1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaadhimisha miaka 28 ya muungano

Oumilkheir Hamidou Scholz,Kay-Alexander
3 Oktoba 2018

Oktoba tatu mwaka 1990, Ujerumani, Mashariki na magharibi, iliungana upya baada ya kutenganishwa na ukuta. Lakini bado kuna Wajerumani ambao mpaka sasa hawajalitembelea eneo la pili.

Deutschland Berlin Tag der deutschen Einheit 1990
Picha: Imago/Gueffroy

Oktoba tatu mwaka 1990, Ujerumani, Mashariki na magharibi, iliungana upya baada ya kutenganishwa na ukuta, ikiwa ni matokeo ya kumalizika vita vikuu vya pili vya dunia. Scholz, Kay-Alexander anachambua miaka 28 ya muungano.

Katikati ya miaka ya 2000 maendeleo ya maana yalianza mashariki mwa Ujerumani. Ikafuata hali ambayo mpaka sasa ipo ya ukuaji wa kiuchumi. Ilidhihirika kana kwamba hali katika sehemu zote mbili za Ujerumani inaanza haraka kulingana. Lakini ukweli ni kwamba "ukuta uliosalia vichwani" hautoweki haraka hivyo.

Bado kuna Wajerumani ambao mpaka sasa hawajalitembelea eneo la pili. Na pia ule mtindo wa kuwaita wajerumani mashariki Ossi na wa magharibi Wessi mpaka leo bado upo. Mpaka kwenye mtandao wa kijamii Twitter mtindo huo unatumiwa sana kama Hashtags.

Mzozo wa wakimbizi na athari kwa uhusiano wa Wajerumani

Kansela Angela Merkel akiwasili katika kanisa la Cathedral mjini Berlin kuhudhuria maadhimisho ya siku ya muungano wa UjerumaniPicha: Reuters/F. Bensch

Tukitupia jicho yaliyotokea miaka ya nyuma, basi mzozo wa wakimbizi kati ya mwaka 2015 na 2016 umekujazidisha ufa katika uhusiano dhaifu miongoni mwa Wajerumani.

Katika mijadala ya kisiasa na kijamii hitilafu za maoni kati ya wakaazi wa mashariki na wenzao wa magharibi huzidi kubainika. Mikururo ya malaki ya wakimbizi ikasababisha wasiwasi katika maeneo ya mashariki ambako wakaazi wake wanahofia wasije wakapoteza tena hali ya utulivu, wakikumbuka yaliyowahi kuwafika zamani.

Hofu hizo hizo ndizo wanazozitumia hivi sasa viongozi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Vyama mfano wa "Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD, vuguvugu la Pegida vinaweka mstari wa mbele tofauti kati ya wajerumani. Tangu muda sasa chama cha AfD kinatajwa kukamata mstari wa mbele kati ya vyama vya kisiasa mashariki mwa ujerumani. Kinasemekana kuwa na nguvu kukipita chama cha jadi cha CDU, chama cha kansela wa muungano Helmut Kohl na kansela anaetokea mashariki mwa Ujerumani Angela Merkel.

Mijadala kuhusu siasa na hali za kijamii

Kutokana na hali hiyo haistaajabishi kwamba siku kuu ya taifa mwaka huu,"Siku ya Muungano, leo hii Oktoba tatu inazusha mjadala wa aina nyengine kuhusu mashariki na magharibi.

Katika miaka ya nyuma mijadala kuhusu mishahara sawa, utajiri na nguvu za kiuchumi ndio iliyokuwa mstari wa mbele badala ya hali za wananchi. Katika mada hiyo ya mwisho, hali za Wajerumani wa mashariki ni asilimia 73 tu ya hali ya wenzao wa magharibi.

Viongozi wakuu nchini Ujerumani akiwemo rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na mkewe pamoja na Kansela Angela Merkel wakihudhuria maombi katika kanisa la Dom Cathedral kwa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Muungano wa UjerumaniPicha: Getty Images/S. Gallup

Mijadala moto moto inaendelezwa na wanasiasa wa vyama tofauti akiwemo pia kansela."Muungano umeleta mageuzi makubwa" anasema kansela Merkel. Mengi yaliyotokea mapema miaka ya 90 yanazingatiwa tena na watu hivi sasa."Yalikuwa maarifa ya aina pekee" anasema kansela Merkel.

Kwa nini wakaazi wa mashariki wanahisi hawasikizwi vya kutosha?

Wengi walipoteza kazi zao na kulazimika kuanza upya. Mfumo wa afya, mfumo wa malipo ya uzeeni-kila kitu kilibadilika. Mageuzi hayo hata hivyo hayawezi kugeuka chanzo cha chuki na matumizi ya nguvu-anasisitiza kansela Merkel.

Matamshi kama haya ameyatoa pia mjumbe maalum wa serikali kuu anaeshughulikia masuala ya sehemu ya mashariki mwa ujerumani Christian Hirte aliyesema wakaazi wengi wa Ujerumani mashariki wanajisikia kana kwamba ni raia wa daraja la pili. Wanahisi hawasikilizwi vya kutosha.

Christian Hirte ameonya kwa kuzingatia jinsi AfD wanavyozidi kujipatia umaarufu katika sehemu ya mashariki" na kusema "hatuwezi kupuuza tunapoona watu wengi wakipoteza imani yao kwa taifa na vyama vya kisiasa.

Mwandishi:Scholz,Kay-Alexander/Hamidou Oumilkheir

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW