1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuwa mwenyeji wa Euro 2024

27 Septemba 2018

Ujerumani ndio itakayokuwa mwenyeji wa mashindano ya Euro 2024 baada ya kuipiku Uturuki katika kinyang'anyiro cha farasi wawili cha kutafuta kibali. Uamuzi huo wa UEFA umeisikitisha Uturuki

Fußball Bekanntgabe EM-Gastgeber 2024
Picha: picture-alliance/dpa/S. Stache

Otone

Ni Rais wa Shirikisho la Kandanda la Ulaya – UEFA Aleksander Ceferin akitangaza matokeo ya uamuzi huo. Ujerumani ilipigiwa kura hiyo na wanachama 17 wa kamati kuu ya UEFA. Uamuzi huo wa UEFA ni wa kusikitisha sana kwa upande wa Uturuki ambayo pia ilishindwa katika ombi lake la kuandaa michuano hiyo katika mwaka wa 2008, 2012 na 2016.

Ceferin alisema uamuzi huo ulikuwa wa wazi na kura ikapigwa kwa njia ya kidemokrasia. Na kila uamuzi wa kidemokrasia ni uamuzi sahili. Nahodha wa zamani wa Ujerumani Philipp Lahm, alizungumzia uamuzi huo.

Waziri wa Vijana na Michezo wa Uturuki Mehmet Kasapoglu amesema kuwa uamuzi wa kuipa Ujerumani haki za kuandaa Euro 2024 ni wa kuhuzunisha kwa UEFA.

Amesema ni wazi kwamba Uturuki ilikuwa imejiandaa vyema kabisa kwa ajili ya dimba hilo kwa sababu ina vifaa na viwanja vipya.

Ujerumani iliandaa Kombe la Dunia 2006, lakini haijawahi kuandaa Euro kama nchi iliyoungana. Maana Iliyokuwa Ujerumani Magharibi iliandaa tamasha hilo mwaka wa 1988.

Kinyang'anyiro kilikuwa kati ya Ujerumani na UturukiPicha: picture-alliance/SvenSimon/F. Hoermann

Michuano hiyo itaandaliwa katika viwanja 10 vya Ujerumani, vyenye uwezo wa kuwa na mashabiki milioni 2.78 – ikiwa ni 290,000 zaidi ya idadi ya mashabiki wa Uturuki – na hivyo kuipa Ujerumani faida ya kifedha  kutokana na mapato ya tiketi za mechi. Rais wa UEFA Aleksander Ceferin ameweka wazi kuwa ni muhimu "kutengeneza faida kubwa kabisa ya kifedha” kutokana na michuano ya Euro 2024.

UEFA huitegemea michuano huyo kusaidia kuvifadhili vyama vya kandanda 55 ambavyo ni wanachama wake. Mapato ya dimba la Euro 2016 nchini Ufaransa lililozishirikisha timu 24 yalikuwa karibu euro bilioni mbili. UEFA ilipata faida ya karibu euro bilioni 850.

Serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan imeonekana kuwa ya kimabavu na ripoti ya UEFA iliyochaposhwa wiki iliyopita ilisema kuwa Uturuki haina mpango maalum wa kushughulikia suala la haki za binaadamu wakati wa mashindano hayo.

Ujerumani italenga kuyatumia mashindano hayo katika kurejesha hisia nzuri na msisimko ulioshuhudiwa katika Kombe la Dunia 2006.

Uamuzi wa leo pia unasaidia kulifufua shirika la kandanda la Ujerumani – DFB na kiongozi wake baada ya miezi minne ya misukosuko.

DFB na mashabiki walikuwa na mahusiano mabaya na wachezaji wa timu ya taifa Mesut Oezil na Ilkay Gundogan, ambao wana asili ya Kituruki, kabla na baada ya  Kombe la Dunia nchini Urusi. Suala hilo lilizuka baada ya wachezaji hao kupiga picha na rais wa Uturuki Erdogan mjini London mwezi Mei. Oezil kisha akatumiwa kama kisingizio cha timu hiyo kuondolewa mapema katika Kombe la Dunia. Alitangaza kutoichezea tena Ujerumani.

Awali, Kamati kuu ya UEFA iliidhisha matumizi ya waamuzi wasaidizi wa kutumia video – VAR katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanzia msimu ujao na Michuano ya Euro 2020, kufuatia hatua kama hizo katika mashindano ya FIFA na ligi nyingine kuu

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef