1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: Mbio za kumrithi Angela Merkel zapamba moto

1 Novemba 2018

Mara tu baada ya Kansela Angela Merkel kutangaza kwamba atajizulu wadhifa wa mwenyekiti wa chama chake cha CDU mwezi ujao, watu kadhaa wamejitokeza kuwa tayari kushika wadhifa huo.

Berlin Merkel-Pressekonferenz nach Hessen-Wahl
Picha: Reuters/H. Hanschke

Watu watatu tayari wameshatangaza nia ya kugombea wadhifa wa mwenyekiti wa chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU) baada ya kansela Angela Merkel kutangaza kwamba hatagombea tena mamlaka hayo kwenye mkutano wa mwaka wa chamahicho utakaofanyika mjini Hamburg mapema mwezi ujao.

Watu hao ni katibu mkuu wa sasa wa chama hicho Annegret Kramp-Karrenbauer. Mama huyo mwenye umri wa miaka 56 anapewa nafasi ya mbele katika kinyang'anyiro cha kuiwania nafasi hiyo kwenye mkutano wa mwezi wa Desemba.

Katibu mkuu wa chama cha CDU Annegret Kramp-KarrenbauerPicha: picture-alliance/dpa/G. Fischer

Bibi Karrenbauer aliyepewa jina la utani la Merkel mdogo kwenye vyombo vya habari, ni mshirika wa ndani  wa kansela Merkel. Pamoja na sifa nyingine, Karrenbauer aliwahi kuwa waziri mkuu wa jimbo dogo la Saarland la magharibi mwa Ujerumani. Anawakilisha siasa za mrengo wa kati.

Aliibuka kuwa katibu mkuu wa chama cha CDU mnamo mwezi Februari, baada ya kumshinda vibaya mgombea wa chama cha SPD katika uchaguzi wa waziri mkuu kwenye jimbo hilo la Saarland uliofanyika  mwaka uliopita. Kuchaguliwa kwa Karrenbauer kuwa katibu mkuu wa chama cha CDU kulizingatiwa kuwa sehemu ya juhudi za chama hicho za kukiimarisha chama baada ya kupata kipigo kibaya katika uchaguzi mkuu.

Mwanasiasa mwengine anayepewa nafasi nzuri ya kumrithi Angela Merkel kama mwenyekiti wa chama ni Friedrich Merz ambaye mnamo miaka ya nyuma alikuwa mshindani mkubwa wa Merkel. Bwana Merz ndiye aliyekuwa wa kwanza kutangaza nia ya kuwa mwenyekiti wa CDU mara tu baada ya Angela Merkel kutangaza kuwa hatawania tena wadhifa huo. Bwana Merz amesema mwanzo mpya na unahitajika katika kambi ya wahafidhina chini ya viongozi vijana na wenye uzoefu.

Friedrich Merz, mwanasiasa aliyetangaza kugombea uenyekiti wa chama cha CDUPicha: Reuters/H. Hanschke

Merz amesema yuko tayari kuchukua wajibu wa uenyekiti na kwamba atafanya kila linalopasa ili kuimarisha mshikamano ndani ya chama cha CDU. Bwana Merz mwenye umri wa miaka 62 aliachana na shughuli za siasa mnamo mwaka 2009 ili kuendelea na kazi yake ya mwanasheria lakini baada ya kuzidiwa kete na Angela Merkel katika mivutano ya kisiasa ya ndani ya chama cha CDU. 

Mtu mwingine anayepewa nafasi ya kuchukua wadhifa wa mwenyekiti wa chama cha CDU baada ya Merkel  kuondoka ni waziri wa afya wa sasa Jens Spahn mwenye umri wa miaka 38. Kijana huyo anayetambulika  kuwa mkosoaji mkali wa Angela Merkel hakuficha nia yake ya kumrithi Merkel. Bwana Spahn ameshajaribu  kuwahamasisha miongoni mwa wahafidhina ndani ya chama cha CDU wamuunge mkono kwa kuukosoa msimamo wa wastani wa Angela Merkel juu ya wakimbizi. Spahn anataka kuwepo msimamo mkali juu ya suala la uhamiaji.

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens SpahnPicha: picture-alliance/NurPhoto/E. Contini

Waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia Armin Laschet ambaye ni mshirika wa ndani wa bibi Merkel pia anazo sifa za kuwa mwenyekiti wa CDU lakini kwa mujibu wa taarifa bado hajatangaza nia hiyo  hadharani. Bwana Laschet anatarajiwa kutangaza mwishoni mwa wiki hii iwapo atajitosa katika kinyang'anyiro hicho.

Pia mwanasiasa mkongwe mwenye tajiriba kubwa ya kisiasa Wolfgang Schäuble ataweza kujiliwaza ikiwa atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa CDU mwezi ujao. Schäuble mwenye umri wa miaka 76 aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, aliwahi kuwa waziri wa fedha kabla ya kuchaguliwa kuwa spika wa bunge la Ujerumani.

Mwandishi:Zainab Aziz/DPA/RTRE

Mhariri:Iddi Ssessanga

      

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW