1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaandaa mkutano wa kilele kutafuta amani ya Libya

Zainab Aziz Mhariri:Tatu Karema
19 Januari 2020

Viongozi wa ulimwengu wanakusanyika mjini Berlin leo Jumapili kujadili mpango mpya wa amani ya nchini Libya. Mkutano huo wa kilele unalenga kuumaliza mzozo katika nchi hiyo na kuiepusha kugeuka kuwa "Syria ya pili".

Libyen | Bundesaussenminister Heiko Maas trifft General Chalifa Haftar
Picha: imago images/photothek/X. Heinl

Wadau muhimu wanakutana Jumapili mjini Berlin kujadili makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Libya yanayoyumba. Wakati huo huo washiriki kwenye mkutano huo wanataka kutafuta njia ya kukabiliana na nchi za kigeni zinazoingilia kati masuala ya nchi hiyo inayokumbwa na machafuko tangu kuzuka ghasia za kuipinga serikali za mwaka 2011 zilizoungwa mkono na nchi wanachama wa jumuiya ya kijeshi NATO.

Ujerumani na Falme za Kiarabu (UAE) zimetoa wito wa pamoja kwa pande zote katika mzozo wa Libya kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa ya kusitisha mapigano ya muda mrefu na kwa vikosi vya kigeni kuondoka nchini humo.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amesema wito huo ulitolewa baada ya kufanyika mkutano kati ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na mwanamfalme wa Abu Dhabi Sheikh Mohammed bin Zayed al Nahyan, kabla ya mkutano wa kilele kuhusu amani ya Libya ambapo viongozi wa kimataifa wanakutana mjini Berlin mnamo Jumapili 19.

Viongozi hao wawili wamesisitiza kwamba mzozo wa Libya hauwezi kutatuliwa kwa njia za kijeshi, bali kwa kudumisha amani na utulivu ambavyo vitafikiwa kwa njia ya mazungumzo. Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan amesema Falme za Kiarabu zingefanya kila jitihada kusaidia utekelezaji wa matokeo ya mkutano wa Berlin kuhusu Libya.

UAE ni mmoja wa washirika muhimu zaidi wanaomuunga mkono kiongozi wa waasi jenerali Khalifa Haftar ambaye vikosi vyake vinadhibiti sehemu kubwa ya Libya na wanaipinga serikali ya Waziri Mkuu Fayez al-Serraj iliyopo katika mji mkuu wa Libya, Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Marais wa Urusi, Uturuki na Ufaransa watafanya mazungumzo yatakayo simamiwa na Umoja wa Mataifa, ambao unataka nchi za nje zenye nguvu na ushawishi mkubwa katika eneo hilo ziache kujiingiza katika vita vya nchini Libya, kupitia utoaji wa silaha, askari au ufadhili wa fedha.

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa anayeshughulikia masuala ya Libya Ghassan Salame pia ametoa wito wa kuondolewa wapiganaji wa kigeni katika nchi iliyoghubikwa na vita kabla ya kuanza mkutano huo wa amani ya Libya unaofanyika katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.

Libya yenye utajiri mkubwa wa mafuta imekuwa kwenye machafuko tangu kuondolewa na kuuawa aliyekuwa rais wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mnamo mwaka 2011. Pande mbili zinazopingana  na makundi mengine kadhaa ya wanamgambo wote wanapigania kuitawala Libya. Serikali ya umoja wa kitaifa inayotambulika kimataifa iko mjini Tripoli wakati jenerali muasi Khalifa Haftar anaunga mkono utawala wa eneo la mashariki mwa Libya.

Mkutano huo wa kilele wa Berlin umeandaliwa kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, anayeongoza mashauriano ya kutafuta suluhisho la amani juu ya mzozo wa Libya pamoja na mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa anayeshughulikia masuala ya Libya Ghassan Salame.

Wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 10 wanatarajiwa kushiriki katika mazungumzo hayo ya amani ya Libya yaliyoandaliwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

Tunisia haitashiriki, kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo na kwamba hatua hiyo ni kutokana na kupokea mwaliko dakika za mwisho kabla ya mkutano huo kuanza.

Tunisia ilikuwa imelalamika hapo awali juu ya kutopokea mwaliko kwa kuzingatia kwamba ni nchi jirani ya Libya ambayo inaathiriwa moja kwa moja na kila kinachoendelea katika nchi jirani yake.

Vyanzo:/AFP/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW