Ujerumani na Ufaransa kuzidi kushirikiana kukabil mizozo.
29 Januari 2017Mawaziri hao wameshutumu marufuku ya wakimbizi kuingia Marekani iliowekwa na Trump.Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel ameahidi Jumamosi(28.01.2016) kushirikiana kwa karibu na Ufaransa ili kuimarisha mshikamano wa wa Ulaya wakati vitisho vya Urusi vikiongezeka mashariki mwa Ulaya na kule kunaonekana kupooza kwa uhusiano wao na Marekani.
Katika ziara yake ya kwanza ya kigeni akiwa waziri wa mambo ya nje Gabriel amewaambia waandishi wa habari mjini Paris "Ulaya haina haja kuwa hofu na mustakbali wake hatuna sababu ya kuwa wanyenyekevu au kujizuwiya"
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault ameyakinisha shauku ya pamoja ya Ufaransa na Ujerumani kuwepo kwa Ulaya madhubuti kwa kusema "Iwapo na Ujerumani na Ufaransa zitakuwa zinaelekea kwenye mwelekeo mmoja na zinafikiri kwa mwelekeo huo huo mmoja hapo tena Ulaya itakuwa inasonga mbele."
Kukabiliana na mizozo ya nje
Mawaziri hao pia wameahidi makundi ya kazi kati ya nchi hizo mbili katika kukabiliana na masuala makuu ya nje likiwemo mzozo wa Urusi na Ukraine.
Gabriel amesema Ujerumana na Ufaransa zimekubaliana kwmaba hatua zozote za kuiondolea Urusi vikwazo lazima zihusishwe na hatua za maendeleo zitakazofikiwa kuelekea amani mashariki ya Ukraine.
Gabriel amesema " Sisi nchini Ujerumani na Ufaransa tuna msimamo ulio wazi kwa suala la vikwazo na tunataka kutekelezwa kwa mchamakato wa amani wa Minsk ......hiyo ndio njia pekee ambapo vikwazo vinaweza kuondolewa."
Licha ya juhudi za Ujerumani na Ufaransa kutaka kutekelezwa kwa Makubaliano ya Minsk ya mwaka 2015 hakuna hatua kubwa zilizopigwa katika mchakato huo wa amani.Rais mpya wa Marekani Donald Trump amedokeza yumkini akaondowa vikwazo vya Marekani viliowekwa dhidi ya Urusi.
Mapigano yaendelea mashariki mwa Ukraine
Licha ya majaribio ya kuleta amani huko Ukraine vikosi vinaendelea kupambana dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi mashariki mwa nchi hiyo.
Gabriel na Ayrault wameushutumu uamuzi wa kusitisha mpango wa wakimbizi wa Marekani.Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani agizo la rais lililotolewa Ijumaa kuwapiga marufuku wakimbizi kutoka nchi fulani zenye idadi kubwa ya Waislamu unakwenda kinyume na mila za jadi Wakristo nchini Marekani ya "umpende jirani yako."
Ayrault amesema kuzuiliwa huko kwa wakimbizi kunawatia tu mashaka na kwamba "kuwakaribisha wakimbizi ambao wanakimbia vita na ukandamizaji ni sehemu ya wajibu wetu."
Mawaziri hao wa mambo ya nje wa Ujerumani na Ufaransa pia wamesema wanapanga kuwa na mkutano wa pamoja na mteuliwa wa Trump wa wadahifa wa waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson mara tu atakapochaguliwa rasmi Ili "kujadili suala hilo kipengele kwa kipengele na kuwa na uhusiano ulio wazi."
"Ufasaha,kupatana na ikibidi uthabiti vinahitajika kutetea imani zetu,maadili yetu ,dira yetu kwa dunia ,maslahi yetu ya Ufaransa, Ujerumani na Ulaya." amesema hayo Ayrault.
Katika dhima yake mpya akiwa waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Gabriel anatarajiwa kuelekea Brussels hapo Ijumaane kwa mazungumzo na maafis wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/Reuters/dpa
Mhariri : Isaac Gamba