Ujerumani yaamini kanda ya euro itahimili kujitoa kwa Ugiriki
4 Januari 2015Serikali ya Ujerumani inaamini kwamba kanda ya sarafu ya euro itaweza kuhimili iwapo Ugiriki itajitoa kutoka katika kanda hiyo kama itakuwa lazima, jarida la Der Spiegel limeripoti siku ya Jumamosi(03.01.2015), likinukuu vyanzo vya serikali ambavyo havikutajwa.
Kansela Angela Merkel na waziri wa fedha Wolfgang Schauble wanaamini kanda ya euro imetekeleza mageuzi ya kutosha tangu kuzuka kwa mzozo wa kanda hiyo mwaka 2012 na kuwezesha kuhimili vishindo iwapo Ugiriki itajitoa, limeripoti Der Spiegel.
"Hatari ya kuporomoka ni ndogo kwasababu Ureno na Ireland zinaonekana kuwa zimefanikiwa kuufufua uchumi wao," gazeti hilo la kila wiki limenukuu chanzo kimoja kutoka serikalini.
Kanda ya euro haitatetereka
Zaidi ya hayo, mfumo wa uthabiti wa Ulaya (ESM), fuko la kanda ya euro la uokozi , ni mfumo madhubuti wa uokozi na kwa sasa unaweza kutumika, duru nyingine imeongeza. Benki kubwa zitalindwa na umoja wa mabenki.
Serikali ya Ujerumani mjini Berlin haikuweza kupatikana kutoa maelezo. Bado haijafahamika ni vipi mwanachama wa kanda ya sarafu ya euro anaweza kujitoa kutoka sarafu hiyo na bado ikabaki kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya, lakini Der Spiegel limemnukuu "mtaalamu wa ngazi ya juu wa masuala ya sarafu " akisema kwamba "wanasheria wenye ujuzi" wataweza kufafanua hilo.
Kwa mujibu wa ripoti , serikali ya Ujerumani inatafakari kuondoka kwa Ugiriki kwamba hakuwezi kuepukika iwapo chama cha upinzani cha mrengo wa shoto cha Syriza kinachoongozwa na Alexis Tspras kitashinda uchaguzi unaopangwa kufanyika Januari 25.
Chama cha Syriza kinaongoza
Uchaguzi nchini Ugiriki umeitishwa baada ya wabunge kushindwa kumchagua rais mwezi uliopita. Uchaguzi huo ni mpambano kati ya chama cha waziri mkuu Antonis Samaras cha kihafidhina cha New Democracy, ambacho kinatekeleza hatua za kubana matumizi zisizokubalika na wengi chini ya makubaliano ya kuipatia Ugiriki fedha za kuuokoa uchumi wake, dhidi ya chama cha Tsipras cha Syriza, ambaye anataka kufuta hatua za kubana matumizi na kufuta kiasi fulani cha deni la Ugiriki.
Maoni ya wapiga kura yanaonesha kwamba chama cha Syriza kinaongoza dhidi ya chama cha New Democracy, licha ya kuwa kiwango kinachotenganisha vyama hivyo viwili kimepungua hadi asilimia tatu katika wakati wa kuelekea uchaguzi huo.
Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schauble tayari ameionya Ugiriki dhidi ya kwenda kando ya njia ya mageuzi ya kiuchumi, akisema serikali mpya itawajibika kuheshimu ahadi zilizotolewa na serikali ya sasa ya Samaras.
Wakati huo huo waziri mkuu wa zamani wa Ugiriki George Papandreou ametangaza kuunda chama kipya kiasi ya wiki tatu kabla ya uchaguzi wa mapema wa taifa hapo Januari 25.
Papandreou alizindua chama cha Movement of Democratic Socialists jana Jumamosi(03.01.2015) mbele ya maelfu ya wafuasi wake.
Papandreou , mtoto na mjukuu wa mawaziri wakuu waliopita, amejieleza kuwa ni mtu mwenye nia ya kuleta mageuzi dhidi ya mfumo wa kizamani uliojaa rushwa, ambao umesababisha mzozo mkubwa wa kifedha nchini Ugiriki. Alikiongoza chama cha PASOK, kilichoasisiwa na baba yake mwaka 1974, kuanzia mwaka 2004 hadi 2012.
Mwandishi: Sekione Kitojo . rtre / afpe
Mhariri: Amina Abubakar