1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani na Uhispania zaanza vizuri

Admin.WagnerD13 Juni 2016

Mabingwa wa dunia Ujerumani waanza vizuri mashindano ya kombe la mataifa ya Ulaya Euro 2016. Mabingwa watetezi Uhispania yaanza kutetea taji lake lao.

Frankreich UEFA EURO 2016 Fußball EM Deutschland - Ukraine
Shkrodan Mustafi akishangiria bao la kwanza kwa UjerumaniPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Probst

Nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani , Die Manschaft , Manuel Neuer na Toni Kroos wameonya kwamba mabingwa wa dunia wataendelea kuja juu baada ya kuwatupilia kando Ukraine kwa kuwafunga mabao 2-0 jana Jumapili mjini Lille na kuanza vizuri kampeni ya mashindano ya Euro 2016.

Mashabiki wa Ujerumani katika Euro 2016Picha: DW/M. Drabok

Kroos alitajwa kuwa mchezaji bora katika mtanange huo na mlinda mlango Manuel Neuer aliokoa mikwaju kadhaa ambayo ilionekana kabisa kutinga wavuni wakati Ukraine ikitishia kuwavimbua mabingwa hao wa dunia ambao ngome yao ya kuunga unga imedhoofishwa na kuumia kwa Mats Hummels na Antonio Rediger.

Hata hivyo , goli la mapema la Shkrodan Mustafi na goli la kwanza katika mchezo wa kimataifa kwa muda wa miaka mitano la Bastian Schweinsteiger, katika dakika za majeruhi , liliwapa vijana wa kocha Joachim Loew mwanzo mzuri katika juhudi zao kufikia mafanikio waliyoyapata Brazil miaka miwili iliyopita.

Mario Goetze akipita katikati ya wachezaji wa UkrainePicha: picture-alliance/Citypress24

"Kukimbia kwenda mbele, huo ndio uwezo wangu kwa kweli na mpira ule haukuwa rahisi hivyo kuufanyia kazi. Lakini , kwa maajabu, ndivyo ilivyokuwa. Unaweza tu kuwa na matarajio. Kwa mwaka huu nimekuwa pengine na dakika 300 tu za kucheza uwanjani, halafu haya yanatokeo."

"Tulicheza vizuri na kuweka viwango vyetu katika ulinzi," amesema Manuel Neuer. Hatujaonesha bado kila kitu ambacho tunapaswa kukionesha, tutaendelea kuwa bora." Ameongeza Neuer.

Jerome Boateng wa Ujerumani akiondisha mpira katika lango lakePicha: Reuters/B. Tessier

Mpira wa krosi uliopigwa na Kroos ulitengeneza bao la kwanza, lakini Kroos amekiri kwamba Ukraine ilikosa bahati na kushindwa kusawazisha kabla ya mapumziko wakati kazi kubwa ya Neuer na Jerome Boateng kufuta bao katika mstari kuliwazuwia.

Shkrodan Mustafi mlinzi wa Valencia ya Uhispania amesema anafuraha kuweza kufunga bao.

"Kwangu mimi nafurahi, kufunga bao, lakini ilikuwa ni muhimu kwanza kuanza na ushindi katika mashindano haya. hususan bila kufungwa bao. Kwetu sisi ni mafanikio makubwa, kwa kuwa tumeshinda na kupata pointi tatu na bila kufungwa bao, ambapo katika mashindano kama haya ni muhimu sana , na tumefanikisha kila kitu.

Bastian Schweinsteiger akikumbatiana na Manuel Neuer baada ya mchezoPicha: picture-alliance/augenklick/GES/M. Giliar

Ilikuwa usiku maalum kwa Schweinsteiger , ambaye amecheza kwa dakika 23 tu tangu alipopata maumivu ya goti Machi mwaka huu, lakini aliweza kupambana kuweza kuwa fit ili kuwa katika timu hiyo akiwa ni nahodha.

Kocha Joachim Loew akimzungumzia Schweinsteiger amesema.

"Kwa kweli hatukupanga, kwamba awe anakwenda mbele . Nilimwambia kwamba , kuna dakika chache zilizobakia na aende kuleta utulivu na kuweka mambo sawa uwanjani. Nilitaka kwa kweli mtu mwenye uwezo wa ulinzi katikati, ili tuweze kunasa mipira inayorudi kutoka katika mashambulizi, kwa kuwa Ukraine wamekuwa wakicheza mipira mingi ya mbali. Na mipira inayorudishwa ni lazima tuipate."

Neuer alikuwa nahodha usiku wa jana badala ya Schweinsteiger, lakini ana matumaini kuwa mchezaji mwenzake wa zamani wa Bayern atakuwa fiti na kuchukua jukumu kubwa hadi mwisho wa mashindano haya.

Wachezaji wa timu ya taifa ya UjerumaniPicha: picture-alliance/Revierfoto

Tathmini kwa walinda mlango

Wakati Neuer akifanya vizuri langoni mwake siku tatu baada ya kuanza kwa mashindano haya ya Euro 2016 , baadhi ya walinda mlango tayari wamegonga vichwa vya habari kwa sababu ambazo ni kinyume na ubora wao, wakifanya makosa ama juhudi za hovyo baada ya michezo saba tu ya mashindano haya.

Gazeti la Ujerumani la Sueddeutsche Zeitung limewakumbusha wasomaji wake kwamba walinda mlango "wanaweza kufanya mambo mazuri kwa dakika 89 lakini iwapo watafanya kosa moja katika nusu dakika mazungumzo baadaye ni kuhusu tu makosa hayo.

Wachezaji wa Uhispania wakishangiria bao lao la ushindiPicha: Getty Images/I. Walton

Tathmini hiyo imekuja katika michezo saba iliyokwisha fanyika katika Euro 2016, ambayo imeshuhudia makosa mawili, kutoka kwa Etrit Berisha wa Albania na mlinda mlango wa Romania Ciprian Tatarusanu, na kudokeza kwamba Matus Kocacik wa Slovakia na Volkan Babacan wa Uturuki wangeweza kufanya vizuri zaidi langoni mwao badala ya kuruhusu mabao kirahisi.

Na mlinda mlango wa Hungary Gabor Kiraly , mmoja kati ya walinda mlango machachari , anatarajiwa kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kucheza katika mashindano ya Ulaya pale atakapojitokeza na timu yake kesho kwa ufunguzi wa michuano ya kundi F dhidi ya Austria.

Akiwa na umri wa miaka 40 na miezi miwili, atampiku Lothar Matthaaeus wa Ujerumani , alipocheza katika michuano ya Euro 2000.

Gerard Pique akifunga bao kwa kichwaPicha: Reuters/V. Kessler

Mlinda mlango huyo mwenye upara anatambulika duniani kwa kuwa mlinda mlango pekee anayefaa suruali ya joging, akiivaa kulinda magoti yake dhidi ya ardhi ngumu.

Mabingwa watetezi Uhispania

Mabingwa watetezi wa kombe hili la Ulaya , Uhispania wanaanza kampeni yao kutetea taji hili la Euro 2016 dhidi ya Jamhuri ya Cheki leo jioni , wakiwania kunyakua taji la tatu mfululizo la Ulaya mjini Toulouse katika kundi D, mchezo utakaonza saa tisa jioni kwa saa za Ulaya ya kati .

Roy Hodgson kocha wa UingerezaPicha: picture-alliance/offside/M. Atkins

Na katika kundi linalotajwa kuwa la kifo la E pambano la mwanzo litakuwa kati ya Ireland ikitoana jasho la Sweden saa 12 jioni kwa saa za Ulaya ya kati sawa na saa moja jioni kwa saa za Afrika mashariki katika uwanja wa Stade de France , kabla ya Ubelgiji kutiana kifuani na Italia mjini Lyon saa tatu usiku sawa na saa 4 usiku kwa saa za Afrika mashariki.

Kocha wa Uingereza Roy Hodgson amemwita Gareth Bale kuwa mtu asiye na heshima , baada ya nyota huyo wa Wales kusema nchi yake imefanya vizuri na kuonesha uwezo na fahari kuliko majirani zao wa England katika fainali hizi za Euro 2016.

Ulinzi umeongezwa katika viwanja vya mpira katika Euro 2016Picha: picture-alliance/Maxppp/E. Bride/La voix du nord

England na Wales zinakabiliana mjini Lens siku ya Alhamis , wakati timu ya Bale iko mbele katika kundi B baada ya kuilaza Slovakia kwa mabao 2-1 katika mchezo wao wa ufunguzi na kikosi cha Hodgson kiliambulia sare tu ya bao 1-1 dhidi ya Urusi.

Ghasia Euro 2016

Ghasia mwishoni mwa pambano la England na Urusi zimesababisha wasi wasi juu ya mashabiki wa Urusi kufanya vufo tena, wakati shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA likiimarisha ulinzi katika viwanja.

UEFA inataka kuepuka kurejea kwa ghasia ambazo zilichafua mwisho wa pambano kati ya Urusi na England na ulinzi mkali utawekwa kudhibiti mashabiki katika mchezo wa Jumatano wa kundi B kati ya Urusi na Slovakia.

Mashabiki wa Urusi walionekana kushambulia sehemu ya mashabiki wa England katika uwanja baada ya sare ya bao 1-1 mjini Marseille siku ya Jumamosi, na kuwalazimisha kukimbia.

Nalo shirikisho la kandanda la Uingereza FA limewataka mashabiki wa nchi hiyo kuwajibika na kuwa na adabu , kufuatia kitisho cha shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA kuiondoa England kutoka Euro 2016 iwapo ghasia zitarejea tena kwa mashabiki wa Ufaransa.

Wahuni wa Urusi wakiwa tayari kupambanaPicha: picture-alliance/Maxppp/E. Bride/La voix du nord

Nayo magazeti ya Uingereza , yamesisitiza kwa kuandika "Muwe na tabia nzuri , ama sivyo tutaondolewa katika mashindano," limeandika gazeti la Daily Mirror.

The Daily Star limeandikwa kifupi tu, "Kuweni na adamu", lakini gazeti limewashutumu mashabiki wa Urusi kwa kuanzisha ghasia.

Shabiki mmoja wa Ireland ya kaskazini amefariki katika mji wa Nice baada ya kupanda katika bomba la uzio wa ufukwe wa bahari na kuanguka katika eneo lenye mawe, amesema afisa wa eneo hilo leo.

Ni shabiki wa kwanza kufariki katika mashindano haya ya Euro 2016 ambayo yamekumbwa na machafuko na ghasia nje ya uwanja baina ya mashabiki tangu mashindano hayo yafunguliwe Ijumaa iliyopita.

Copa America

Na katika mashindano ya kombe la mataifa ya America kumezuka utata jana Ijumaa baada ya baada ya refa kufanya makosa na kuirejesha nyumbani Brazil baada ya kufungwa bao 1-0 na Peru.

Kipigo hicho kimeiacha Brazil ikihangaika kutafakari ushiriki wake mbovu kabisa katika Copa America tangu mwaka 1987, mara ya mwisho mabingwa hao mara tano wa dunia kushindwa kutoka katika awamu ya makundi.

Brazil ikihitaji sare tu kuweza kufuzu kuingia katika robo fainali kama washindi katika kundi B, ilionekana kutimiza azma hiyo kuingia katika timu nane za robo fainali ikiwa zimebakia dakika 15 mpira kumalizika dhidi ya Peru.

Lakini mashambulizi kadhaa katika eneo la Brazil kutoka Peru yaliishia kwa Raul Ruidiaz kuuweka mpira wavuni baada ya kupata krosi kutoka kwa Andy Polo , akionekana kutumia mkono wake.

Wachezaji wa Brazil wakimzingira mwamuzi baada ya bao lililoonekana kuwa la mkono.Picha: Reuters/Winslow Townson-USA TODAY Sports

Wachezaji wa Brazil walilalamika kwa nguvu sana, wakimvamia refa Curha, ambae alionekana akitazama huku na huku kuamua iwapo bao hilo ni halali. Na baada ya muda refa aliamua kuwa bao hilo ni halali.

Mexico na Venezuela zimefanikiwa kuingia katika robo fainali ya Copa America.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / afpe / rtre / dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga