Ujerumani yaadhimisha miaka 65 ya Katiba
23 Mei 2014Rais wa Bundestag, Norbert Lammert (CDU) amesema kwenye sherehe iliyofanyika kwenye jengo la bunge hilo kwamba Katiba hiyo ni ya wakati wa furaha katika historia ya Ujerumani.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Bunge, serikali kuu ya shirikisho na Mahakama ya Katiba walikusanyika kuadhimisha siku ya tarehe 23 Mei 1949 ilipoanzishwa Sheria Msingi, neno linalotumika kumaanisha Katiba ya Shirikisho la Ujerumani.
Spika wa Baraza la Wawakilishi ambaye ni waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony, Stephan Weil, wa chama cha Social Democratic, amesema miaka hiyo 65 ni awamu ya ufanisi usiokuwa na mfano katika historia ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, kwani kutokana na Sheria hiyo, haki za kimsingi zimezidi kupata nguvu na mfumo wa shirikisho kuimarika.
Navid Kermani, aliyetoa hotuba ya kuadhimisha miaka 65 ya Sheria Msingi ya Ujerumani ni mwandishi vitabu na mtaalamu wa masuala ya Mashariki kutoka jiji la Cologne. Profesa huyo anayesomesha Marekani anathaminiwa sana katika mjadala kuhusu kujumuishwa wageni katika maisha ya kila siku ya jamii humu nchini.
Mwandishi: Oummilkher Hamidou, dpa
Mhariri: Mohammed Khelef