1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kuzidisha idadi ya wanajeshi Mali Magazetini

Oumilkheir Hamidou
9 Machi 2018

Uamuzi wa serikali kuu ya Ujerumani kuzidisha wanajeshi nchini Mali, siku ya wanawake na kesi dhidi ya vijana 4 wa Eritrea waliombaka bibi mmoja huko Dessau, ni miongoni mwa mada magazetini wiki hii.

Deutschland | Soldaten der Deutsch-Franzöische Brigade beim Appell
Picha: picture-alliance/W. Rothermel

Tunaanzia Berlin ambako serikali ya mhula wa tatu iliyokamilisha jukumu lake, ilikutana kwa mara ya mwisho wiki hii na kupitisha maamuzi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuzidisha idadi na kuimarisha shughuli za wanajeshi wa Ujerumani-Bundeswehr, wanaosaidia kuleta amani nchini Mali. Magazeti takriban yote mashuhuri ya Ujerumani yamezungumzia mada hiyo inayohitaji kuidhinishwa na bunge la shirikisho Bundestag. Gazeti la Die Welt linazungumzia kuhusu "majukumu yasiyokuwa na mpango na jeshi lisilokuwa na vifaa vya kutosha. Linanukuu wawakilishi wa wanajeshi wanaoonya dhidi ya madhara ya utaratibu wa aina hiyo.

Die Welt linasema idadi ya wanajeshi wa Ujerumani wanaotumikia kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa mataifa MINUSMA nchini Mali itaongezeka kutoka wanajeshi 11000 na kuwa wanajeshi 1100. Na sambamba na hayo wanajeshi 400 wa Ujerumani watasaidia juhudi za kutoa mafunzo zinazoongozwa na Umoja wa Ulaya nchini humo EUTM. Kwanini Ujerumani inatuma wanajeshi katika maeneo ya mizozo, linajiuliza gazeti la die Welt. Jibu amelitoa waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen aliyetilia mkazo azma ya serikali kuu ya Ujerumani ya kusaidia kuleta utulivu katika nchi dhaifu. Kama jibu la suala hilo linatosha, ikizingatiwa ugumu wa mzozo wa Mali,bunge la shirikisho ndilo litakaloamua, linamaliza kuandika gazeti hilo la mjini Bonn.

Mali ni kituo muhimu cha muda kwa wanaokimbilia Ulaya

Gazeti la Der Tagesspiegel linahisi uamuzi wa serikali  kuu ya Ujerumani kuzidisha idadi na kuimarisha shughuli za wanajeshi wa Ujerumani nchini Mali umetokana na ile hali kwamba nchi hiyo ndiko wanakopitia wakimbizi wanaoelekea Ulaya. Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema idadi ya wanajeshi inaongezwa na majukumu kuimarishwa kwasababu wanajeshi wa Ujerumani ndio waliokabidhiwa uongozi wa kambi ya kijeshi ya  Gao ambao hadi wakati huu umekuwa mikononi mwa wanajehi wa Uholanzi.

 Elimu sawa kwa wanawake ni tija kwa nchi zinazoinukia

Siku ya wanawake, marchi nane imekuwa fursa kwa gazeti la Süddeutsche kumulika matatiizo wanayokabiliana nayo wanawake na wasichana barani Afrika, matatizo ambayo Süddeutsche linahisi wanaume wa bara hilo hawayatambui. Süddeutsche linayataja matatizo hayo kuwa ni pamoja na umaskini uliokithiri, vizingiti wanavyokabiliana navyo wasichana ambao hawakupata nafasi ya kwenda shule, kuambukizwa virusi vya HIV na kufariki dunia mapema, kuolewa wakiwa bado wadogo na kadhalika.

Gazeti la Süddeutsche linazungumzia faida zakuwekeza katika sekta ya elimu; Wasichana wakipata fursa ya kwenda shule, nafasi yao ya kuajiriwa inakuwa kubwa sawa na mapato yao kuongezeka. Pindi wasichana wakipatiwa nafasi sawa ya kwenda shule kama wenzao wa kiume, basi  hazina ya nchi zinazoinukia ingeongezeka kwa angalao dala bilioni 112, fedha ambazo Süddeutsche linasema zingeweza kuwekezwa katika shule, vyuo vikuu pamoja na kuongezwa idadi ya waalimu. Gazeti hilo la mjini Munich linamaliza kwa kusema wanawake waliosoma wanapitisha maamuzi muhimu na ya busara.

Waeritrea wanne watuhumiwa kumbaka mwanamke wa miaka 56

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii inahusu kesi iliyofunguliwa katika korti moja ya mjini Dessau katika jimbo la Sachsen Anhalt.Vijana wanne wa kutoka Eritrea wanatuhumiwa kuhusika na kumbaka bibi mmoja mwenye umri wa miaka 56, mwezi Agosti mwaka 2017. Ikidhihirika kama vijana hao wanne walimbaka  kweli kwa pamoja bibi huyo, basi kisa hicho kitakuwa kibaya kabisa kuwahi kushuhudiwa.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ BASIS/PRESSER/ALL

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman