1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kutafakari udhibiti wa silaha

24 Julai 2016

Serikali ya Ujerumani yatakiwa kuchukuliwa hatua zaidi kudhibiti mauzo ya bunduki kufuatia mauaji ya watu tisa Munich aliofanywa na kijana aliechanganyikiwa akili ambaye alikuwa na shauku ya kufanya mauaji makubwa.

Picha: Gemeinfrei

Naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel na kiongozi wa chama cha Social Demokrat (SPD) cha sera za wastani za mrengo wa kushoto ameiambia kampuni ya habari ya Funke yenye kumiliki magazeti kadhaa ya Ujerumani kwamba "lazima tuendelee kufanya kila linalowezekana kupunguza na kuweka udhibiti mkali wa silaha zenye kusababisha vifo".

Gabriel amesema maafisa wa serikali ya Ujerumani wanachunguza vipi kijana huyo wa Kijerumani mwenye asili ya Iran ameweza kuwa na silaha licha ya kwamba ilikuwa ikijulikana kwamba alikuwa na matatizo makubwa ya akili.

Gabriel amesema "udhibiti wa bunduki ni suala muhimu."

Kijana wa Kijerumani mwenye asili ya Iran na mwenye umri wa miaka 18 hapo Ijumaa aliwafyatulia watu risasi katika kituo mashuhuri cha maduka mjini Munich na kuwauwa tisa,kujeruhi wengine 27 kabla ya kujiuwa mwenyewe kwa kujitwanga risasi wakati polisi walipokuwa wakimnyemelea.

Naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel .Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Mashambulizi ya risasi ya Munich ni kisa cha tatu cha matumizi ya nguvu dhidi ya raia kutokea Ulaya Magharibi na cha pili kutokea kusini mwa Ujerumani katika kipindi cha siku nane.

Sheria kuangaliwa upya

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere ambaye ni mwanachama wa chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel cha Christian Demokrat (CDU) naye ameliambia gazeti la Bild am Sonntag katika mahojiano tafauti kwamba anapanga kuziangalia upya sheria za kumiliki bunduki nchini Ujerumani na kuziboresha inapobidi.

De Maiziere amesema sheria za kumiliki bunduki za Ujerumani tayari ni kali sana na kwamba ni muhimu kujuwa vipi muuaji huyo aliweza kuipata bastola ambayo aliitumia kufanyia mauaji.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere wa kwanza (kushoto) akitembelea kituo cha maduka cha Olympia mjinI Munich kilichoshambuliwa.Picha: Getty Images/J. Simon

Katika mahojiano yaliyochapishwa Jumapili (24.07.2016) amesema inabidi tathmni ifanyike kwa uangalifu kuona iwapo kuna haja ya kufanyika kwa marekebisho zaidi ya sheria hiyo.Amesema Ulaya pia imekuwa ikijadili miongozo mipya ya silaha.

Vyama vyote viwili kile cha Kansela Merkel (CDU) na kile cha SPD vinakubali kwamba sheria kali zaidi zinahitajika kuzuwiya watu kuigiza mashambulizi hayo.

Wajerumani na bunduki

Juu ya kwamba kwa kawaida bunduki haziwekwi hadharani nchini haimaanishi kwamba Wajerumani wanaziepuka. Kwa kweli nchi hiyo inashika nafasi ya nne kwa wingi wa umiliki wa silaha wa kila mtu duniani.Lakini umiliki wa silaha nchini unachukuliwa kama ni upendeleo sio haki na leseni ya silaha za moto hutolewa tu baada ya mtu kukidhi vigezo kadhaa vikali.

Aina mbali mbali za bastola.Picha: DW/F. Khan

Vigezo vinavyotakiwa kutimizwa ni pamoja na kuwa na maarifa ya utaaalamu wa kitumia silaha husika maarifa ambayo kwa kawaida hupatikana baada ya kuhudhuria mafunzo kwa miezi kadhaa na kwamba haja ya kuimilki sio lazima iwe kwa ajili ya kujihami na kuonekana kama ni sababu ya kutosha.

Kuna vibali vya aina tatu vya kumiliki silaha nchini Ujerumani.

1)Kwa ajili ya mashindano ya kulenga shabaha

2)Kuwinda

3)Kwa wataalamu na wale wenye kuchanga silaha kwa ajili ya kumbukumbu ambapo manunuzi yake lazima yawasilishwe na mtu binafsi ili kuidhinishwa.

Muuaji aliuwa na matatizo ya akili

Wachunguzi wamebainisha kwamba kijana aliyehusika na mauaji ya Munich alikuwa akijulikana kwamba alikuwa akisumbuliwa na msongo wa mawazo na yeye mwenyewe amekiri kupitia video katika mtandao wa YouTube kwamba alikuwa akipatiwa matibabu ya akili kuhusiana na kutokuwa na subira na rahisi kukasirika.

Afisa wa polisi akiwa kazini siku ya raia waliposhambuluwa kwa risasi Munich.Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Widmann

Hii inamaanisha kwamba asingeliweza kufaulu mtihani wa saikolojia na "utoshelevu wa kibinafsi" kigezo kinachotakiwa kitimizwa kwa ajili ya kupatiwa leseni ya kumiliki bunduki.

Polisi imethibitisha kwamba muaji huyo alikuwa hana kibali hicho na kwamba silaha aliyokuwa nayo ilipatikana kwa njia sisizo halali juu ya kwamba kwa njia gani ni kitendawili. Hii pia inamaanisha kwamba hatua yoyote ile ya kisheria kuzuwiya umiliki wa silaha itabidi ulishughulikie soko la silaha za magendo ambapo kwa serikali ya Ujerumani yumkini hatua hiyo isitosheleze.

Baadhi ya wachambuzi wamedokeza kwamba kuruhusiwa kwa usafiri huru wa watu katika kanda ya Schengen kumewezesha bunduki zinazonunuliwa kwa bei rahisi Ulaya mashariki , ndani au nje ya Umoja wa Ulaya kuenezwa barani kote Ulaya.

Hii inamaanisha kwamba tatizo hilo yumkini likashughulikiwa vizuri zaidi katika ngazi ya Ulaya.

Mwandishi . Mohamed Dahman : DW/Reuters/

Mhariri : Sylvia Mwehozi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW