1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Ufaransa kuwatimua wanadiplomasia wa Urusi

Daniel Gakuba
5 Aprili 2022

Hasira na lawama kutoka nchi za magharibi zimeendelea kuiandama Urusi kuhusiana na mauaji ya watu wengi ambao nchi hizo zinavishutumu vikosi vya Urusi kuyafanya katika mji wa Ukraine wa Bucha.

Ukraine | Leichen auf der Straße in Bucha
Mauaji mbayo wanajeshi wa Urusi wanatuhumiwa kuyafanya mjini Bucha yamezusha hasira kubwa katika nchi za magharibiPicha: REUTERS

Mataifa kadhaa yamesema yatawafukuza wanadiplomasia wa Urusi kutokana na mauaji hayo. Ujerumani pekee imesema itawafukuza wanadiplomasia wa Urusi wapatao 40, Ufaransa itawarudisha nyumbani wapatao 35, na Lithuania imesema itawatimua wanadiplomasia wa Urusi ambao bado haijataja idadi yao. Urusi imesema itazijibu nchi hizo kwa hatua sawa na hizo.

Katika hatua nyingine inayozidisha utengano baina ya Urusi na nchi za magharibi, hapo jana rais wa Urusi Vladimir Putin alitia saini amri inayofuta urahisishaji wa viza za nchi yake kwa maafisa na waandishi wa nchi za Ulaya alizoziita mahasimu.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia amesema taarifa za mauaji ya Bucha ni za kutunga ili kuichafulia jina UrusiPicha: picture alliance / NurPhoto

Ukraine yasema Urusi inajipanga kwa mashambulizi makubwa zaidi

Wakati huo huo Ukraine imesema katika taarifa kuwa Urusi inajipanga kufanya mashambulizi mapya mashariki mwa Ukraine, ikilenga kuuteka mji wa Kharkiv na kuzizingira ngome za jeshi Ukraine kwenye mstari wa mbele upande huo wa mashariki.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Ukraine Oleksandr Motuzyanyk amesema Urusi inaishambulia miji ya Rubizhne na Popasna katika jimbo la Luhansk, ikiazimia kuukamata mji mkuu wa jimbo hilo, Severodonetsk.

Msemaji huyo amesema pia kuwa Urusi inawarundika wanajeshi karibu na mji wa Mariupol uliozingirwa kwa wiki kadhaa. Hata hivyo hakuonyesha ushahidi wowote kuthibitisha madai yake, na shirika la reuters lililomnukuu halikuweza kuthibitisha taarifa hizo.

Rais wa Ukraine, Volodymir Zelenskiy ameutembelea mji wa Bucha kutathmini uhalifu uliofanyika hukoPicha: Ronaldo Schemidt/AFP/Getty Images

Akijibu hasira za nchi za magharibi dhidi ya nchi yake kuhusu mauaji wa mjini Bucha, waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema viongozi wa nchi hizo wanaomuandama rais Putin, wangepaswa kwanza kujitathmini wenyewe na dhamira yao, hususan kuhusiana na matendo yao katika nchi kama Irak na Libya.

Urusi kwa viongozi wa magharibi: Jitathmini kabla ya kuilaumu Urusi

Amerudia msimamo wa Moscow kuwa taarifa zinazoenezwa juu ya mauaji hayo ni za uongo, na kwamba zinaazimia kuipaka matope Urusi na viongozi wake.

Hali ya kibinadamu katika mji uliozingirwa wa Mariupol inaelezewa kuwa mbaya sanaPicha: picture alliance/dpa/AP

Kwenye uwanja wa diplomasia, mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi tano za kiarabu wanaambatana na katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu katika ziara itakayowafikisha katika mataifa yanayohusika na vita vya Ukraine.

Mawaziri hao kutoka Misri, Algeria, Irak, Jordan na Sudan walikutana jana na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov mjini Moscow, na baadaye watakwenda Poland ambako watafanya mazungumzo na mawaziri wenzao wa mambo ya nje wa Poland na Ukraine.

Na juhudi za kuwaondoa raia katika miji yenye mapigano mashariki mwa Ukraine zimeendelea kutatizika. Naibu waziri mkuu wa Ukraina Iryna Vereshchuk amesema kuwa msafara wa magari uliosindikizwa na shirika la kimataifa la msalaba mwekundu ulikuwa ukizuiliwa katika mji wa Manhush. Msemaji wa shirika hilo pia alithibitisha kuwa magari yao yaliyokuwa yakielekea katika mji uliozingirwa wa Mariupol yalikuwa yamesimamishwa.

-ape, rtre

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW