1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuvaana na Engalnd fainali ya Euro

Sylvia Mwehozi
28 Julai 2022

Ujerumani imeichapa Ufaransa mabao 2-1 katika mchezo wa pili wa nusu fainali na kujikatia tiketi ya fainali ya michuano ya kombe la Ulaya upande wa wanawake itayapigwa Jumapili katika uwanja wa Wembley.

Women's Euro 2022 - Deutschland v Frankreich | Tor (2:1)
Picha: Beautiful Sports/IMAGO

Nahodha wa timu ya Ujerumani na mshambuliaji machachari Alexandra Popp ndiye amepeleka kilio kwa timu ya Ufaransa kwa kufunga bao mbili katika kipindi cha kwanza na cha pili.

Popp aliitanguliza mbele Ujerumani kwa kufunga bao la kwanza mnamo dakika ya 40, lakini Ufaransa walisawazisha dakika nne baadae kwa bao zuri la Kadidiatou Diani. Bao la pili liliwekwa wavuni mano dakika ya 76 na kumfanya Popp kufikisha goli sita katika mechi tano.

Ujerumani, ambao ni mabingwa mara nane wa michuano hiyo ya Ulaya upande wa wanawake sasa itavaana na wenyeji England ambao walitinga fainali baada ya kuitandika Sweden bao 4-0 katika mchezo wa Jumanne. Fainali za michuano hiyo itashuhudiwa na mashabiki wapatao elfu 87,000 katika uwanja wa Wembley.

Kadidiatou Diani wa Ufaransa akishangilia mara baada ya kusawazishaPicha: Richard Callis/SPP/Panoramic/IMAGO

Ufaransa walikuwa na nafasi kubwa baada ya kipindi cha mapumziko na kutoa ushindani mkali kwa safu ya mashambulizi ya Ujerumani, lakini hata hivyo jitihada zao hazikuweza kuzaa bao. Kocha wa Ufaransa Corinne Diacre alisema kuwa "kwa bahati mbaya hatukufanya vyema usiku wa leo. Hatukuweza kuboresha nafasi za mabao tulizopata."

Naye kocha wa timu ya Ujerumani Martina Voss-Tecklenburg amesema mchezo wa fainali dhidi ya England utakuwa wa kiwango cha juu. "Tunajua watakuwa mbele ya mashabiki wengi wa nyumbani lakini tuko tayari kuwakabili"

Kutinga fainali kwa Ujerumani ni mafanikio makubwa kwa nahodha wa timu hiyo Alexandra Popp ambaye anaichezea klabu ya Wolfsburg baada ya kukosa michuano miwili iliyopita kutokana na majeraha. Mwaka 2013 Popp aliweka rehani nafasi yake ya kushinda taji akiwa na timu ya taifa wakati alipocheza kutokana na jeraha la kifundo cha mguu na kuisaidia Wolfsburg kushinda mataji matatu msimu wa 2012-13.

Siku ya Jumapili, mshambuliaji huyo hatakuwa tu akipigania taji hilo bali pia kiatu cha dhahabu akiwa amejiunga na Beth Mead wa England wakiwa kileleni mwa orodha ya wafungaji wenye mabao mengi katika michuano hiyo. Wachezaji hao wawili wamevunja rekodi ya mchezaji wa Ujerumani Inka Grings kwa kufikisha mabao sita katika michuano ya kombe la Ulaya kwa wanawake mwaka 2009. Tofauti na Ujerumani ambao wamebeba kombe hilo mara nane, timu ya wanawake ya Ufaransaimeingia hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW