1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaahidi kuendelea kuisaidia Kenya

Admin.WagnerD24 Februari 2020

Serikali ya Ujerumani imeahidi kufadhili miradi ya elimu, na kupiga jeki uzalishaji katika viwanda nchini Kenya ili kukabiliana na tatizo ya ajira ambalo linazidi kuongezeka nchini Kenya.

Kenia | Bundespräsident Steinmeier Staatsbesuch
Picha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Ufadhili huo ni wa kima cha shilingi bilioni 3.9. Hayo yameelezwa leo baada ya rais uhuru Kenyatta wa Kenya na mwezake wa Ujerumani Frank-Walter Steimeier kutia sahihi mikataba ya ushirikiano wa kibiashara na maendeleo baina ya mataifa hayo mawili jijini Nairobi, Kenya. 

Ziara ya rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier inajiri wakati China ikizidi kuacha alama kubwa sio tu nchini Kenya lakini barani Afrika hasa katika sekta ya miundo mbinu huku mataifa ya Ulaya yakitunisha misuli kujaribu  kuwekeza kwenye bara hilo.

Alipopanda kwenye jukwaa na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenya, Steinmeier aliafiki kuwa taifa lake lina mengi ya kujifunza ili kuweza kuwekeza katika maeneo ambayo ni ya msingi. Ujerumani ina uhusiano wa miaka mingi na Kenya, kwani nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilipojinyakulia uhuru wake mwaka 1963, taifa hilo lilikuwa la kwanza kuitambua serikali mpya ya mtu mweusi kwa kutuma risala za heri.

Rais Steinmeier amefuatana na ujumbe wa wafanyibiashara kutoka Ujerumani wanaolenga kuwekeza katika sekta mbali mbali ya uchumi wa nchi ya Kenya.

Rais Frank-Walter Steinmeier akiwa na ujumbe alioongozana nao nchini KenyaPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Kwenye mkutano wao ulioandaliwa katika ikulu ya Nairobi, rais Kenyatta aliipongeza serikali ya Ujerumani kwa kujitolea kwake kufadhili miradi ya elimu nchini Kenya, kuanzia shule za msingi hadi kwenye taasisi za masomo ya juu  na kukiri kuwa hatua hiyo itasaidika pakubwa katika kuboresha uchumi na maisha ya wakenya.

Mazungumzo ya marais hao yamekamilishwa kwa hatua ya kutiwa saini mikataba ya ushirikiano. Hata hivyo Rais Uhuru Kenyattaalilazimika kumfahamisha mwenzake jinsi serikali yake inavyopambana na donda sugu la ufisadi, ambalo limeshindwa kutafutiwa tiba mjarabu, katika taifa ambalo limezongwa na kadhia nyingi. Serikali ya Ujerumani imekubali kushirikiana na Kenya katika sekta za uzalishaji na kilimo kwa kufadhili viwanda vya uzalishaji sawa na kuwaleta wataalam wa viwanda na biashara kusaidia wastawishaji nchini Kenya.

"Serikali ya Ujerumani, imekubali kusaidia mipango mipya nchini Kenya, kusaidia ajira kwa vijana. Vituo vitatu vya ubora vitaanzishwa, awamu ya kwanza itagharimu Euro milioni 26.4 na awamu ya pili itagharimu Euro Milioni 13.” alisema Uhuru.

Wanajeshi wa AMISOM ambao, Ujerumani imeahidi kuendelea kuwapatia ufadhiliPicha: AMISOM

Mbali na hayo Ujerumani imeihakikishia Kenya, kuwa itaendelea kukifadhili kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia  AMISOM  kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa, ili kupunguza visa vya ugaidi vinavyofanywa  na kundi la Al Shaabab.

Marais hao wawili  wanatarajiwa kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo siku ya Jumanne ikiwa ni pamoja na taasisi za mafunzo naa vyuo vya kiufundi hali kadhalika kujadili namna ya kuimarisha maisha ya raia wa mataifa hayo, kabla ya rais huyo wa Ujerumani kuzuru kambi ya wakimbizi ya Kakuma ilioko Turkana.

Frank-Walter Steinmeier ni rais wa kwanza kabisa wa Ujerumani kuitembelea  Kenya tangu ilipojinyakulia uhuru, mara ya mwisho alipozuru Kenya, alikuwa waziri wa masuala ya mambo ya nje mwaka 2015.

Shisia Wasilwa Dw, Nairobi