Ujerumani kutoa msaada zaidi kwa Afrika?
14 Novemba 2016Kwa mujibu wa mashirika hayo iwapo Ujerumani haitachukulia kwa makini ripoti hiyo upo uwezekano wa kuongezeka idadi ya wahamiaji kutoka Afrika wanaohatarisha maisha yao ili mradi tu wafike Bara Ulaya. Mapendekezo hayo ni pamoja na Ujerumani kuanzisha hazina ya siku za baadae ambayo mwanzoni itakuwa na Euro billion 120 kutoka kwa wawekezaji binafsi.
Fedha hizo zitatumika katika sekta ya nishati mbadala, maendeleo ya viwanda na kuboresha miundo mbinu. Kwa sasa Ujerumani inatumia Euro mbili kwa kila mtu Afrika katika maswala ya maendeleo, kiasi hicho cha hela ni kidogo sana. Wataalamu hao pia wameonya kuwa idadi ya wahamiaji kutoka Afrika itaongezeka kwa kasi katika siku zijazo iwapo hakuna hatua zitakazokuwa zimepigwa katika kuunda nafasi za ajira kwa vijana wa bara hilo.
Waziri huyo wa maendeleo wa hapa Ujerumani Gerd Müller anaunga mkono wazo hilo na kusema katika kipindi cha wiki kadhaa kijacho atawasilisha wao lake kama hilo. "Ni lazima tuwekeze katika nchi hizo, tunahitaji kuwapa watu matumaini. Vinginevyo hatutashuhudia mamia kwa maelfu ya wakimbizi bali mamilioni katika miungo kadhaa ijayo. Kwa hivyo vijana Bara Afrika hatakuwa bila ajira na kutofahamu hali yao ya baadae katika nchi zao,” amesema Müller.
Wakimbizi watakiwa kusaidiwa zaidi
Uchunguzi wa mashirika hayo pia ulibaini kuwa Afrika ina uwezo mkubwa katika maeneo kama vile kilimo na nishati mbadala. Kufuatia hilo wanapendekeza ujenzi wa vituo vya uzalishaji nishati inayotokana na jua katika baadhi ya maeneo ya Bara la Afrika, ambavyo havitatoa tu nafasi za ajira lakini pia kutatoa tatizo sugu la ukosefu wa nguvu za umeme katika bara hilo swala alilokubaliana nalo Waziri Müller. "Ni kuhusu kuimarisha na kuendeleza uwezo wa watu wao wenyewe. Sio eti twende kule na mipango yetu na fedha zetu na pia tushiriki katika usimamizi. Sisi hatutaki ukoloni mambo leo. Hivyo ndivyo inavyofanya China. Huo sio mtizamo wetu."
Ripoti hiyo pia inatoa wito wa kupanuliwa programu ya misaada ya kiutu kwa wakimbizi na pia wakimbizi wa ndani kwa ndani. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakati wa ziara yake nchini Niger hata hivyo aliondoa uwezekano wowote wa Ujerumani kutenga mfuko wa fedha kwa maendeleo Barani Afrika. Kansela Merkel alisema hali ilivyo hivi sasa Afrika ni tofauti na ilivyokuwa bara ulaya wakati wa vita vya pili vya dunia. Mpango huo uliopendekezwa na mashirika hayo ni sawia na ule uliotolewa na Marekani kwa Bara Ulaya ili kujijenga upya kufuatia vita vya pili vya dunia.
Mwandishi: Jane Nyingi/Africa Link
Mhariri: Yusuf Saumu