1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Japan na Ujerumani kushirikiana zaidi

5 Februari 2019

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amefanya mazungumzo na mfalme wa Japan Akihito kabla ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili nchini humo. mataifa hayo yamekubaliana kushirikiana zaidi.

Bundeskanzlerin Merkel in Japan
Picha: picture-alliance/dpa/Jiji Press

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amefanya mazungumzo na mfalme wa Japan Akihito hii leo kabla ya kuhitimisha ziara yake ya siku mbili nchini humo, kabla ya kukutana na mwana mfalme hapo baadae, anayetaraji kurithi kiti hicho hivi karibuni. 

Kansela Merkel amekutana na mfalme huyo mkongwe wa miaka 85, aliyeamua kulivua taji lake April 30, tukio la aina yake kuwahi kushuhudiwa tangu miaka 200 iliyopita nchini humo. baadae hii leo, Kansela Merkel atakutana pia na mrithi wa kiti cha ufalme, Mwanamfalme Naruhito atakayekabidhiwa waadhifa huo May mosi inayokuja. 

Ziara yake hii ya tano nchini humo inakuja siku tatu tu baada ya makubaliano ya ushirikiano wa kikanda wa kiuchumi, EU-EPA ambayo ni makubwa zaidi ya biashara huru yaliyofikiwa kati ya Japan na Umoja wa Ulaya na yaliyoanza kutekelezwa Februari Mosi. Makubaliano hayo yanafikia theluthi ya uchumi wa dunia. Kansela Merkel alisema hapo jana kwamba hatua hiyo ni ujumbe tosha kwa dunia.

Merkel na Abe wamekubaliana kuimarisha zaidi mashirikiano ya kiuchumi kupitia EU-EPAPicha: Reuters/F. Robichon

Hapo jana, Kansela Merkel alikutana na waziri mkuu Shinzo abe, na kujadiliana kwa kina masuala kadhaa kuanzia uchumi hadi Teknolojia. Kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo, Abe alisema Japan na Ujerumani zinataraji kuongoza ukanda huo mkubwa zaidi wa kiuchumi duniani.

Alisema "Japan na Ujerumani zitakuwa vinara wa ukanda huu mkubwa zaidi wa uchumi huru, ulioanzishwa chini ya mkataba wa mashirikiano ya kiuchumi, EPA, na ulioanza kutekelezwa siku ya kwanza ya mwezi huu. Kwa mantiki hiyo, tunatakiwa kupunguza athari za Brexit kwa Umoja wa Ulaya na uchumi wa kidunia kwa ujumla."

mfumo wa 5G umezua mjadala mkubwa nchini UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa/Z. Min

Aidha wakuu hao wamekubaliana kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na kuhamasisha mashirikiano katika eneo la teknolojia ya juu ikiwa ni pamoja na ujasusi bandia na makubaliano ya msingi kuhusu usalama wa taarifa ili kuimarisha mashirikiano ya kiulinzi.

Aidha, Abe na Merkel wamethibitisha kushirikiana katika kuhakikisha mkutano ujao wa kilele wa kundi la mataifa yaliyoinukia kiuchumi duniani, G20 unakuwa wa mafanikio. Japan itakuwa mwenyeji wa mkutano huo, katika mji wa Osaka, mnamo mwezi Juni.

Kansela Merkel, aliyewasili Japan jana Jumatatu, alizungumza pia na wanafunzi wa chuo kikuu cha Keio, mjini Tokyo, alikotoa mwito wa ulinzi katika kuhakikisha makampuni ya Kichina hayatoi taarifa binafsi kwa Beijing, katika wakati ambapo kunaongezeka wasiwasi wa kiusalama dhidi ya vifaa vilivyotengenezwa na kampuni kubwa ya mawasiliano ya Huawei.

Amesema, kuna mjadala mkubwa nchini Ujerumani kuhusu matumizi ya  vifaa vya Huawei, wakati hakuna ongezeko la miito ya kuizuia kampuni hiyo kutounda mfumo mpya wa mawasiliano wa kiwango cha 5G, unaoeleezwa kushika nafasi ya akili ya mwanadamu.

Mwandishi: Lilian Mtono/dw/DPAE/AFPE

Mhariri:

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW