1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kodi za nyumba zazidi kupaa Ujerumani

3 Agosti 2023

Watu zaidi na zaidi wanahangaika kutafuta nyumba nchini Ujerumani. Upatikanaji ni mdogo sana, kodi zinapanda na mapato hayatoshi tena. Ni hali ya kutisha

Deutschland Demonstration gegen hohe Mieten in Berlin
Picha: Christophe Gateau/dpa/picture alliance

Kwa jadi Ujerumani ni taifa la wapangaji. Wakati kote Ulaya karibu asilimia 70 ya watu wanamiliki nyumba au ghorofa wanamoishi, ni asilimia 46 tu ya watu wanaoishi Ujerumani wanafanya hivyo. Katika miji mikubwa, uwiano huo ni wa chini zaidi.

Ikiwa unataka kukodisha nyumba nzuri katika eneo zuri mjini Berlin, unahitaji pesa nyingi. "Ghorofa kubwa la vyumba vinne" katika wilaya ya wenye uwezo ya Charlottenburg ya mjini Berlin: mita za mraba 182, yenye samani, kodi ni €8,190 ($8,947) kwa mwezi. Pamoja na kuongeza joto, umeme na gharama nyinginezo zisizotarajiwa, ambazo ni zaidi ya €50 kwa kila mita ya mraba.

Soma pia: Ujerumani yapambana kuwahifadhi wakimbizi

Kile kinachojulikana kama kikomo cha bei ya ukodishaji kilijumuishwa katika kanuni ya kiraia ya Ujerumani mnamo Juni 2015. Kulingana na hili, wakati wa kusaini mkataba mpya wa ukodishaji, kodi haiwezi kuzidi asilimia 10 ya kodi ya ulinganifu wa ndani.

Kupata nyumba mpya ni rahisi kwa familia zilizo na mapato mazuri, zenye nguvu ya kupanda ngazi, na zinazoweza kurekebisha nyumba zao mpya.Picha: Rainer Hackenberg/picture-alliance

Lakini huko Berlin na miji mingine mikubwa, wamiliki wa nyumba wamepata njia nono ya kukwepa hili: Ukomo hautumiki kwa nyumba zenye samani na mikataba y aukodishaji wa muda mfupi. Kwa hivyo sasa, zaidi ya nusu ya nyumba zote mjini Berlin zinakodishwa kama "zenye samani."

Kiwango cha kukodisha cha euro 6.50 hadi euro 7.50 kwa kila mita ya mraba kinachukuliwa kuwa kinakubalika kijamii nchini Ujerumani. Lakini kwa bei hiyo, huwezi hata kupata ghorofa nje kidogo ya Berlin siku hizi.

Jukwaa la mtandaoni linaorodhesha ghorofa katika kitongoji cha mashariki mwa Berlin - kwenye ghorofa ya sita isiyo na lifti kwa bei hiyo. Kwa kuzingatia hitaji la ukarabati, wapangaji wanapaswa kuwa "wenye kipaji katika kazi za mikono," tangazo linasomeka.

Nchini Ujerumani, wastani wa mapato halisi - kiwango kinachosalia baada ya makato ya kodi na malipo hifadhi ya jamii -- hivi kinasimama kwenye euro 2,165, kulingana na ofisi ya takwimu ya shirikisho. Karibu theluthi moja ya mapato haya inatumika kwenye kodi ya nyumba. Lakini hata hiyo haitoshi.

Malazi ya bei nafuu yanaweza kupatikana nje kidogo ya Berlin.Picha: Volker Witting/DW

Mjini Munich, mita ya mraba sasa inagharimu €19 katika kukodi, mjini Stuttgart €18, mjini Dusseldorf na Cologne €12 hadi €13 na Berlin €11. "Mahitaji makubwa ya nyumba za bei nafuu yanakutana na ongezeko la kihistoria la kodi na upatikanaji ambao hautoshi kwa kiasi kikubwa," tathmini ya hivi karibuni kwenye tovuti ya mtandao ya Immoscout24 inasomeka.

Bei za mali zisizohamishika zapanda tena

Bei ya mali isiyohamishika inaongezeka duniani kote. Katika utafiti, taasisi ya ifo na taasisi ya sera ya kiuchumi ya Uswisi iligundua kuwa ongezeko la wastani la bei la kila mwaka la asilimia 9 linaweza kutarajiwa katika miaka 10 ijayo.

Soma pia: Wapiga kura wa Berlin waunga mkono kutaifisha nyumba zinazomilikiwa na makampuni makubwa

Kwa Ujerumani, takwimu hiyo imewekwa kwa asilimia 7. Ikiwa viwango vinavyoongezeka vya riba ya mikopo vinazingatiwa, kununua nyumba au ghorofa inakuwa vigumu kwa Wajerumani wengi.

Chaguo pekee la bei nafuu ni nyumba za zamani ambazo zina mifumo ya zamani ya kupasha joto kwa kutumia mafuta, ambayo italazimika kubadilishwa kwa miaka michache ijayo.

Bila chaguo la kununua nyumba, kukodisha ndio mbadala pekee. Hii inazidisha uhaba kwenye soko la nyumba za kupanga na kusababisha kuongezeka kwa bei huko.

Mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi wa kampuni ya Amaryllis eG mjin Bonn.Picha: Karl-Heinz Hick/Joker/IMAGO

Kulingana na utafiti wa Taasisi ya Eduard Pestel ya Utafiti wa Mifumo, Ujerumani ina uhaba wa zaidi ya nyumba 700,000 - hasa katika kipengele cha makazi ya bei nafuu. Serikali ya Ujerumani ilikuwa imetangaza mipango ya kujenga nyumba mpya 400,000 kwa mwaka.

Kiuhalisi, zaidi ya nusu tu itafikiwa mwaka huu, na mnamo 2024 lengo litakosa kufikiwa kwa kiasi kikubwa zaidi. Hili lilikokotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Mzunguko wa Biashara inayohusishwa na chama cha wafanyakazi.

Vita vya Ukraine na mfumuko wa bei vimepaisha gharama za ujenzi. Kuna uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na vifaa vya ujenzi, na kazi zinasimamishwa katika maeneo mengi ya ujenzi.

Hakuna kilichosalia cha kukodisha

Watu zaidi na zaidi wanashindania nyumba chache za bei nafuu zilizobaki. Kati ya wakimbizi waliowasili nchini Ujerumani mwaka 2015/2016, karibu asilimia 25 bado wanaishi katika makazi ya wakimbizi ya serikali kwa sababu bado hawajaweza kupata mahali pao wenyewe. Mnamo 2022, zaidi ya wakimbizi milioni moja wa vita waliwasili Ujerumani kutoka Ukraine. Mwaka huu, karibu waomba hifadhi 300,000 wanatarajiwa kuja.

Lango la Brandenburg. Mji Mkuu wa Berlin umekuwa ghali zaidi kwa wapangaji.Picha: Schoening/picture alliance

Ujenzi wa nyumba kwa ruzuku ya serikali ni chaguo kwa wale katika jamii ambao hawawezi kumudu kodi kwenye soko huria la nyumba. Lakini serikali za Ujerumani zimepuuza "mpango wa makazi ya jamii" kwa miongo kadhaa.

Mwishoni mwa 2022, kulikuwa na nyumba za kijamii chini ya milioni 1.1 tu kote nchini - kiwango cha chini cha kihistoria. Chama cha Ujamaa cha mrengo wa kushoto -- die Linke -- kinapendekeza mpango wa makazi ya umma na mfuko maalum wa makazi ya bei nafuu.

Lakini serikali ya sasa inataka kupunguza ukopaji wa umma na kuzingatia kile kinachojulikana kama breki ya deni. Mnamo Mei, Waziri wa Ujenzi wa Shirikisho Klara Geywitz kutoka chama cha mrengo wa kushoto wa Social Democrat (SPD) aliongeza posho ya nyumba - ambayo ni ruzuku ya serikali kwa gharama za kodi - na kundi la wale walio na haki hiyo lilipanuliwa. Lakini hii inaonekana kama tone tu katika bahari.

Makazi ya kutosha ni haki ya binadamu, kinasema Chama cha Ustawi wa Wafanyakazi. Lakini mashirika yasiyo ya kiserikali yanaonya kuwa makazi yanazidi kuwa tatizo la uwepo kwa watu zaidi na zaidi, jambo ambalo linaweza kugeuka janga.

Wakosoaji wanaonya kuwa kuna haja ya kuwa na motisha ya kifedha kwa wawekezaji kuweka pesa zao katika ujenzi wa nyumba. Lakini mambo hayana uwezekano wa kuimarika kwa muda mfupi katika soko la nyumba la Ujerumani.