Ujerumani na Uholanzi kuumana tena katika Euro 2020
3 Desemba 2018Ujerumani na Uholanzi hazitaki kuachana. walicheza pamoja katika ligi ya mataifa ya ulaya, na sasa tena tutapata michezo miwili mikubwa katika kundi C.
Kwa upande wa kandanda la kimataifa, mabingwa wa zamani wa kombe la Ulaya Ujerumani watapambana na Uholanzi tena katika kinyang'anyiro cha kuwania kufuzu kwa ajili ya fainali za Euro 2020 baada ya kuwekwa pamoja katika upangaji wa makundi mjini Dublin, lakini Uingereza iliyofikia nusu fainali ya kombe la dunia mwaka huu haina sababu ya kulalamika juu ya hilo.
Ujerumani ilikuwa timu hatari zaidi katika chungu namba mbili baad ya kushuka kutoka katika kundi la timu za juu la ligi ya mataifa, kwa sehemu fulani kutokana na kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Uholanzi mwezi Oktoba.
Ujerumani itaanza kampeni yake kwa kusafiri kwenda Uholanzi Machi 24 mwakani kabla ya kuwa wenyeji wa majirani zao hao Septemba 6. Huyu hapa kocha wa uholanzi Ronald Koeman.
"Ni ngumu, inafurahisha kuwa na Ujerumani katika kundi moja. Timu ngumu kabisa katika chungu cha pili lakini sawa tu tulicheza dhidi yao wakati huo na tunawajua na wanatujua na nafikiri mengine katika kundi hili yankubalika na naangalia matokeo ya kupangwa katika kundi hili kwa matumaini makubwa."
Kundi C
Ireland ya kaskazini, Estonia na Belarus ni timu nyingine zenye jukumu la kuleta mshangao katika kundi la C. Hata hivyo timu mbili za juu katika kila kundi katika makundi haya 10 zitaingia moja kwa moja katika kinyang'anyiro cha fainali zitakazokuwa na timu 24, ambazo zitachezwa kwa mara ya kwanza katika nchi 12 wenyeji, hakuna shaka kwamba mataifa makubwa vigogo wa soka la Ulaya yatakuwapo katika fainali hizo.
kundi hili ni gumu," amesema kocha wa Ujerumani Joachim Loew, ambaye yuko chini ya mbinyo akitakiwa kuirejesha timu yake katika nafasi yake baada ya kuanguka katika awamu ya makundi katika kombe la dunia.
Hakuna sababu ya kikosi cha kocha Gareth Southgate kuhofia katika kundi A kwa kuwa inaanza na mchezo wa nyumbani dhidi ya Jamhuri ya Cheki Machi 22, ambapo pia England inakumbana na Bulgaria , Montenegro na Kosovo. Kocha gareth Southgate:
"Kwa hakika kuna nchi ambazo tungepangwa nazo ambazo tumeepuka kama Ujerumani katika chungu cha pili na serbia pamoja na nyingine kadhaa katika chungu namba 3, lakini tunashauku kubwa kufikia fainali hizi na moja kati ya miji wenyeji. Sisi ni moja ya miji wenyeji, kwa hiyo tunahitaji kuwa na uhakika wa kufikia huko."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae / rtre / ape
Mhariri: Mohammed Khelef