1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Mazungumzo ya kuunda serikali yafikia pazuri

13 Oktoba 2021

Vyama vilivyojiimarisha zaidi kwenye uchaguzi wa mwezi uliopita huenda vikafikia makubaliano ya pamoja ifikapo mwishoni mwa wiki hii, ingawa bado kuna tofauti katika masuala ya kodi na mabadiliko ya tabianchi.

Deutschland Berlin | Ampel-Koalition | Symbolbild
Picha: Klaus-Dieter Esser/agrarmotive/picture alliance

Vyama hivyo hata hivyo vimesema bado vinashughulikia tofauti zilizopo baina yao, lakini vina imani ya kufikia makubaliano katika siku mbili zijazo. 

Katibu mkuu wa chama cha Waliberali mamboleo cha Free Democratic (FDP) Volker Wissing amesema wanatathmini matokeo ya mazungumzo yao ya siku kadhaa zilizopita na kukubaliana kile watakachoweza kukifanya kwa pamoja, lakini sasa vinaendelea kujadiliana kuhusu vizingiti vilivyopo baina yao.

Soma Zaidi: SPD,Kijani na FDP waanza mazungumzo rasmi

Katibu mkuu wa chama cha SPD Lars Klingbeil kwa upande wake amesema baada ya majadiliano hayo wana hakika watakubaliana iwapo watashughulikia vizingiti hivyo na kuongeza kuwa huenda ikawa katika kipindi cha siku mbili zijazo.

Alisema, "Haya yalikuwa mazungumzo ambayo masuala yote muhimu yalishughulikiwa, na ninasema haya huku nikijua kabisa kwamba bado tuna njia ndefu na kutakuwa na vizuizi. Lakini nina hakika baada ya siku hii moja na nusu na iwapo tutaona kama ni changamoto za kawaida, tutaweza kuvikabili vizuizi vilivyoko mbele yetu pamoja."

Chama cha SPD kiliongoza kwenye matokeo ya uchaguzi wa mwezi Septemba na sasa kinafanya mazungumzo ya kuunda serikaliPicha: Ralph Goldmann/picture alliance

SPD kiliongoza kwenye matokeo ya uchaguzi huo wa Septemba wa bunge. Chama hicho kinataka kuunda muungano wa serikali na vyama vya Kijani na FDP, maarufu kama "Traffic Light", kutokana na rangi za vyama hivyo.

Tofauti za kimsingi zilizopo.

Mkurugenzi wa kitaifa wa chama cha Kijani Michael Kellner amesema mazungumzo hayo yalikuwa ni ya kina na kuongeza kuwa kiwango cha kuaminiana kati yao kimeongezeka na tofauti zikizidi kuwa ndogo.

Vyama hivyo vitatu hata hivyo havikuzungumzia kwa kina majadiliano yao yaliyodumu kwa masaa 14 siku ya Jumatatu, vikisema vinataka faragha vinaposhughulikia kwanza tofauti zao zinazojikita katika masuala ya sera za kodi na namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ingawa itikadi za chama cha Kijani na SPD zinaonekana kukaribiana, lakini kuna tofauti kubwa kati yao na chama cha FDP na hasa yanapokuja masuala ya uchumi na sera za fedha. Ingawa SPD na Kijani wanaunga mkono ongezeko la wastani la kodi kwa matajiri, FDP wanapinga vikali hatua hiyo. Na kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi, FDP wanataka kuegemea zaidi nguvu ya soko tofauti na SPD na Kijani.

Uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni umeonyesha asilimia 51 ya waJerumani wanaunga mkono muungano wa serikali wa SPD, FDP na Kijani, huku wengi wakionyesha kutotaka chama cha Christian Democrats cha kansela Angela Merkel kuunganishwa kwenye serikali, ingawa kilishinda nafasi ya pili kwenye uchaguzi.

Soma Zaidi: Uhariri: Wajerumani wachagua mabadiliko

Iwapo makubaliano yatafikiwa siku ya Ijumaa, chama cha Kijani kimesema kitahitaji kufanya kongamano dogo la chama litakaloidhinisha uwepo wao ndani ya serikali. Wamesema watafanya mkutano huo siku ya Jumapili ili kutoa maamuzi haraka.

Mashirika: DW