1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Uingereza na Italia zathibitisha visa vya Omicron

Sylvia Mwehozi
28 Novemba 2021

Uingereza, Ujerumani na Italia zimeripoti visa vya kirusi kipya cha Omicron huku Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson akitangaza hatua mpya za kukabiliana na kirusi hicho.

Neue COVID-19-Variante Omicron
Picha: Pavlo Gonchar/Zumapress/picture alliance

Kugunduliwa kwa aina hiyo mpya ya kirusi cha Omicron, kumesababisha wasiwasi duniani kote, kuchochea wimbi la marufuku ya safari au vizuizi vya kukikabili, wakati masoko ya fedha yakiyumba siku ya Ijumaa, mnamo wakati wawekezaji wakihofu kwamba kirusi cha Omicron kinaweza kuathiri uchumi ambao ulianza kuimarika.

Waziri wa afya wa Uingereza Sajid Javid amesema visa viwili vya Omicron vilivyogundulika Uingereza vinahusishwa na safari za kutoka Kusini mwa Afrika. Waziri Mkuu Johnson ametangaza hatua za kukikabili kirusi cha Omicron, lakini hatua hizo hazikuzuia shughuli za kijamii zaidi ya watu kutakiwa kuvaa barakoa katika baadhi ya maeneo.

"Tutahitaji kila mmoja anayeingia Uingereza kufanya kipimo cha PCR kufikia mwishoni mwa siku ya pili baada ya kuwasili na kujitenga hadi pale matokeo yatakapotoka", alisema waziri Mkuu Johnson.

Wizara ya afya katika jimbo la Bavaria la Ujerumani, nayo pia imetangaza kuthibitisha visa viwili vya Omicron. Watu wawili waliingia katika uwanja wa ndege wa Munich Novemba 24, kabla ya Ujerumani kuitaja Afrika Kusini kuwa sehemu hatarishi ya kirusi hicho.

Wasafiri wakiwa katika msururu katika uwanja wa ndege wa OR TamboPicha: Jerome Delay/AP/picture alliance

Nchini Italia, wizara ya afya nayo imerekodi kisa cha kwanza mjini Milan kwa mtu mmoja aliyetokea Msumbiji. Jamhuri ya Czech nayo imesema inafuatilia kisa kinachoshukiwa kuwa cha Omicron kwa mtu mmoja aliyetoka Namibia.

Aina hiyo mpya ya kirusi cha Omicron iliyotajwa kuwa yenye kutia wasiwasi na shirika la afya ulimwenguni WHO, inaelezwa kuenea zaidi kuliko virusi vya awali vya ugonjwa huo, ingawa wataalamu hawajajua bado ikiwa kitasababisha athari zaidi za Covid-19 ukilinganisha na aina nyingine.Shirika la ndege la Qatar lawapiga marufuku abiria kutoka Afrika Kusini

Mamlaka za Uholanzi zimesema kuwa watu 61 kati ya 600 waliowasili Amsterdam na ndege mbili za kutoka Afrika Kusini siku ya Ijumaa, walikuwa na maambukizi ya corona. Mamlaka ya afya nchini humo inafanya vipimo zaidi kubaini ikiwa miongoni mwa walioambukizwa kimo kirusi kipya.

Abiria mmoja Paula Zimmerman aliyewasili siku ya Ijumaa kutoka Afrika Kusini hakupatikana na maambukizi lakini amekuwa na wasiwasi tangu wakati huo.

Masoko ya fedha yaliporomoka siku ya Ijumaa hususan hisa za mashirika ya ndege na hisa nyinginezo katika sekta ya usafiri. Bei za mafuta nazo zimeshuka kwa karibu dola 10 kwa kila pipa.