1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Uingereza kuendelea kuisaidia Ukraine

Angela Mdungu
24 Aprili 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak, wameahidi kuisaidia Ukraine kwa kadri itakavyohitajika. Wametoa ahadi hiyo wakati wa ziara ya Sunak mjini Berlin.

Mkutano wa Kansela Olaf Scholz, Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na waandishi wa habari mjini Berlin
Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak na Kansela Olaf Scholz wa UjerumaniPicha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Licha ya ahadi ya wawili hao Kansela Scholz ameendelea kushikilia msimamo wake wa kukataa kuipatia Kyivv makombora ya masafa marefu aina ya Taurus. Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak  aliyewasili Berlin baada ya ziara aliyoifanya Poland Jumanne, ameahidi msaada zaidi wa kifedha kwa Kyiv.

Soma zaidi: Sunak: Uingereza itasimama kidete na Ukraine

Sunak amewaambia waandishi wa habari kuwa yeye na Kansela Scholz wanaungana pamoja katika kuisaidia Ukraine na kwamba uchokozi wa Rais Vladmir Putin wa Urusi unapaswa kufikia kikomo. Kwa upande wake Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz naye ametilia mkazo hatua ya mataifa hayo mawili kuisaidia Ukraine.

Scholz asisitiza hatoipatia Ukraine makombora ya Taurus

Licha ya kuiunga mkono kijeshi Ukraine, Scholz ameutetea uamuzi wake wa kukataa kuipa Ukraine makombora ya masafa marefu aina ya Taurus akisema , hakuna nchi iliyoipatia Ukraine mifumo mingi ya silaha kama Ujerumani lakini kamwe, haitatoa makombora hayo na msimamo wake hautobadilika.

Kombora la masafa marefu aina ya TaurusPicha: Leonhard Simon/Getty Images

Sunak amesema kuwa nchi yake inajiweka katika hali ya utayari kwa vita kwa kuongeza bajeti yake ya ulinzi kwa asilimia 2.5 ya pato la taifa kufikia mwisho wa mwaka 2030. Alitoa kauli hiyo akisema kuwa mataifa ya magharibi yanakabiliwa na moja ya nyakati ngumu zaidi tangu vita baridi vilipokwisha.

Soma zaidi: Zelenskiy aishukuru Ujerumani, Ufaransa na Uingereza

Aliahidi pia kupeleka silaha zenye thamani ya pauni milioni 500 nchini Ukraine. Awali Sunak aliwatembelea wanajeshi wa Uingereza na Ujerumani katika kambi ya jeshi mjini Berlin kabla ya kukutana na Kansela Scholz. Nchi hizo mbili mbali na ushirikiano katika masuala ya usalama zimejadili pia kushirikiana katika masuala ya nishati na mapambano dhidi ya uhalifu wa kupangwa.

Katika hatua nyingine mataifa hayo mawili yametangaza mpango wa kutengeneza mifumo ya kisasa ya mizinga ya ufyetuaji makombora  aina ya Howitzer inayoweza kuendeshwa kutoka mbali  kwa ajili ya operesheni za kijeshi za hapo baadaye.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW