Ujerumani: Mwenyekiti mpya wa baraza la Umoja wa Ulaya
28 Mei 2020Sera hizo ni pamoja na mahusiano na Urusi pamoja na suala la mgogoro wa kiafya linaloendelea kwa sasa.
Nafasi ya rais wa baraza la Umoja wa Ulaya ni ya kuzunguka,mara mbili kwa mwaka nchi mwanachama tofauti anachukua uongozi wa baraza hilo,kwa maneno mengine ni nafasi ya miezi sita, nchi ikihusika kuandaa mikutano ya ngazi ya juu pamoja na kuwa kiungo kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo katika kufikia maridhiano kuhusu masuala muhimu.
Lakini pia anayeshikilia uongozi wa baraza hilo anahusika kusukuma mbele agenda za jumuiya hiyo ya Umoja wa Ulaya. Kansela Angela Merkel akizungumza mjini Berlin siku ya Jumatano amesema hasa Ujerumani itajikita zaidi katika kuimarisha mahusiano na Urusi kupitia mdahalo utakaolenga kutowa mtazamo wa kukosoa lakini pia kujenga.
Kauli hii ya Merkel imekuja kabla ya mazungumzo kwa njia ya mtandao yaliyoandaliwa na wakfu wa Konrad Adenauer. Aidha Kansela Merkel alisisitiza umuhimu wa kuendeleza mahusiano mazuri na Marekani kwa ajili ya Ujerumani na Ulaya akisema mshirika muhimu zaidi ni Marekani.
Merkel amekiri kwamba kwa sasa ushirikiano na Marekani ni mgumu kuliko ambavyo angependelea linapohusika suala la sera ya biashara na Mazingira na umuhimu wa mashirika ya kimataifa kufuatia mgogoro wa kiafya uliopo kwa wakati huu duniani.
Hata hivyo kilichowazi ni kwamba Merkel amebaini uhusiano kati ya Ulaya na Marekani ni nguzo kuu ya sera ya kigeni na usalama na kwahivyo hawapaswi kusahau kwamba Ulaya haisimami peke yake.
Ulaya ni sehemu ya siasa za Magharibi. Katika suala zima la Urusi Kansela huyo wa Ujerumani amefafanua kwamba ni muhimu iwekwe wazi kwamba katika uhusiano wa kimataifa hakuna suala la sheria ya mwenye nguvu bali ni nguvu ya sheria.
Na katika hilo mikataba ya Umoja wa Ulaya kuhusu haki za binadamu pia inahusika. Ikumbukwe kwamba Urusi mara kadhaa imekwenda kinyume kwa kupinga sheria na kanuni hizi amesema Kansela Merkel huku akitaja kwamba nchi hiyo imetengenezá msururu wa migogoro na kuinyakua kwa nguvu rasi ya Crimea ambalo ni eneo la Ukraine katika hatua ambayo imekiuka sheria ya kimataifa.
Lakini pia kiongozi huyo wa Ujerumani hakuchelea kusema wazi kwamba nchi hiyo ya Urusi imeunga mkono tawala za vibaraka wake katika maeneo ya Mashariki mwa Ukraine na kuanzisha mashambulizi dhidi ya nchi za Magharibi zenye demokrasia ikiwemo Ujerumani.
Na kwa maana hiyo akaongeza kusema, hapana shaka Urusi itaendelea kuhodhi agenda za Ujerumani kama rais wa Umoja wa Ulaya.
Lakini pia masuala mengine yatakayochukua nafasi ni Libya,Syria,ulinzi wa mazingira pamoja na suala la afya duniani. Kadhalika Ujerumani inatarajia kushughulikia suala la uhusiano wa baadae kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya,pamoja na mfumo ulaya kuhusu hifadhi ya wakimbizi.
Mtazamo wa kansela Merkel inaonesha kwamba anatarajia Ulaya inaweza kuondokana na mgogoro wa janga la kirusi cha Corona ikiwa na nguvu kuliko ilivyotumbukia kwenye janga hilo.
Steffen Seibert ambaye ni msemaji wa serikali nae katika mkutano uliofanyika hapo kabla kati ya Kansela Merkel na maafisa wa ngazi ya juu wa bunge la Ulaya,akasisitiza kwamba kuliangazia suala la kirusi hicho haikuwa wakati wote mpango wa Ujerumani lakini janga hilo limeilazimisha serikali mjini Berlin kuandaa upya mpango wake wa kipindi cha miezi sita. Rasimu ya Ujerumani inayoweka wazi mipango yote ya Ujerumani kama rais wa Umoja wa Ulaya itatolewa katika kipindi cha siku kadhaa kuelekea Julai Mosi.