaidi ya watu 10,000, wengi wao wakiwa Wakurdi , wanakadiriwa kujiunga na maandamano hayo.
Kiasi ya waandamanaji 4,000 waliingia mitaani mjini Frankfurt, wakati waandamanaji 3,000 katika kila mmoja ya miji ya Hamburg na Hannover walishiriki maandamano.
Maandamano zaidi yaliripotiwa mjini Bremen, Berlin na Saarbrueken.
Maandamano pia yaliripotiwa katika miji ya Ufaransa. Maandamano makubwa kabisa yalikuwa katika mji mkuu Paris, ambako watayarishaji wameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa watu 20,000 walijitokeza.
Baada ya tangazo la Maas , Katrin Goering-Erkardt wa chama cha walinzi wa mazingira The Green, alisema ; "Marufuku ya serikali ya Ujerumani ya mauzo ya silaha ni hatua ya kwanza iliyochelewa mno. Hata hivyo, haipaswi tu kutekelezwa kwa ajili ya mauzo ya baadaye lakini pia kwa mauazo ambayo tayari yamekwisha idhinishwa."
Ujerumani imejizuwia kusitisha kabisa mauazo ya silaha kwa Uturuki katika mashambulizi ya hapo zamani ya Uturuki nchini Syria.