1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merz: 2026 unaweza kuwa 'mwaka wa mwanzo mpya'

31 Desemba 2025

Kansela Friedrich Merz aligusia vita Ukraine, ongezeko la bajeti ya ulinzi, uhusiano unaobadilika na Marekani, mabadiliko ya kiteknolojia, kudorora kwa viwanda na mageuzi ya polepole katika hotuba yake ya Mwaka Mpya.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz akitoa hotuba ya mwaka mpya kwenye televisheni
Merz aliorodhesha changamoto zinazoikabili Ujerumani na ulimwengu mzima lakini akasema 'mikono yetu haijafungwa'Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela Friedrich Merz alianza hotuba yake ya kwanza ya televisheni kwa taifa kwa kukumbushia Februari 23 na uchaguzi wa mapema uliomfanya mhafidhina huyo kuwa kansela wa Ujerumani, akimshinda Olaf Scholz na serikali iliyoongozwa na chama cha Social Democratic.

"Ninyi, raia, mliamua kuhusu mustakabali wa kisiasa wa nchi yetu mnamo siku hiyo. Serikali mpya ya Shirikisho iliundwa ambayo imeazimia kuiongoza Ujerumani katika mkondo sahihi  kwa dhamira na mwelekeo wazi," Merz alisema hayo katika hotuba yake ya mwaka mpya. Hata hivyo, alikiri mara moja kwamba lengo hili halikuwa "kazi ndogo." Alisema mwaka wa 2025 uliipa Ujerumani na dunia nzima mfululizo wa changamoto kubwa.

"Vita mbaya inazidi kupamba moto barani Ulaya, vita ambayo inatishia moja kwa moja uhuru wetu na usalama wetu. Uchumi wetu unakabiliwa na shinikizo kutokana na mageuzi muhimu, gharama kubwa na migogoro ya biashara duniani. Zaidi ya hayo, teknolojia mpya zinabadilisha ulimwengu wetu wa kazi na jinsi tunavyoishi pamoja," Alisema Merz.

Katika hali hii, Merz alisema, serikali yake iliona jukumu lake la msingi kuwa ni "uboreshaji upya wa misingi ya uhuru wetu, usalama wetu na ustawi wetu."

Hotuba ya Merz ya mwaka mpya itarushwa kwenye Televisheni Jumatano usikuPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Vita vya Urusi nchini Ukraine 'sehemu ya mpango unaolenga Ulaya nzima'

Kuiboresha misingi hii kunawezekana tu "ikiwa tutalinda amani barani Ulaya," kansela huyo alisema, akibainisha jinsi Ukraine itakavyoukaribisha Mwaka Mpya wa nne mfululizo "chini ya mazingira magumu zaidi." Merz alisisitiza kwamba vita nchini Ukraine vinaihusu pia Ujerumani.

"Ni wazi zaidi kwamba uchokozi wa Urusi ulikuwa, na ni sehemu ya mpango unaoilenga Ulaya nzima, akiongeza kuwa Ujerumani ilikabiliwa na vitendo vya hujuma, ujasusi na mashambulizi ya mtandaoni kila siku.”

Baadaye kansela huyo alibainisha mipango ya serikali yake ya kuongeza bajeti ya ulinzi na kutekeleza sera ya huduma ya kijeshi ya hiari kwa baadhi ya vijana, ikiwa ni pamoja na mageuzi ya kikatiba ili kuwezesha kukopa zaidi na kulifadhili jeshi.

Ushirikiano na Marekani 'unabadilika'

Ingawa kansela hakuunganisha moja kwa moja wazo hilo na vita vya uchokozi vya Urusi au ongezeko la matumizi ya ulinzi ya Ujerumani, pia alirejelea uhusiano unaobadilika na Marekaniwakati Donald Trump aliporejea Ikulu ya White House.

Makubaliano ya kibiashara kati ya Marekani na Ulaya

12:25

This browser does not support the video element.

 "Wakati huo huo, ushirikiano wetu na Marekani, ambayo kwa muda mrefu amekuwa mdhamini wa kuaminika wa usalama wetu, unabadilika," Alisema Merz. "Kwetu sisi Ulaya, hii ina maana kwamba lazima tulinde na kutetea maslahi yetu kwa nguvu zaidi sisi wenyewe."

Udhaifu wa kiuchumi, mageuzi ya polepole nchini na barani Ulaya

Kiongozi huyo wa chama cha Christian Democratic, mwenye uzoefu katika sheria za makampuni mbali na siasa, alilalamika kuhusu kile alichokiita "kurudi kwenye ulinzi wa masoko katika uchumi wa dunia." "Utegemezi wa kimkakati wa Ujerumani kwa malighafi unazidi kutumiwa kama njia ya ushawishi wa kisiasa dhidi ya maslahi yetu," alisema, huku Ujerumani kama taifa linalosafirisha nje ikihisi athari zake haswa, akiashiria matatizo ya kifedha kwa viwanda vikubwa kama vile vya kutengeneza magari.

Alisema serikali yake inatafuta njia za kuweka unafuu katika maeneo ikiwemo kodi, bei za nishati na kupunguza urasimu.

Lakini Merz pia alisema kwamba "mrundikano wa mageuzi ya ndani unadhoofisha uwezo wa makampuni yetu," wakati hasa ambapo ubunifu na uvumbuzi wa uchumi unahitajika ili kukabiliana na shinikizo la kimataifa.

Kansela aligusia ugumu wa kutekeleza mageuzi kadhaa muhimu, kama vile mabadiliko ya ustawi wa jamii na pensheniPicha: Michael Gstettenbauer/IMAGO

Mwaka wa 2026 unaweza kuwa 'mwanzo mpya'

Kansela huyo aligusia kukatishwa tamaa kwa umma kutokana na mapigano ya ndani ya serikali yake ya muungano na ugumu wa kutekeleza mageuzi kadhaa muhimu, kama vile mabadiliko ya ustawi wa jamii na pensheni, kwa kukubali kwamba wengi wanahisi mafanikio ya serikali hadi sasa "hayatoshi."

"Na nataka kuwaambia kwamba mko sahihi! Hayatoshi," Alisema Merz. Lakini alihoji kwamba kazi hiyo imeanza na kwamba ana uhakika Ujerumani "itavuna faida za mageuzi haya, hata kama itachukua muda."

Kansela alisema kwamba mwaka wa 2026 unaweza kuwa "mwaka wa mwanzo mpya," ambapo Ujerumani na Ulaya "zitaungana tena na miongo ya amani, uhuru na ustawi."

Alisema maendeleo mbalimbali ya kijiografia, kiuchumi na kiteknolojia yalisababisha "mabadiliko ya nyakati," lakini akasema ni juu ya Ujerumani kumudu changamoto hizo kwa nguvu zake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW