1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuwarejesha wanawake wa IS kutoka Syria

Sekione Kitojo
23 Novemba 2019

Mwanamke Mjerumani anayeshukiwa  kuwa  mwanachama  wa kundi  linalojiita  "Dola  la  Kiislamu" atarejeshwa  nchini  humo pamoja  na  watoto  wake  watatu, kwa  mujibu wa  vyombo  vya habari  vya  Ujerumani.

Syrien, verschleierte Frauen
Picha: Getty Images/D. Souleiman

 

Itakuwa  ni mara ya  kwanza  kwa  Ujerumani kuwarejesha watuhumiwa  wa  aina  hiyo.

Maafisa  nchini  Ujerumani  wameamuru mwanamke  Mjerumani, anayeaminika  kuwa  ni  mwanachama  wa  kundi  linalojiita  "Dola  la Kiislamu" IS , kurejeshwa  nchini  mwake  kutoka  katika  kambi nchini  Syria, kwa  mujibu wa  ripoti iliyotolewa  jana  Ijumaa.

Wanawake waliokuwa katika kundi linalojiita Dola la Kiislamu nchini SyriaPicha: Getty Images/AFP/D. Soleilman

Gazeti  la  Spiegel limemtambua mwanamke  huyo  kuwa  ni Laura H. mwenye  umri  wa  miaka  30 kutoka  katikati  mwa  Ujerumani, likisema  kuwa  aliondoka  nchini  na  kujiunga  na   wanamgambo wa  jihadi  mwaka  2016. Yeye  pamoja  na  watoto  wake  watatu wanaripotiwa   kuishi  hivi  sasa  katika  kambi  inayoendeshwa  na Wakurdi  ya  al-Hol kaskazini  mwa  Syria. Wanatarajiwa  kuwasili nchini  Ujerumani , 'katika  siku  za  karibuni' kwa  kusafiri  kupitia  mji wa  Wakurdi wa  Erbil  nchini  Iraq, kwa  mujibu  wa  gazeti  la Siegel.

Siku  ya  Ijumaa, maafisa  wa  Ujerumani  walithibitisha  kuwa watoto  watatu "Wajerumani wanaoshikiliwa  kaskazini  mwa  Syria, wataweza  kuondoka  kwenda  Iraq pamoja  na  mama  yao." Hata hivyo , hawakuthibitisha  jina la  mama  yao  ama  kutoa  taarifa zaidi.

Mwanamke akiondolewa kutoka katika kundi la IS pamoja na watoto wakePicha: Getty Images/AFP/D. Souleiman

Wanawake walioko  kizuwizini

Kwa  mujibu wa  ripoti  za  vyombo  vya  habari, maafisa  wa Ujerumani  wamekuwa  wakimchunguza mama  huyo  kwa  shaka  ya kuwa  mwanachama  wa  shirika  la  kigaidi  na  kuwatelekeza watoto.

Washukiwa  wanawake  wa  kundi  hilo  la  "Dola  la  Kiislamu", tayari wamekuwa  kizuwizini  na  kufikishwa  mahakamani  nchini Ujerumani, lakini  mashitaka yamekuwa  tu katika  hatua  ya washukiwa  ambao  wamesafiri kurejea  nyumbani  kwa matakwa yao  ama  wamerejeshwa  na  nchi  nyingine. Iwapo  suala  la  laura H. litathibitishwa , litakuwa  ni  mara  ya  kwanza  kwa  Mjerumani kurejeshwa  nchini.

Wanawake waliokuwa katika kundi la IS wakiachiliwa huruPicha: AFP/B. Kilic

Duru za  usalama  nchini  Ujerumani  zinaamini  kuwa  zaidi  ya wanachama  80  wa  IS  ambao  ni  Wajerumani  wanaendelea kushikiliwa  nchini  Syria. Serikali  mjini  Berlin ilitangaza  hivi karibuni  kuwa  itatoa  maamuzi  ya  kurejeshwa  kwa  wanawake waliolewa  na  wanamgambo  wa  Jihadi  kwa  misingi  ya kesi  kwa kesi.

Watoto  kadhaa  tayari  wamekwisha  rejeshwa  kutoka  katika kambi  katika  mashariki  ya  kati. Mapema  mwezi  huu, mahakama nchini  Ujerumani  iliamuru  kuwa  akina  mama mbali  mbali wanaohusishwa  na  IS pamoja  na  watoto  wanalazimika kurejeshwa  pamoja , kwasababu  watoto  hao  walikuwa wanategemea  "ulinzi  na  malezi ya  mama  zao."

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW