1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Ufaransa na Poland zaazimia kuepusha vita Ulaya

Daniel Gakuba
9 Februari 2022

Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Poland waliahidi kushirikiana katika juhudi za kuuzuia mzozo wa Ukraine kusababisha vita barani Ulaya. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema diplomasia imeleta matumaini mapya.

Berlin Weimar Triangle Duda Scholz und Macron
(Kuanzia kushoto) Rais wa Poland Andrzej Duda, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: HANNIBAL HANSCHKE/REUTERS

Wakisimama pamoja baada ya mazungumzo hayo mjini Berlin, kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na rais wa Poland Andrzej Duda, kwa sauti moja walielezea mshikamano wao katika kudumisha uhuru wa Ukraine.

Soma zaidi: Macron aendeleza juhudi kuzima mzozo Ukraine

Viongozi hao wamekutana mnamo wakati shughuli za kidiplomasia zikishika kasi kubwa, katika kujaribu kuzuia mapigano kati ya Ukraine na Urusi ambayo imerundika wanajeshi zaidi ya 100,000 kwenye mpaka wa Ukraine.

Rais wa Urusi Vladimir Putin, amemuahidi Macron kuwa hatakuwa wa kwanza kuupanua mzozoPicha: Thibault Camus, Pool/AP/picture alliance

Lengo ni kuzuia vita barani Ulaya

Kansela Scholz aliyeupokea mkutano wa viongozi wa nchi hizo tatu ujulikanao kama Pembetatu ya Weimar, alisema kuwepo kwa wanajeshi wengi wa Urusi na zana nzito za kivita kwenye mpaka wa Ukraine ni hali ya kutia wasiwasi mkubwa.

''Lengo letu la pamoja ni kuzuia vita barani Ulaya. Sambamba na mtazamo huo, hatua nyingine ya Urusi kuukiuka uhuru wa kieneo wa Ukraine haukubaliki,'' amesema Scholz na kuongeza kuwa ''ikitokea itakuwa na athari mbaya sana kwa Urusi, kisiasa, kiuchumi na bila shaka kimkakati.''

Soma zaidi:Magharibi wahaha kusaka suluhu ya mzozo wa Ukraine 

Kabla ya mkutano huu wa Berlin, Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani alikutana na rais wa Marekani Joe Biden mjini Washington, mada kuu ikiwa mzozo huo wa Ukraine, na wakati huo huo rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa katika mbio za kidiplomasia, kwanza akianzia mjini Moscow alipofanya mazungumzo marefu na rais Vladimir Putin, na kisha nchini Ukraine kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Volodymyr Zelenskiy.

Rais Volodymyr Zelenskiy (kushoto) alipokea kwa mashaka ahadi ya Putin ya kutoupanua mzozo zaidiPicha: Reuters/P. Wojazer

Diplomasia yafungua milango mipya ya matumaini

Katika mkutano wa jana, rais Macron alisema juhudi kubwa zinazoendeshwa na pande mbali mbali zinaleta matumaini.

''Kwa upande mwingine kuna kazi kubwa inayofanywa na NATO, Marekani na sisi washirika wa Ulaya, kujenga vigezo hivi vya kuhakikisha usalama,'' alisema Macron, akiongeza kuwa siku chache zilizopita zimefungua mlango kwa fursa mpya.''

Soma zaidi: Kansela wa Ujerumani Scholz kukutana na Biden Washington

Alipokuwa nchini Ukraine, Rais Emmanuel Macron alisema alipata ahadi kutoka kwa Rais Putin wa Urusi, kuwa hatachukua hatua ya kwanza kuupanua mzozo. Ni hakikisho ambalo rais wa Ukraine Zelenskiy alilipokea kwa mashaka, akisema uzeofu wa kisiasa unataka ahadi kama hizo za maneno zithibitishwe kwa vitendo.

Baada ya mkutano huu Ujerumani, Ufaransa na Poland, inatarajiwa kuwa mwingine utafanyika kesho Alhamis huko huko Berlin chini ya kile kijulikanacho kama Mpango wa Normandy, ukihusisha wajumbe kutoka Ujerumani, Ufaransa, Urusi na Ukraine.

Vyanzo: rtre, afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW