1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuwabana waomba hifadhi

12 Oktoba 2016

Waziri wa masuala ya ndani ya nchi wa Ujerumani, Thomas de Maiziere ameandaa rasimu ya sheria itakayorahisisha mchakato wa kuwarejesha makwao waomba hifadhi ambao maombi yao yamekataliwa.

Deutschland Flüchtlinge kommen an der ZAA in Berlin an
Picha: Getty Images/S. Gallup

Waziri huyo wa mambo ya ndani na wahafidhina wengine ndani ya serikali walianza kutafuta namna ya kuongeza kasi ya mchakato huo wa urejeshwaji tangu majira ya joto yanayomalizika.  

Waziri wa mambo ya ndani Thomas de Maiziere ameandaa rasimu ya kisheria inayolenga kuongeza kasi ya kuwarejesha makwao waombaji wa makazi ya kibanaadamu waliokataliwa, limeandika gazeti la Ujerumani la Die Welt, Jumatano hii.

"Kama urejeshwaji huo hauwezi kuwa wa haraka, labda kwa mfano kutokana na taarifa za uongo zinazohusiana na utambulisho ama utaifa wa mwombaji, ama kutokuwepo kwa ushirikiano wa kutosha wa kupatikana kwa pasi mbadala ya kusafiria , basi mwombaji huyo hataendelea kupata ruhusa ya kuendelea kuishi, ripoti kuhusu rasimu hiyo inasema.   

Zaidi ya watu 210,000 wametakiwa kuondoka Ujerumani, kufikia mwezi Agosti, ingawa 158,190 miongoni mwao wana msamaha wa kuendelea kuishi nchini humo kwa kipindi fulani , gazeti hilo la Die Welt limesema, kwa kuizingatia rasimu hiyo.

De Maiziere na washirika wake wa mrengo wa kulia wanataka kupunguza sababu zinazowabeba waomba hifadhi hao wakizingatia misamaha iliyopo, gazeti hilo limeongeza. Hata hivyo amesema idadi ya wanaoomba hifadhi kwa sasa imepungua

Waziri wa mambo ya ndani, Thomas de Maizere(Kulia) na kiongozi wa shirika la wakimbizi na wahamiaji nchini Ujerumani, Frank-Jürgen Weise walipozungumza na waandishi wa habari kuhusu rasimu hiyo.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Aidha, rasimu hiyo itazitaka mamlaka kuwatambua watu katika kipindi cha ndani ya siku 30 kabla ya siku ya kuwarejesha nyumbani, ili kupunguza uwezekano wa kutumia nguvu kuwaondoa kwa kutumia mahakama ama kwa kuzificha mamlaka. Rasimu hiyo ya sheria kwa upande mwingine itaongeza muda wa maafisa kuwatia kifungoni wale wanaokataa kuondoka, kuanzia siku nne hadi wiki mbili.

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria, Joachim Herrmann na maafisa wengine wanaotoka chama cha Christian Social Union, chama ndugu na chama cha De Maiziere na Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union, kwa pamoja wametaka kurejewa upya kwa uchunguzi wa watu waliopatiwa vibali vya hifadhi, baada ya kuingia kwa wingi mwaka jana, kwa karibu watu milioni moja. 

Katika hatua nyingine, rasimu hiyo mpya inaelezwa kuwa inaweza kuwa kibano kwa wahamiaji waliokataa kuomba hifadhi nchini Ujerumani kupata msamaha wa kuendelea kuishi nchini Ujerumani, kutokana na sheria mpya zinazolenga kuwarejesha makwao wahamiaji wanaovunja sheria za nchi na watakaobainika kuwa kitisho kwa usalama wa nchi.

Picha: picture-alliance/maxpp/A. Marchi

Wakati tayari rasimu hiyo ikiwa imesambaa kwa wizara mbalimbali nchini Ujerumani, baadhi ya maafisa wa juu wanataka kuanza kurejeshwa kwa haraka kwa waomba hifadhi ambao maombi yao yamekataliwa kufuatia matukio ya mashambulizi nchini Ujerumani, yaliyotukia mnamo mwezi Julai, ambao mawili kati yake yalitekelelezwa na mkimbizi kutoka Syria, anayehusishhwa na kundi la kigaidi la Dola la kiislamu, IS.

Jumatatu hii, polisi walimkamata kijana wa miaka 22, raia wa Syria aliyepata kibali cha muda cha hifadhi mwezi Juni mwaka 2015, na ambaye anasemekana alikuwa tayari kutekeleza mashambulizi yalishabihiana na lililofanyika Brussels, Ubelgiji na Paris, Ufaransa. Vyanzo vya kiusalama vimesema jumanne hii kwamba kijana huyo ana mahusiano na kundi hilo la IS.

Mwandishi: Lilian Mtono/http://www.dw.com/en/de-maiziere-seeks-to-further-limit-asylum-exceptions/a-36019931/Rtre.
Mhariri: Iddi Ssessanga. 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW