Ujerumani kuumana na Norway; wahuni nje
4 Septemba 2017Rais wa shirikisho la kandanda nchini Ujerumani Reinhard Grindel anataka vyama vya kandanda barani Ulaya kufanyakazi kwa karibu kupambana na tabia mbaya ya wahuni katika michezo baada ya mashabiki kuimba kauli mbiu za Wanazi katika mchezo wa kufuzu katika fainali za kombe la dunia mjini Prague ambapo Ujerumani ilikuwa inacheza dhidi ya Jamhuri ya Cheki.
Grindel ameliambia jarida la Kicker , kwamba " tunahitaji kujadili suala la mauzo ya tikiti kwa pamoja na vyama vya kandanda barani Ulaya na kupata njia ya kuhakikisha udhibiti zaidi kote barani Ulaya.
Grindel alikosoa vikali kundi la mashabiki wapatao 200 wa Ujerumani ambao waliimba kauli mbiu za Wanazi wakati wa mchezo huo siku ya Ijumaa ambapo Ujerumani iliishinda kwa taabu Jamhuri ya Cheki kwa mabao 2-1. Pia walimtusi mshambuliaji wa Ujerumani Timo Werner.
Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew ameomba mashabiki katika mchezo wa leo kati ya Ujerumani na Norway kuheshimu wachezaji ambao wamehama kutoka timu zao kwenda kwingine kwasababu huo ni uamuzi wa mtu binafsi.
Alikuwa akilenga kuwatahadharisha mashabiki wa Stuttgart ambao huenda wakamuona mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Timo Werner kuwa ni msaliti baada ya mshambuliaji huyo kuimaha timu hiyo iliposhuka daraja na kujiunga na RB Leipzig ambapo hivi sasa anang'aa na timu hiyo na kuitwa katika ya taifa.
Kundi C
Mchezo mwingine wa kundi C ni kati ya Azerbaijan dhidi ya San Marino, na Ireland ya kaskazini inapambana na Jamhuri ya Cheki.
Ubelgiji imekuwa timu ya kwanza katika bara la Ulaya kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwakani nchini Urusi. Ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Ugiriki jana Jumapili ulitosha kuipeleka timu hiyo katika nafasi ya juu katika kundi H na kuingia katika fainali yake ya pili mfululizo baada ya kumaliza katika robo fainali katika mashindano ya mwaka 2015 nchini Brazil. Matokeo ya jana yamerefusha pia rekodi yake ya timu hiyo kutoshinda katika michezo 11.
Italia iliyopata jeraha kwa kipigo dhidi ya Uhispania siku ya Jumamosi inataka leo kubadi mkondo wakati itakapokuwa mwenyeji wa Israel kesho Jumaane katika mchezo wa kundi G. Squadra Azzuri inahitaji ushindi ili kujiimarisha katika nafasi ya pili katika kundi G nyuma ya Uhispania ili kuwa salama dhidi ya timu inayoshikilia nafasi ya tatu Albania wakati wakijiweka vizuri kufikia fainali nchini Urusi mwakani.
Uhispania yafanya kweli
Nayo Uhispania iliyoifanyia kitu mbaya Italia kwa kuicharaza mabao 3-0 siku ya Jumamosi inataka kuimarisha nafasi yake kuwa moja kati ya timu zinazopigiwa upatu kunyakua kombe la dunia mwakani kwa kutayarisha kipigo kingine dhidi ya Liechtestein kesho Jumaane.
Nayo Uholanzi imeweka matumaini yake hai ya kufikia fainali za mwakani za kombe la dunia baada ya kuirarua Bulgaria jana kwa mabao 3-1 , lakini Sweden iliikaanga Belarus kwa mabao 4-0 na kuifikia Ufaransa katika msimamo wa kundi A jana Jumapili kwa kufikisha pointi 16 .
Kwa nchi tano ambazo bado zinapambana kuwania nafasi mbili za moja kwa moja kuingia katika fainali za mwakani nchini Urusi , kampeni ya kufuzu kuingia katika fainali hizo kwa mataifa ya Asia imefikia sasa uamuzi wa dakika 90. Iran na Japan tayari zimefuzu kuingia katika fainali kama washindi wa makundi A na B, lakini timu hizo mbili bado zinajukumu la kuamua ni mahasimu wao gani , ikiwa ni mabingwa wa kombe la mataifa ya Asia , Australia na Korea kusini , zitajiunga nazo katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwakani.
Timu saba za Asia zinaweza kufuzu ama kwa kumaliza zikiwa nafasi ya pili katika makundi yao ama kwa kupitia mchujo katika bara hilo ama kutoka bara moja kwenda jingine.
Iran inakuwa mwenyeji kwa Syria inayowashangaza wengi , timu ambayo haikuweza kucheza nyumbani kutoka na hali ya kivita nchini humo, lakini imejisogeza hadi nafasi ya tatu katika kundi A wiki iliyopita kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Qatar. Licha ya kushindwa kujitayarisha kwa njia ya utulivu , Syria bado ina nafasi ya kufuzu kucheza katika fainali yake ya kwanza ya kombe la dunia iwapo matokeo yatakuwa mazuri kesho Jumanne.
Syria lakini inalazimika kushinda mjini Tehran na kutegemea Korea kusini ipoteze mchezo wake kwa ushindi mdogo dhidi ya Uzbekistan.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman