Ujerumani kuweka sheria kudhibiti uwekezaji wa kigeni
7 Agosti 2018Serikali kuu mjini Berlin inataka kupunguza masharti ya kuingilia kati kwenye uwekezaji wa siku za baadaye na kuchukuwa dhamana kutoka kampuni Za kigeni, kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa leo (7 Agosti).
Mabadiliko haya mapya yataiwezesha serikali kuweza kuhakiki kwa urahisi na hata ikibidi kupiga kura ya turufu dhidi ya kuzichukuwa dhamana za kampuni za Ujerumani ambazo zinaonekana ni muhimu kwa usalama wa nchi, liliripoti gazeti la Welt la Ujerumani.
Kwa mujibu wa matakwa ya serikali, wizara yake ya uchumi itakuwa na uwezo wa kuingilia kati pale ambapo mwekezaji kutoka nje ya Umoja wa Ulaya amepata hisa za moja kwa moja au hata zisizo za moja kwa moja kwenye kampuni ya Kijerumani ambazo zinafikia asilimia 15.
Katika hali ya sasa, serikali ya Ujerumani inaweza tu kuingilia kati ikiwa mwekezaji kama huyo amepata asilimia 25 ya hisa.
Sheria hii mpya inayokuja, itajikita zaidi kwenye kampuni zinazojihusisha na masuala ya ulinzi, miundombinu au teknolojia inayohusiana na mambo ya usalama.
Serikali yakanusha kuzuwia uwekezaji
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Peter Altmaier, aliliambia gazeti la Welt kwamba jukumu la serikali ni kulinda maslahi ya usalama ya nchi, hasa kwa sekta ambazo zinafahamika kuwa ni 'nyeti' sana kwa taifa.
Hata hivyo, Altmaier alikanusha kwamba serikali inataka kuzuwia uwekezaji wa kigeni na kushajiisha, badala yake, sera ya kulinda kampuni za ndani, isipokuwa inataka tu kujuwa zaidi wale wanaohusika na uchukuwaji wa kampuni hizo na kile kinachowasukuma kufanya hivyo.
"Hapana shaka, tunataka kampuni ziendelee kuwekeza nchini Ujerumani. Lakini pia tuna wajibu wa kulinda maslahi na utulivu wa nchi na usalama wa taifa", alisema kwenye mahojiano yake na gazeti la Welt.
Licha ya kukanusha huko, ni wazi kuwa sheria hii mpya itawalenga, kimsingi, wawekezaji wa Kichina ambao utundu wao wa kibiashara unawatia wasiwasi maafisa hapa Ujerumani kwamba huenda ukaiibia teknolojia ya viwanda na, hivyo, kutishia nafasi ya Ujerumani kwenye sekta ya uvumbuzi duniani.
Wiki iliyopita, serikali kuu mjini Berlin ilisema iko tayari kutumia kura yake ya turufu dhidi ya hatua ya kampuni ya Kichina ya Yantai Taihai kuichukuwa kampuni ya utengenezaji vifaa ya Leifeld.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DW English
Mhariri: Iddi Ssessanga