1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Gaza basi, zasema Ujerumani, Ufaransa na Uingereza

12 Agosti 2024

Viongozi wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wametoa wito wa pamoja wa kusitishwa mapigano huko Gaza, kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas na kuruhusu ufikishaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza bila vikwazo.

Eneo la Jebaliya | Mwanamke na msichanakatikati ya sehemu iliyoharibiwa na vita
Mama na mwanawe katika eneo la Jebaliya, kaskazini mwa GazaPicha: Enas Rami/AP/picture alliance

Viongozi hao wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza wamesema leo kwenye tamko lao la pamoja kwamba haiwezekani tena kuyachelewesha zaidi mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza kati ya jeshi la Israel na wanamgambo ya Hamas na wakati huo huo wameionya Iran na washirika wake dhidi ya kuongeza kuuchochea mzozo huo.

Soma Pia: Blinken aitaka Mashariki ya Kati kujizuia kuongeza mzozo  

Tamko hilo la pamoja limetolewa baada ya taarifa ya Israel kufanya shambulio baya zaidi katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa kwa zaidi ya miezi 10 sasa tangu vilipoanza vita.
Takriban watu 93 waliuawa kwenye mashambulizi ya jeshi la anga la Israel, Kaskazini mwa Gaza siku ya Ijumaa wiki iliyopita katika shule iliyokuwa inatumiwa kuwahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao, kulingana na waokoaji ambao pia ni walinzi wa raia. 

Eneo la Jabaliya kaskazini mwa Gaza lililoshambuliwaPicha: Abdul Rahman Salama/Xinhua/IMAGO

Viongozi watatu wa Ulaya

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer wamesema mapigano ni lazima yamalizike sasa na mateka wote ambao bado wanazuiliwa na Hamas pia ni lazima waachiliwe.
Viongozi hao wamesisitiza kwamba watu wa Gaza wanahitaji misaada haraka bila vikwazo vyovyote.

Soma Pia: Umoja wa Ulaya waunga mkono juhudi za kusitisha vita Gaza 

Pia wamesifu kazi kubwa inayofanywa na wapatanishi wa Misri, Qatar na Marekani kuelekea kupatikana makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka.
Katika tamko lao, viongozi hao watatu wa Ulaya pia wameitaka Iran na washirika wake kujiepusha na mashambulizi ambayo yatazidisha mivutano ya kikanda na kuhatarisha fursa ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka.
Scholz, Macron na Starmer wamesema hakuna taifa litakalofaidika kutokana na kuongezeka mivutano katika Mashariki ya Kati.
Duru kadhaa za mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza hazijafaulu hadi sasa, isipokuwa makubaliano ya wiki moja yaliyofikiwa mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka jana.

Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Wapaatanishi wanasemaje?

Wapatanishi wa kimataifa wamezialika Israel na kundi la Hamas kuanza tena mazungumzo yaliyokwama kwa muda mrefu wakati ambapo mapigano huko Gaza na mauaji ya viongozi wa wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran yamesababisha kuongezeka kwa hali ya wasiwasi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Hamas inawataka wapatanishi hao kutekeleza mpango wa mapatano uliowasilishwa na Rais wa Marekani Joe Biden badala ya kufanya mazungumzo zaidi, huku Wapalestina wakizidi kukimbia huku na kule kuepuka operesheni mpya ya jeshi la Israel.
Vita vya Gaza vilianza baada ya kundi la Hamas kufanya mashambulio mnamo Oktoba, 7 kusini mwa Israeli. Watu wapatao 1,198 waliuawa, wengi wao walikuwa raia, kulingana na hesabu za shirika la AFP na takwimu rasmi za Israel.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Jose Luis Magana/AP Photo/picture alliance

Soma Pia: Baraza la Usalama la UN laijadili hali ya Mashariki ya Kati  

Wanamgambo wa Hamas pia waliwachukua mateka watu 251, na watu 111 kati ya hao bado wanazuiliwa huko Gaza, wakiwemo watu 39 ambao jeshi limesema wamekufa.
Mashambulizi ya kijeshi ya Israel ya kulipiza kisasi huko Gaza yamesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 39 kwa mujibu wa wizara ya afya Gaza.

Vyanzo: AFP/AP
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW