Ujerumani: Tunaendelea kutoa misaada ya afya duniani
28 Aprili 2026
Pembezoni mwa kongamano hilo la kilele ambalo ni la pili kufanyika barani Afrika, alisisitiza kuwa nchi yake kamwe haitajiondoa kwenye jukwaa la kimataifa mintarafu sekta ya afya na kwamba linalotiliwa mkazo ni ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya pande zote.
"Hatutajiondoa kwenye mifumo ya afya ya ulimwengu. Tuna azma ya kuimarisha ushirikiano wa Kenya na Ujerumani kwenye uchumi katika sekta ya afya: Alisema.
Aliongeza kuwa tayari yanashuhudiwa matokeo mazuri ya ushirikiano wa kampuni ya Ujerumani ya dawa ya Merck kwa hiyo tumeshuhudia hatua muhimu na tungependa kuimarisha hayo katika siku za usoni.
Mkutano huo unafanyika wakati ambapo jamii ya kimataifa inajipanga upya baada ya Marekani kubadili sera zake za kufadhili miradi ya maendeleo ya kigeni hali iliyochangia bajeti za mashirika muhimu kupunguzwa.
Kenya yachaguliwa kuwa mfano
Kenya imeteuliwa kuwa taifa la majaribio ya mbinu za ushirikiano wa kiuchumi na uwezo wa kufanya kazi pamoja na sekta ya binafsi.
Moja ya matunda ya mikakati hiyo ni kampuni ya kutengeza dawa ya Universal Cooperation iliyoko Kikuyu, kaunti ya Kiambu iliyo na uwezo wa kuzalisha aina zaidi ya 100 za dawa zinazotimiza vigezo vya shirika la afya duniani, WHO.
Dawa hizo zinasambazwa na kutumika katika zaidi ya mataifa 20. Kampuni ya Ujerumani ya dawa ya Merck inashirikiana na Universal Cooperation ya Kenya kutengeza dawa za watoto za kupambana na minyoo.
Washirika wengine ni pamoja na wakfu wa Konrad Adenauer, kampuni ya Siemens,na shirika la maendeleo la kimataifa la Ujerumani, GIZ.Kwenye ufunguzi rasmi wa mkutano huo wa kilele mwanzoni mwa wiki hii,Rais William Ruto alisisitiza kuwa upo umuhimu wa kuwekeza kwenye sekta ya afya kwa ushirikiano na wadau wa kimataifa.
"Hatima ya sera za afya, ubunifu na utoaji huduma hauwezi kupiga hatua bila ya mchango wa Afrika kuwa kwenye majadiliano, utendaji na utekelezaji. Afrika leo iko katika njia panda. Tunabeba mzigo mzito zaidi wa magonjwa ila tunachangia chini ya asilimia tatu ya gharama za mahitaji ya sekta ya afya duniani.”
Kauli mbiu ya kongamano hilo la afya ni kutokea majanga hadi uimara: ubunifu kwa afya na inajikita katika kusaka mbinu bora zaidi za kupambana na migogoro ya kiafya kwa kuzingatia ubunifu na teknolojia ya kisasa.
Zaidi ya wajumbe alfu 2 wanahudhuria mkutano huo muhimu unaowaleta pamoja viongozi,watafiti, watunga sera na washirika wa maendeleo kufanya kazi pamoja ili kuunda mifumo ya afya inayoweza kuhimili dhoruba za majanga. Mkutano huo unahitimishwa kesho Jumatano.