Ujerumani kuweka sheria ya kitaifa kudhibiti COVID-19
9 Aprili 2021Akizungumza na waandishi wa habari, msaidizi wa msemaji wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Ulrike Demmer amesema Ujerumani iko katikati ya wimbi la tatu la virusi vya corona na kwamba serikali ya kuu ya shirikisho pamoja na majimbo wamekubaliana kweka sheria ya kitaifa ya kudhibiti mambukizi ya virusi hivyo.
Lengo kuu la hatua hiyo ni kutaka kuwa na sheria zinazofanana na kwamba mabadiliko hayo yatawasilishwa kwenye baraza la mawaziri Jumanne ijayo. Idadi ya maambukizi nchini Ujerumani imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa licha ya kufungwa kwa shughuli za kiutamaduni, migahawa na maeneo ya starehe.
Akizungumzia umuhimu wa kuwa kuchukua hatua zaidi kukabiliana na maambukizi, waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn amesema, ili kupunguza idadi ya maambukizi, ikiwezekana, hatua za pamoja zinahitajika kuchukuliwa nchi nzima na kwamba mazungumzo ya serikali kuu na majimbo yatakuwa sahihi ili kupambana na janga hilo. Ametahadharisha kuwa, kama viongozi wengine hawatofikiri hivyo kuhusu hali halisi, basi mapambano yatakuwa magumu.
Taasisi ya Robert Koch yasisitiza tahadhari zaidi
Naye rais wa taasisi inayohusika na magonjwa ya kuambukizwa ya Robert Koch, Lothar Wieler ametahadharisha juu ya athari kubwa iwapo hatua zaidi za kukabiliana na mambukizi hazitochukuliwa nchini humo.
Amesema ikiwa hakutowekwa vizuizi vya shughuli, na mwenendo wa watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine hautadhibitiwa, maambukizi yataendelea kuongezeka na watu wengi watazidi kufa nchini humo.
Hadi sasa maamuzi ya kuweka masharti ya kupambana na COVID-19 yamekuwa yakifanywa kwa mashauriano na serikali kuu Berlin huku viongozi wengine wakiwa na mgawanyiko juu ya kuweka vizuizi na miji mingine imelegeza masharti ya kukabiliana na virusi hivyo. Hayo yanajiri wakati nchi hiyo ikiwa na ongezeko kubwa la virusi vya corona na hospitali zikizidi kuelemewa na wagonjwa.