Ujerumani: Mzozo kuhusu hati ya kukamatwa kwa Netanyahu
30 Novemba 2024Alhamisi ya wiki iliyopita, uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague uliiweka serikali ya Ujerumani katika hali ngumu: Mahakama hiyo ilitoa hati ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, na Waziri wa Ulinzi wa Israeli aliyeachishwa kazi hivi karibuni, Yoav Galant. Sababu iliyotolewa ni kuwa wote wawili wameshutumiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kutokana na hatua zao za kijeshi katika Ukanda wa Gaza.
Ujerumani imekuwa mojawapo ya nchi 124 zilizotia saini tangu kuanzishwa kwa Mahakama ya Kimataifa mwaka 2002 na inachukuliwa kuwa mfadhili wa kudumu wa mahakama hiyo. Lakini, kutokana na mauaji ya Holocaust dhidi ya Wayahudi wa Ulaya wakati wa utawala wa Wanazi, pia inajulikana kama mshirika wa karibu wa Israeli.
Barenboim: "Maisha ya kibinadamu ni magumu Gaza"
Ijumaa ya wiki hii, wataalam kadhaa kwenye mkutano wa waandishi wa habari wa serikali ya shirikisho mjini Berlin waliutaja uamuzi kutoka The Hague kama mwito wa uamsho kwa serikali ya Ujerumani. Serikali hiyo ilikuwa ikisisitiza kuwa serikali ya Israeli ilikuwa na haki ya kujilinda hata kwa njia kali baada ya shambulio la kigaidi la Oktoba 2023.
Soma pia: Viongozi wa dunia watofautiana kuhusu waranti wa ICC wa kukamatwa Netanyahu
Christine Binzel, Profesa wa Uchumi na Jamii ya Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Erlangen-Nürnberg, alisema Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu imekuwa ikilaani mara kwa mara hatua za Israel. Hata hivyo, Ujerumani ililikatia mahakama hiyo msaada wake: "Ujerumani haijatimiza wajibu huo kwa miezi 14. Ujerumani haikuangalia tu, serikali ya shirikisho inaendelea kuiunga mkono Israel kisiasa, kifedha, kijeshi, na kisheria. Ujerumani ni mtoaji wa pili mkubwa wa silaha baada ya Marekani."
Na Michael Barenboim, mwanamuziki na profesa katika Chuo cha Barenboim-Said, aliongeza: "Tangu mwanzoni mwa Oktoba 2024, Israel imeweka kaskazini mwa Gaza katika hali kamili ya mzingiro na kufanya maisha ya kibinadamu kuwa magumu huko."
Nini kitatokea Netanyahu akitembelea Berlin?
Kwa serikali ya Ujerumani, tangu uamuzi wa The Hague, swali lingine lilikuwa katika kitovu: Nini kingetokea kama kiongozi wa serikali ya taifa rafiki la Israel angekuja Berlin sasa? Kimsingi, mfumo wa haki wa Ujerumani ungemkamata Netanyahu.
Hata hivyo, ziara kama hiyo haipo wakati huu, tangu shambulio la wanamgambo wa kigaidi wa Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana, Netanjahu hajakuwa sana nje ya nchi, ziara yake ya mwisho Berlin ilikuwa Machi 2023.
Wiki iliyopita, msemaji wa Kansela wa Shirikisho Olaf Scholz, Steffen Hebestreit, alisema Ujerumani inapaswa kufikiria mambo yote mawili: mshikamano na Israel kama taifa na pia kuunga mkono sheria za kimataifa: "Hapo kuna umuhimu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ambayo tunaunga mkono sana, na pia kuna jukumu la kihistoria.
Soma pia: Erdogan apongeza ujasiri wa ICC kwa viongozi wa Israel
Ningejikuta nikisema kuwa ni vigumu kwangu kufikiria kwamba tungetekeleza ukamataji hapa Ujerumani kwa msingi huo." Wakati huo pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock (wa Chama cha Kijani) alizungumzia kuwa serikali inapaswa kuchunguza suala hilo kwa uangalifu.
Uchunguzi wa Kisheria nchini Israel?
Kwa sasa, inaonekana Baerbock anasema kwa njia tofauti kidogo: "Serikali ya Shirikisho inafuata sheria na haki, kwa sababu hakuna mtu aliye juu ya sheria," alisema mwanasiasa huyo wa chama cha Kijani pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G7 huko Fiuggi, Italia. Aliendelea kusema: "Uhuru wa mfumo wa haki ni muhimu, na katika kesi hii umefikia hitimisho kwamba kuna dalili za kutosha kuendeleza hatua hii sasa."
Njia mojawapo ya kutoka katika hali ngumu hii, kwa mujibu wa baadhi ya wanasiasa wa Ujerumani, ni kwamba: Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huchukua hatua tu pale ambapo nchi husika haiwezi kuwafungulia mashtaka wanasiasa wake kwa uhalifu. Kwa hivyo, Ujerumani inapaswa kushinikiza ili uchunguzi wa kisheria ufanyike nchini Israel baada ya vita kumalizika, ambao unaweza pia kuhusisha jukumu la Netanyahu.
Hivyo ndivyo anavyoeleza Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje katika Bundestag, Michael Roth (SPD): "Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu inapoteza uaminifu wake kwa kiwango kikubwa, kwa sababu haiwafuatilii wahalifu wa vita na madikteta kama Bashar al-Assad, lakini inamfuatilia kiongozi wa serikali ya nchi yenye mfumo huru wa haki kupitia hati ya kukamatwa."
Marekani inasimama imara upande wa Israel
Rais wa Marekani, Joe Biden, ameonyesha wazi kuunga mkono serikali ya Israel. Kama ilivyo kwa Israel, Marekani na Urusi haziitambui Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Biden alisema: "Nirudie tena kwa uwazi: Lolote lile ambalo ICC inaweza kudokeza, Israel na Hamas si sawa – hata kidogo," alisema Biden.
Alikuwa akirejelea ukweli kwamba hati ya kukamatwa haikutolewa tu dhidi ya dhidi ya wanasiasa wawili wa Israel, bali pia dhidi ya mwanachama mmoja wa ngazi ya juu wa Hamas. Biden aliendelea kusema: "Tutakuwa daima upande wa Israel, pale usalama wake unapokuwa hatarini."
Na msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karine Jean-Pierre, alisema, Marekani haitatekeleza hati yoyote ya kukamatwa kwa maafisa wa Israel. Vile vile, Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, alionyesha msimamo sawa kwa kumwalika Netanjahu kwa makusudi kwenda Budapest.
Aliongeza kuwa, bila shaka, Netanjahu hatakamatwa wakati wa ziara hiyo.