Ujerumani na Ufaransa, Brazil wanamiadi na Colombia
4 Julai 2014Brazil ilifanikiwa tu kujipenyeza katika awamu hii ya robo fainali kwa kuiondoa kwa taabu Chile kwa mikwaju ya penalti, wakati Colombia , ikiwa na mfungaji bora hadi sasa katika kinyang'anyiro hiki James Rodriguez mwenye mabao matano , wameshinda michezo yao yote minne katika fainali hizi na kupachika mabao 11 na kufungwa mawili tu hadi sasa.
Kocha wa Brazil Luiz Filipe Scolari anaamini kuwa kutokuwapo kwa uhasama kati ya kikosi chake na Colombia kutaruhusu mchezo mzuri kuonekana leo.
Makamanda wa Scolari walihitaji mikwaju ya penalti na dakika 120 kuweza kuwashinda nguvu Chile katika awamu ya mtoano ya timu 16, mchezo ambao ulisababisha wengi wa wachezaji wa Brazil kumwaga machozi mwishoni mwa mchezo huo.
Scolari ana matumaini
Hata hivyo Scolari mwenye umri wa miaka 65 ana matumaini kuwa pambano la leo litakuwa si la kupimana ubavu zaidi na kuruhusu wachezaji wake kuonesha kile wanachokiweza zaidi, samba ya Brazil.
Colombia ni timu inayocheza kwa ustadi zaidi kuliko Chile, amesema Scolari.
Chile inacheza kwa nguvu zaidi na wanacheza kwa moyo hali inayoufanya mchezo kuwa tofauti kabisa, ameongeza Scolari.
Ujerumani ina miadi na Ufaransa katika mchezo wa kwanza leo jioni na matokeo ya mchezo huo yanaelekeza katika nusu fainali dhidi ya Brazil ama Colombia mjini Belo Horizonte hapo Julai 8 licha ya maswali kadha kuhusiana na uchezaji wa kikosi cha kocha Joachim Loew.
Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps ameamua kupuuzia vipigo mara mbili katika nusu fainali dhidi ya Ujerumani mwaka 1982 na 1986 wakati Les Bleus, ambao wamepachika wavuni mabao 10 katika mashindano haya katika michezo yao minne, wanawania kuendeleza uwezo wao wa kupachika mabao.
Kibarua kigumu kwa Ujerumani
Mchezo huu unaonekana kuwa ni kibarua kigumu kwa Ujerumani katika fainali hizi hadi sasa , nini kinaonekana kizuri zaidi kwa Ufaransa. Jibu analo mchezaji wa zamani wa Ufaransa Valerie Ismail.
"Ufaransa imeanza kucheza kama timu kadri kombe la dunia linavyoendelea na kuonekana kuwa ni timu inayocheza kwa pamoja, na sio kama ilivyokuwa mwaka 2010, na hii ndio inakifanya kikosi cha Ufaransa kuwa hatari."
Wakati huo huo polisi mjini Rio de Janeiro wamemtambua afisa wa FIFA jana ambaye wanamtuhumu kusaidia genge la wanaotuhumiwa kufanya juhudi za kuuza tena tikiti za kombe la dunia, ikiwa ni pamoja na zile ambazo tayari zimepangiwa wachezaji.
Katika uchunguzi ambao mapema wiki hii umesababisha kukamatwa kwa kundi la watu 11 wanaotuhumiwa kuuza tikiti hizo, polisi imesema wamefichua jina la kwanza la afisa wa FIFA anayedaiwa kuhusika na uhalifu huo kutokana na simu alizopiga.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Mohammed Khelef