1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatakiwa kuiachia meli yenye bendera ya Uingereza

20 Julai 2019

Ujerumani na Ufaransa zimelaani hatua ya Iran kuikamata meli yenye bendera ya Uingerea katika mlango wa bahari wa Hormuz na zimeitaka nchi hiyo kuiachia huru meli hiyo mara moja.

Öltanker Stena Impero
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. M. Karatzas

Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imeandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba sio sawa kuingilia shughuli za meli za biashara na hatua hiyo inazidisha mvutano ambao tayari upo. Ujerumani imetoa wito wa kuachiwa mara moja meli hiyo pamoja na wafanyakazi wake na imesema kwamba iko pamoja na Uingereza.

Kwa upande wake wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imeelezea mshikamano thabiti na ushirikiano na Uingereza.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, hatua ya Iran kuiteka meli yenye bendera ya Uingereza ni kutoheshimu uhuru wa kusarifi kwenye maji katika Ghuba ya Uajemi. Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amekuwa akiongoza juhudi za kupunguza mvutano uliopo na kuazisha mazungumzo.

Shirika la habari la Iran-ISNA, limeripoti kuwa maafisa waliikamata meli inayoitwa Stena Impero pamoja na wafanyakazi wake 23 siku ya Ijumaa, baada ya kudai kuwa iligongana na meli ya uvuvi. Jeshi la Mapinduzi nchini Iran limesema liliikamata meli hiyo baada ya kukiuka kanuni za kimataifa za usafiri wa bahari katika mlango wa bahari wa Hormuz, eneo muhimu linalopitisha karibu theluthi ya mafuta ghafi duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian na mwenzake wa Ujerumani, Heiko MaasPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/M. Euler

Meli nyingine ilikamatwa

Kikosi hicho cha walinzi wa mapinduzi pia kimesema kiliikamata meli nyingine ya mafuta ya Uingereza iliyokuwa na bendera ya Liberia iitwayo MV Mesdar, kabla ya kuiachia huru na kuiruhusu kuondoka.

Siku ya Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Jeremy Hunt alisema kuwa uamuzi wa kuikamata meli ya Stena Impero unaonesha dalili ya wasiwasi kwamba Iran inachukua njia ya hatari isiyo ya halali na inaonesha tabia ya kusababisha kukosekana kwa utulivu.

Matukio hayo yametokea saa chache baada ya mahakama ya Gibraltar kusema kuwa inarefusha kwa siku 30 kushikiliwa kwa meli ya mafuta ya Iran inayoitwa Grace 1, iliyokamatwa katika ardhi ya Uingereza mwanzoni mwa mwezi Juni kwa madai ya kuikuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa kusafirisha mafuta kinyume cha sheria kwenda Syria.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Jeremy HuntPicha: picture-alliance/AP Photo/F. Seco

Kutokana na hilo, Iran ilitishia kuziteka meli za mafuta za Uingereza ikiwa ni katika kulipiza kisasi, hatua iliyoilazimu Uingereza kupeleka meli zaidi za kivita katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Wakati huo huo, Shirika la habari la Iran-ISNA, limeripoti kuwa meli ya mafuta yenye bendera ya Uingereza iliyokamatwa na Iran, haikuwa na mzigo wowote. Hayo yameelezwa na mkuu wa shirika la bandari na masuala ya baharini, Allahmorad Afifipour kwenye jimbo la Hormozgan.

Afifipour amebainisha kuwa wafanyakazi 23 wa meli hiyo wanaweza wakahojiwa kuhusu masuala ya kiufundi. Amefafanua kuwa iwapo italazimika, na kwa ombi la maafisa wa mahakama, wafanyakazi hao wanaweza wakaitwa kwa mahojiano ya kiufundi na kiutaalamu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW