Ujerumani yaahidi msaada zaidi wa Ebola kwa DRC
4 Septemba 2019"Hatuwezi kuendelea kutazama tu bila kuchukua hatua wakati virusi vinaendelea kusambaa," alisema Maas wakati akiwa ziarani mashariki mwa Congo, ambapo zaidi ya watu 2,000 wamefariki kutokana na Ebola katika kipindi cha miezi 13 iliyopita na 3,000 wameambukizwa na virusi hivyo.
"Licha ya juhudi kubwa, maendeleo yaliyofikiwa siyo tuliyoyatarajia," alisema Maas, ambaye anapanga kuzungumza na mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uitikiaji wa dharura dhidi ya Ebola David Gressly, na rais wa Congo Felix Tshisekedi kuhusu uwezekano wa msaada zaidi wa kifedha baadae Jumatano.
Ujerumani tayari imetoa dola milioni 4.4 katika msaada wa dharura wa kupambana na Ebola nchini DRC. Zaidi ya hapo, Ujerumani imetoa mamilioni ya dola kwa shirika la afya duniani WHO, Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia, ambazo zinatumiwa kwa sehemu katika mapambano dhidi ya Ebola.
Maas apimwa Ebola Goma
Kama ilivyo kwa wageni wengine wanaozuru Congo, Maas, ambaye yuko katika ziara ya pili ya safari barani Afrika, alipimwa joto lake la mwili baada ya kuwasili Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini siku ya Jumanne jioni.
Joto la juu ni moja ya viashiria vya kwanza vya uwezekano wa maambukizi ya Ebola. Mkoa wa Kivu Kaskazini, ulioko mashariki mwa Congo, umeathirika pakubwa na mripuko wa sasa wa Ebola.
Juhudi za kudhibiti mripuko huo zimetatizwa na mapigano katika eneo hilo, ambako makundi mbalimbal ya wanamgambo yanaendesha shughuli zao, na wafanyakazi na vituo vya afya vimekuwa walengwa wa mashambulizi.
Maas pia amekutana na wanawake waliowahi kuathirika na vurugu za ubakaji na ngono na ambao wanapewa matibabu katika hospitali ya Panzi, na kusema baada ya Daktari Denis Mukwege kuipata tuzo ya Nobel na kutaka wanawake hao walipwe fidia, nchi ya Ujerumani imechukua fursa ya uwepo wake katika baraza la Umoja wa Mataifa kuwajaali waathirika wa ubakaji.
Mukwege anaendesha hospitali katika mji wa Bukavu katika mkoa wa Kivu Kusini, karibu umbali wa kilomita 200 kusini mwa mji wa Goma. Siku ya Jumanne, Maas alizuru taifa la Sudan ambako aliahidi kiasi cha dola milioni 5.5 katika msaada wa ziada kufanikisha ujenzi wa demokrasia nchini humo.
Ahadi hiyo ilikuwa ni nyongeza kwenye msaada mwingine wa kiutu wa dola milioni 11 ambao Ujerumani iliutoa tayari mwaka huu.
Chanzo: dpae